Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kwa kuniona. Kabla ya yote nimponze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya. Hongereni sana, endeleeni kuchapa kazi. Tunajua mna kazi kubwa lakini kazi mnayoifanya nayo ni kubwa, Watendaji wenu wa Wizara tunawapongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuweza kumteua Katibu Mkuu Profesa Kitila ambaye anatokea ACT. Nataka kuwaambia Wapinzani, ukionekana unafaa kwenye CCM kazi utafanya. Usikate tamAa, Bwana Kitila fanya kazi na nina imani wale watakupa ushirikiano mzuri ili utekeleze Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, kwanza kuna ndugu yangu mmoja, Mheshimiwa Kangi Lugola, simwoni hapa, jana alisema watakaopitisha hii bajeti ataenda kupiga miluzi nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mheshimiwa Kangi Lugola ana shibe. Pale Jimboni kwake Mwibara maji yako hatua tano. Anaweza kuamua kuvua samaki wa saa nne, wa saa nane, wa saa tisa; ni kama kata mbili hazina maji. Yeye maji yamemzunguka. Ila namshauri, akitaka kupiga miluzi, apige kule Mwibara, akivuka geti sisi kwenye Chama tutamdhibiti. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest, mimi kabla ya kuwa Mbunge nilikuwa Mjumbe wa Bodi ya DAWASA. Waheshimiwa Wabunge, mliochangia naomba nikwambieni wazi, tunaweza tukachangia lakini hujaingia ndani ya nyumba kujua kuna nini? DAWASA imeundwa kwa mujibu wa Sheria; DAWASCO anakasimiwa Mamlaka na DAWASA.
Mheshimiwa Naibu Spika, historia inaonesha, huko nyuma tulikuwa na kitu kinaitwa NUWA. Tukaiondoa NUWA kupunguza mzigo, ikaja City Water na DAWASA. City Water akafeli, alivyoondoka DAWASCO akapewa nafasi hiyo ili aichukue kwa mkataba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yanasemwa hapa, kwamba nani mzuri? Haiwezekani mwenye nyumba akawa sio mzuri, mpangaji akawa mzuri. Sisi wote tunaishi Dar es Salaam, kazi kubwa aliyonayo DAWASCO ni kukusanya kutengeneza matengenezo madogo, akishapata zile bili kutoka kwa watu, anapata pesa; lakini anayetengeneza miundombinu ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, anaitwa DAWASA. Kwa hiyo, haiwezekani mtu akatengeneza miundombinu, wewe ukakusanya pesa, ukaonekana uko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara na Serikali yangu, hebu tuwe makini. Msemaji wa saa hivi amesema, anaipongeza REA na TANESCO. Kwa nini imetoka TANESCO tukaenda REA? Kwa nini? Unaipunguzia mzigo TANESCO; REA imepatikana, inafanya kazi zake vizuri. Leo mna mpango wa kuiunganisha, naomba Wizara muwe makini sana, tusije tukarudi tulikotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo TANROAD ipo kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi. Kwa nini hatusemi Wizara ya Ujenzi iende ijenge? Leo tunataka kuanzisha Mfuko wa Maji Vijijini, kwa nini tunauanzisha mfuko? Suala hili ni kumwondolea mtu mzigo mkubwa ili angalau wafanye wengi, ufanisi uweze kupatikana. Leo kwa Dar es Salaam ufanisi upo. Maji yanatosha, DAWASCO wapo, DAWASA wapo, hili neno linatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, wazo lenu labda ni zuri sana, lakini mrudi kwenye historia, kwa nini tulitoka huko na tukafika hapa? Kama hatukwenda vizuri, tunataka kuanzisha mgogoro mpya katika Jiji la Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam leo limepanuka, lilikuwa na Wilaya tatu, leo lina Wilaya tano; watu wameongezeka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tena niseme, kwa sababu ukienda kwa DAWASA leo, ndani ya Ilani yangu ya Chama cha Mpinduzi tumesema katika ukurasa wa 106 kwamba tutajenga bwawa la Kidunda. Ni DAWASA hiyo!
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kuna tatizo la TANESCO kukata umeme kwenye Mamlaka za Maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini wananchi hawadaiwi, anakuwa anadaiwa Mamlaka za Maji; sasa mkikata maji kule TANESCO mnawaumiza wananchi kwenye miji!