Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunatambua kuwa maji ni uhai katika maisha ya mwanadamu, maji ni maendeleo, maeneo ambayo hakuna maji hakuna maendeleo na asilimia kubwa ya shughuli za kijamii na kiuchumi zinategemea uwepo wa maji. Naishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza tozo ya maji kwa lita moja ya petroli na dizeli kutoka Sh.50/= hadi Sh.100/= ili kutunisha Mfuko wa Maji ambao umekuwa mkombozi mkubwa wa maendeleo ya miradi ya maji maeneo mengi nchini lakini wanufaika wengi wamekuwa ni wale wanaoishi mijini. Nashauri Serikali itazame zaidi maeneo ya vijijini angalau kupeleka 70% ya makusanyo ya tozo ya Mfuko wa Maji maeneo ya vijijini ambapo ndio kwenye shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama maji yanapatikana wakati wote wanawake wa Mkoa wa Singida ambao ni wachapakazi na wabunifu wanaweza kutumia fursa hii kwa kulima mazao ya chakula na biashara kwa mwaka mzima. Hata hivyo, kwa Mkoa wa Singida mambo yamekuwa sivyo ndivyo pamoja na adha kubwa wanayoipata wananchi wa Singida kutokana na ukosefu wa maji safi na salama na changamoto nyingi za maji katika Mkoa wa Singida bado bajeti ya miradi kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018 imepunguzwa ambapo tumetengewa shilingi bilioni 4.7 tofauti na mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo tulipewa shilingi bilioni 6.7 jambo hili si sawa. Naiomba Serikali yangu kuangalia upya bajeti hii na kuiongeza kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mosi, Singida ipo katikati ya nchi na ni mkoa unaokuwa kwa kasi, unategemea vyanzo vya maji ya visima virefu na vifupi ambavyo maji yake ni ya chumvi na hata hivyo hayakidhi viwango vya mahitaji. PiIi, hali ya hewa ya Mkoa wa Singida ni kame hivyo ingetakiwa kupewa kipaumbele katika miradi mikubwa ya maji. Maeneo mengi ya Mkoa wa Singida yanakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama na tatizo hili limekuwa ni la muda mrefu licha ya Serikali kuambiwa tatizo hili mara kwa mara bila kulipatia ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi Mkoa wa Singida hususan wanawake wameteseka sana na adha kubwa ya ukosefu wa maji. Ni vyema Serikali ikasikia kilio cha wakazi wa Mkoa wa Singida na kuchukua hatua madhubuti na za haraka kumaliza tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaliwa kuwa na mito mikubwa, maziwa na bahari, ni lini tutatumia kikamilifu rasilimali hizi? Ni kwa nini tusitumie vizuri uwepo wa Ziwa Manyara ambalo lipo umbali wa kilomita 177 kuvuta maji kuja Singida ama kutoka Ziwa Viktoria kupitia Tabora, Nzega, Igunga hadi Singida? Tutaendelea kuwatesa wanawake wa Mkoa wa Singida mpaka lini na kuhatarisha ndoa zao kwa kutoka usiku kufuata maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama bado kuna changamoto nyingi zinazoikabili Idara ya Maji ya Mkoa wa Singida (SUWASA). Changamoto hizo ni ukosefu wa vitendea kazi, uhaba wa watumishi na ucheleweshaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji. Ni jambo la kushangaza mkoa ambao unatakiwa kupewa kipaumbele kutokana na jiografia yake lakini unaongoza kwa uhaba wa watumishi. Kuna wahandisi 12 tu lakini wanaohitajika ni wahandisi 28, mafundi sanifu wanaotakiwa ni 52 ila waliopo ni 20 na kwa kuwa kazi nyingi za miradi ya maji ni field work sasa kwa mazingira haya tutafanikisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa mzima hauna GPS machine, kuna magari matatu ambayo yapo juu ya mawe na pikipiki moja tu. Je, kwa staili hii kazi zinaweza kufanyika kweli kwa ufanisi? Mkoa wa Singida unahitaji crane truck 15, computer nane, GPS machine sita, pikipiki 10 ili kuwezesha maofisa wa maji kufika wilayani na vijijini kutatua kero ya maji na hata Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji- Singida (SUWASA) hana gari. Naomba Serikali ipeleke vitendea kazi ili kuwawezesha wananchi wa Mkoa wa Singida kupata huduma bora za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya miradi ambayo tuliamini ingekuwa mkombozi wa wananchi wa Singida lakini mingi imekwama kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu na ucheleweshwaji wa fedha kutoka Serikalini. Kuna miradi ambayo tayari imeshafanyiwa usanifu ya Manyoni na Kiomboi lakini haijapata fedha mpaka sasa. Miradi mingine ni ya Mkwa, Iyumbu, Ulyampiti na Sepuka ambapo inasubiri fedha toka Serikalini. Niishauri Serikali ipeleke fedha kwa wakati ili kukamilisha miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Singida Vijijini na Wilaya ya Manyoni ni wilaya zinazokabiliwa na upungufu na ukosefu mkubwa wa maji safi na salama na wakazi wake wanategemea zaidi maji ya visima virefu na vifupi. Mfano, Wilaya ya Singida visima vyake vingi ni vibovu na miundombinu yake ni chakavu ambayo haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa fedha na kutopelekwa fedha hizo. Ukarabati wa miradi ya visima vifupi na virefu ambavyo vilikuwa vinafadhiliwa na fedha za WDPS kutoka Serikali Kuu, fedha hizi kwa muda mrefu hazijaletwa. Sasa ni vyema Serikali ikaangalia uwezekano wa kupeleka fedha hizo ili wananchi wa Mkoa wa Singida wa Wilaya ya Singida Vijijini waweze kupata huduma bora za maji ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuelezea changamoto hizi hapo juu, naunga mkono hoja na nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu Waziri wa Maji, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa namna ambavyo wanashughulika kutatua kero ya maji pamoja na changamoto zinazoikabili Wizara yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.