Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja zangu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa Walimu hauwiani katika ya shule za mijini na vijijini ambapo katika Wilaya ya Kilosa Shule ya Msingi Mabwegere kwa zaidi ya miaka 10 ilikuwa na Mwalimu mmoja hali iliyosababisha baadhi ya wazazi wasio na taaluma ya elimu kujitolea kwenda kufundisha watoto wao, hali hii ilisababisha shule hiyo kushindwa kufanya vizuri. Ipo haja ya kuangalia upya mgawanyo huu wa Walimu badala ya kurundikana katika Manispaa ya Morogoro wakati Wilayani hakuna Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la X-ray mashine katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro unategemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili kutoa huduma za matibabu zilizoshindikana katika Wilaya saba za Mkoa lakini X-ray mashine iliyopo imenunuliwa zaidi ya miaka 14 iliyopita na haina ufanisi hali inayolazimu wagonjwa kwenda nje ya hospitali (private) kufanya kipimo hiki. Aidha, kutokana na matukio mengi ya ajali wajeruhi pia wanategemea hospitali hiyo. Naomba Serikali ione umuhimu wa kununua X-ray machine mpya kwa ajili ya hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya zahanati zimefunguliwa na Mwenge miaka mitano iliyopita na baada ya Mwenge zimefungwa badala ya kutoa huduma kwa wananchi licha ya kuwa zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Mfano wa zahanati hizi ni Bigwa iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la mafuriko ya mara kwa mara katika Mto Mkondoa, Wilayani Kilosa. Serikali iliahidi tangu mwaka 2010 kuwa wangejenga tuta ili kuzuia mafuriko lakini mkandarasi alipewa fedha kazi haijaisha na wananchi wanaendelea kupata madhara makubwa ya nyumba kujaa maji kila msimu wa masika pamoja na kusomba reli ya kati maeneo ya Godegode.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa TASAF katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero, baadhi ya kaya zisizo maskini zimepewa fedha bila utaratibu na wenye shida na maskini wanakosa nafasi hizo. Ipo haja kwa watathmini wa TASAF kufanya upya uhakiki wa kaya maskini zinazostahili kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wa Viti Maalum kukosa ofisi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kama Waziri wa TAMISEMI alivyoeleza Bungeni. Ipo haja ya Waziri wa TAMISEMI kuwaandikia Wakuu wa Mikoa kutoa ofisi hizo ili kuwezesha Wabunge wa Viti Maalum kufanya kazi zao za kisiasa kwa wananchi badala ya kutumia ofisi za chama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji wa watumishi wa umma bila kutumia haki za msingi za binadamu. Tumeshuhudia Serikali ikiwafukuza watumishi kwa madai ya kutumbua majipu, hatupingani na utumbuaji huu, lakini haki za msingi za binadamu zizingatiwe. Mfano, Mkurugenzi Kabwe wa Dar es Salaam kutumbuliwa mbele ya mkutano wa hadhara bila kujali staha yake, familia, mke, watoto na marafiki, hali hii ni ya kukemewa. Utaratibu mwingine ungeweza kufuatwa kwa Waziri mwenye mamlaka kumshughulikia badala ya kumuaibisha hadharani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji huu wa watumishi umewakumba pia Mabalozi ambao walipewa saa 24 wawe wamerudi nchini. Lazima haki za mtumishi zizingatiwe mfano kuangalia utu na familia. Mfano, kuna watoto ambao wapo shuleni nje ya nchi na wazazi wao bila kumpa muda wa kujiandaa kuhamisha familia inakuwa sio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuiaji wa vyombo vya habari kufanya kazi zake mfano waandishi wa TV hawaruhusiwi kuingia Bungeni na kamera badala yake wanapewa taarifa ambazo ni edited. Huu ni ukiukwaji wa Katiba na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi juu ya Bunge lao linaloendeshwa kwa kodi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama kubwa za Mwenge. Mwaka huu uzinduzi wa Mwenge umefanyika Mkoani Morogoro ambapo tumeshuhudia kila halmashauri zimeelekezwa kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi hayo na halmashauri zote zimetoa fedha za wananchi na kuzipeleka katika shughuli za Mwenge. Kama hiyo haitoshi Walimu wa shule za msingi na sekondari wamelazimishwa kutoa mchango wa Sh.10,000 ili kuchangia maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge. Hii si sahihi, si haki fedha za wananchi walipa kodi kutumika kukimbiza Mwenge ambao bado hauna tija kwa wananchi huku wanafunzi wakikosa masomo ili kuhudhuria shughuli za Mwenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hewa kudumu katika Wizara mbalimbali kwa miaka mingi ni udhaifu kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana na Serikali. Badala ya kuwakamata watuhumiwa pekee ni muda muafaka kuwatia hatiani wasimamizi na maafisa wa idara tofauti walioshindwa kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo la Rais kuhusu watumishi kulipwa mshahara usiozidi milioni kumi na tano ni lini utekelezaji huu utaanza?