Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napongeza Wizara na Serikali kwa kuwasilisha hotuba na utekelezaji wa miradi 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgao wa bajeti za Halmashauri. Ukifuatilia mgao wa bajeti kwenda katika Halmashauri kwa vyanzo vya ndani unahitaji marekebisho kwa uhitaji na matatizo ya kila Halmashauri hayakuzingatiwa ipasavyo. Mfano Nsimbo, 34% ya watu ndiyo wanaopata maji. Hivyo basi, tunashauri Wizara igawe Sh.1,000,000,000 kwa kila Halmashauri ambapo itakuwa Sh.185,000,000,000 kwa idadi ya Halmashauri 185.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia mgao huo, kila Halmashauri itaweza kutatua kwa kiasi matatizo ya maji. Baada ya mgao huo, ndipo Wizara iongeze kwa kila Halmashauri kulingana na miradi mikubwa na kero za maji kwa eneo husika. Vilevile ni muhimu kwa Wizara kuangalia idadi ya watu ambao hawapati huduma ya maji na kuwapatia mgao ambao utatatua kwa kiasi tatizo la maji kwenye eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maji ya 2002 iliyoeleza kwamba wananchi wapate maji ndani ya mita 400 bado ufanisi wake haujaonekana. Hivyo, sera hii ifanyiwe utafiti na kuwe na kigezo cha kugawa fedha kwa Halmashauri ambazo hazijafikia malengo ya Sera ya Maji, kigezo cha mita 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maji Vijijini. Ni muhimu sana Serikali kuboresha Mfuko wa Maji Vijijini kwa kuwa ndiyo maeneo ambayo wananchi wanateseka sana kwani ndiyo ambao hawapati maji. Hivyo basi Sh.50 kwa kila lita katika mafuta iongezwe na fedha ipatikane kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maji vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya umwagiliaji. Serikali ifanye ufuatiliaji wa miradi ya umwagiliaji. Mfano Mradi wa Kijiji cha Katambike, Kata ya Ugala, Halmashauri ya Nsimbo - Katavi mpaka sasa bado haujaanza kufanya kazi na haujakamilika. Hivyo, tunaomba Serikali ifanye haraka kumalizia mradi huo ili wananchi wafaidike.

Mheshimiwa Naibu Spika, vizibo vya umwagiliaji. Serikali ikamilishe kizibo cha Mwamkuli katika Manispaa ya Mpanda. Pia Serikali iendeleze vizibo vile ambavyo vimejengwa na watu binafsi ili wananchi wa Kata ya Itenka ambao wanalima zao la mpunga waweze kufaidika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.