Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kukushukuru wewe na kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kunipa fursa ya kusimama na kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu ya maji ambayo ndiyo uhai wa mwanadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja; na sababu zangu za kuunga mkono hoja hii ni kama zifuatazo:-

Kwanza, taarifa ya Waziri juu ya utekelezaji wa kazi zilizofanyika mwaka 2016/2017 na mpango wa utekelezaji wa kazi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imeandaliwa vizuri na hasa kilichonivutia ni taarifa ya hatua iliyofikiwa ya kila mradi wa maji ukiachilia mbali ile miradi michache iliyosahaulika.

Pili, naunga mkono kwa kuwa Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais - Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa K. Majaliwa, wanaonesha kwa vitendo dhamira ya CCM na dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuwatua wanawake ndoo kichwani. Pamoja na pongezi, naomba nijielekeze kutoa ushauri kwa Serikali katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kupeleka fedha za maendeleo, bado Serikali haijapeleka fedha za kutosha katika miradi ya maendeleo. Hadi Machi, 2017 Serikali ilikuwa imepeleka shilingi bilioni 181.2 sawa na asilimia 19.8 tu. Ni ukweli usiopingika kuwa upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo uko chini sana, hivyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya maji unakwama kwa sababu hakuna fedha za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, kama kweli ina dhamira ya kuwatua ndoo wanawake kichwani, basi ni lazima Serikali ihakikishe kuwa inapeleka fedha zote zilizotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya miradi ya maji iliyopangwa kwa mwaka wa fedha husika. Hapa
nashauri, fedha ambazo hazijapelekwa zipelekwe sasa kabla ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono pendekezo la Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji la kuongeza sh.100/= ya kila lita ya petroli na dizeli. Natoa ushauri huu kwa sababu tozo ya sh.50/= ya dizeli na petroli inayotolewa sasa imeleta matokeo mazuri sana ya miradi ya maji. Hivyo, tukiongeza tozo ikawa sh.100/=, kasi ya ujenzi wa miradi ya maji itaongezeka na dhamira ya Mheshimiwa Rais na CCM ya kuwatua ndoo wanawake kichwani itatekelezwa na wanawake wataachana na adha wanayopata ya kutembea masafa marefu kwenda kutafuta maji badala ya kufanya kazi zitakazowakomboa kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia fedha zitakazopatikana kutokana na tozo zipelekwe mapema katika miradi ya maji iliyopo vijijini ili kuwatua akinamama ambao hasa ndio wanaoathirika zaidi na shida ya kukosa maji. Katika kitabu cha maoni ya Kamati ukurasa wa 15 inaonesha kuwa asilimia 46 tu ya wakazi wa vijijini ndiyo wanapata maji safi na salama. Kwa hiyo, fedha za tozo kwenye mafuta zielekezwe kusaidia upatikanaji wa maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwashukuru Serikali na BADEA na SFD kwa mpango uliopo wa kutekeleza Mradi wa Mugango na Kiabakari (Butiama) kwa Dola za Kimarekani 30.69 ingawa mradi huu mpaka sasa haujaanza kutekelezwa. Pamoja na kuishukuru Serikali na Wadau kwa hatua zinazoendelea za kumpata Mkandarasi na kupeleka taarifa hizo BADEA kwa ajili ya kupata kibali cha ujenzi unaotarajiwa kuanza mwaka 2017/2018. Hapa naomba niseme kwamba, mradi huo umechukua muda mrefu kuanza, kiasi kwamba wananchi wanakaribia kukata tamaa juu ya mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kwa Serikali; kwa kuwa mpango wa mradi huu ni wa muda mrefu na mpaka sasa wananchi wanaelekea kukata tamaa na mradi huu, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie hawa wadau wetu wa maendeleo watatoa lini hicho kibali na mradi uweze kuanza ili wananchi zaidi ya 80,000 waweze kupata maji safi na salama? Je, kama wadau wetu hawako tayari kutoa fedha hizi, Serikali ina mpango gani juu ya kutoa fedha ili mradi uanze bila kutegemea fedha za wafadhili?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mradi wa Maji – Mji wa Musoma, naishukuru Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Musoma kwa gharama ya shilingi bilioni 45 ambapo mradi unalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 10.14 za sasa hadi kufikia lita milioni 34 kwa siku ambazo zitakidhi mahitaji ya wananchi wa Musoma hadi mwaka 2025 na utekelezaji wa mradi umefikia kiwango cha asilimia 90. Tunashukuru sana. Pamoja na shukrani hizi, naomba kushauri yafuatayo juu ya mradi huu:-

(i) Ijengwe miundombinu ya maji ili wananchi waliopo kwenye chanzo cha maji cha Kata ya Etaro, Nyigina wapate maji kutokana na chanzo hiki; na

(ii) Pia kwa kuwa matenki ya maji yanaweza kuhifadhi maji mengi, nashauri ijengwe miundombinu itakayopeleka maji haya Kata ya Nyakanga, Bukabwa na Butiama kwa kuwa wataalam wa mradi huo wanasema inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kujenga miundombinu ya maji katika mradi wa Dar es Salaam na Pwani. Naipongeza DAWASA na DAWASCO kwa kusimamia mradi huu kwa kiwango cha hali ya juu. Pamoja na pongezi hizi, naishauri Serikali ihakikishe mradi huu unawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Pwani, Kisarawe, Mkuranga, Bagamoyo na Kibaha kwa sababu vyanzo vya maji vya miradi hii viko Mkuranga na Kibaha na matenki ya maji yamejengwa Kisarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Bwawa la Kidunda ni wa muda mrefu takriban miaka 20 mradi haujaanza. Napenda kujua Serikali ina mkakati gani ili kuhakikisha mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu uvunaji wa maji ya mvua na kilimo cha umwagiliaji. Napenda kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Maji ije na mpango wa kuvuna maji kwa kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji hasa katika Mikoa ya Kanda ya Kati kama vile Singida, Dodoma na Shinyanga. Uvunaji wa maji ya mvua utasaidia kukuza kilimo cha umwagiliaji hapa nchini hasa katika mikoa ambayo imekuwa haipati mvua za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, katika Mkoa wa Dodoma kumekuwa na ongezeko kubwa la watumishi kuhamia Dodoma ambapo zaidi ya watumishi 2000 wamehamia Dodoma huku chanzo cha maji kikiwa ni kile kile cha Mzakwe. Sambamba na hilo ujenzi wa mabwawa kama vile bwawa la Farkwa umekuwa ukisuasua. Katika mwaka 2017/2018, Serikali iendelee kufanya utafiti ili kupata vyanzo vipya vya maji ili kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji bado kuna changamoto ya kupeleka fedha katika miradi ya umwagiliaji. Katika kitabu cha maoni ya Kamati inaonesha kuwa Serikali ilipeleka asilimia tatu tu kwa mwaka 2002, lakini kwa mwaka 2003 na 2004 Serikali haikupeleka hata shilingi moja pamoja na kuwa bajeti ya umwagiliaji ilitengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.