Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimia Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kuniona. Bila kupoteza muda naomba pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa ndugu zetu ambao wamepoteza wapendwa wetu kule Mkoani Arusha. Pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naungana na kaka yangu kiongozi wangu Mzee Bulembo kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kumchagua Profesa Kitila, Mwalimu wangu. Naomba nimtakie kazi njema ya kututumikia Watanzania, naamini hutotuangusha katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika mambo machache yanayohusu eneo la Jimbo langu la Nachingwea. Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa nyakati tofauti wamefika katika Jimbo la Nachingwea, wameona hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji vya Jimbo la Nachingwea. Hapa kuna mradi mkubwa wa Mbwinji ambao unahudumia Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Nachingwea pamoja na Wilaya ya Rwangwa.

Mheshimia Naibu Spika, iko ahadi, vile vile iko fedha ambayo mwaka 2016 tulitengewa kwa ajili ya kusambaza maji katika vijiji ambavyo viko umbali wa kilomita tano. Naomba kupitia nafasi hii, niwakumbushe juu ya hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji vinavyozunguka Jimbo la Nachingwea. Tafadhali sana naomba wayafanyie kazi maombi ambayo tayari yako katika ofisi yao kwa ajili ya kutoa fedha ambayo tayari ilishapitishwa katika bajeti iliyopita ili tuweze kuwapa wananchi maji ya uhakika na maji salama ambapo wamekuwa wanapata shida kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Naipanga, Mkotokwiana, maeneo ya Chemchem, ni maeneo ambayo wanaathirika kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hiyo, utekelezaji wowote utakaofanyika, basi tutakuwa kweli tumekwenda kuwatua mama zetu ndoo kichwani kwa ajili ya kuwapunguzia adha wanayoipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala la ulipaji wa bili za umeme. Ndani ya Wilaya yangu ya Nachingwea, zaidi ya wiki mbili tumekaa bila kupata maji kwa sababu ya umeme, ambapo kimsingi siyo kosa la wananchi. Wananchi wanalipa bili zao, lakini wamelazimika kukaa bila maji kwa sababu tu Wizara imeshindwa kulipia bili ambazo kimsingi wananchi hawahusiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na timu nzima kwamba jambo hili kwa kweli tusingependa lijurudie kwa sababu tunawapa adhabu wananchi ambao wao wanatimiza wajibu wao wakulipia bili zao za maji. Kwa Wilaya ya Nachingwea peke yake kupitia MANAWASA, zaidi ya shilingi milioni 100 zinatakiwa zilipwe. Kwa hiyo, naomba tafadhali hiyo fedha ilipwe ili wananchi wa Jimbo la Nachingwea waweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Maji, kupitia Naibu Waziri ambaye alishakuja Jimboni Nachingwea, alikuja katika Kijiji cha Chiola, nafikiri anakumbuka ule mradi; na kuna ahadi ambayo aliitoa na wale wananchi wananiulizia: Ni lini utekelezaji wa yale ambayo tayari aliyaahidi pale ya kuleta wataalam kuja kuchunguza ule mradi? Ni lini tutakwenda kuukamilisha? Sina majibu, namwomba mzee wangu kwa sababu tumefanya kazi nzuri katika Jimbo hili, tafadhali sana anisaidie ili wale wananchi waweze kupata maji ya uhakika na maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo nataka nilizungumzie ni suala la Miradi ya Umwagiliaji. Katika Jimbo la Nachingwea, tunayo miradi miwili; tunao Mradi wa Matekwe, huu ulishapewa fedha kipindi cha nyuma zaidi ya shilingi milioni 500, lakini mpaka sasa hivi mradi huu sijauona hata kwenye kitabu unatajwa kwa namna yoyote; sijui kama umefutwa! Zile fedha zilizotolewa kama zimepotea, basi tunaomba tuelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.