Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Chemba, Wilaya ya Chemba, vipo visima kadhaa katika Kijiji cha Mondo, Daki, Chandama, Mapango, Machiga na Pangai ambavyo vimechimbwa huu ni mwaka wa pili Serikali haijatoa fedha kukamilisha miundombinu ili watu wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili mradi wa maji wa Ntomoko bado unasuasua na kuna dalili kwamba mradi huu hautakidhi haja ya vijiji 13 kama ilivyopangwa awali. Naiomba Serikali isimamishe kutoa shilingi milioni 800 zilizobaki kulipwa mkandarasi na zipelekwe Chemba ili zitumike kuchimba visima katika Vijiji vya Hamai, Chivuku, Kirikima, Songolo na Madaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naishauri Serikali sasa ijenge mabwawa mawili katika Vijiji vya Itolwa na Chivuku ambapo maji ya mvua yanapotea sana na hiyo itaondoa kabisa tatizo la maji katika eneo hili la Lower Irangi. Eneo hili limekuwa na shida kubwa ya maji lakini kama hatua hiyo itachukuliwa ni dhahiri tatizo hili litakuwa limekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Jumuiya ya Watumia Maji (COWSO) liangaliwe upya kwani sera hii imekuwa na tatizo kubwa na wananchi au Kamati za Maji hazina utaalam na matokeo yake miradi mingi inakufa. Nashauri Halmashauri za Wilaya zichukue jukumu la kusimamia mradi huu badala ya COWSO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya mradi wa maji ya bwawa la Farkwa imeanza. Naiomba Serikali ikamilishe malipo ya wananchi wa Mombose na Bubutole haraka ili kuepusha watu wanaoweza kufariki kabla ya kulipwa na matokeo yake watu wanashindwa wakawazike wapi kwa sababu tathmini ya makaburi inakuwa imeshafanywa. Naomba Serikali kabla ya kuleta maji Dodoma ianze na Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba ambapo tatizo la maji ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.