Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maji ni uhai na kichocheo kikuu cha uchumi wa Taifa. Watu wanapokosa maji safi na salama ni tatizo katika Taifa. Wanafunzi wanapokosa maji kwa wakati wanaathirika kwa uchafu katika mazingira yao na husababisha kufeli kwa sababu katika mabweni wanafuata maji mbali sana. Kata ya Misunkumilo wanafunzi wa Mpanda Girls wanapokosa maji wanasafiri karibuni kilometa tano kufuata maji katika shule ya Milala Sekondari au Bwawani, usalama mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji kuchelewa kwisha. Hili ni tatizo kabisa. Miradi Katavi inachukua muda mrefu kwisha, je, ni utaratibu gani unatumika ili kuokoa hela hizi za wananchi na huku miradi inaharibika? Kwa mfano, Mradi wa Maji Kata ya Mwamapuli Wilaya ya Mlele – Katavi na Mradi wa Maji na Umwagiliaji Kata ya Ugala.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha namna gani Serikali haikujipanga katika miradi hii, mmetumia pesa nyingi lakini mpaka sasa miradi haifanyi kazi. Je, ni lini mtakamilisha miradi hii kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Ikonongo katika Manispaa ya Mpanda; ni lini mradi huu utakamilika? Wizara waache maneno mengi waseme ni lini watakamilisha mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu UDOM. Mfumo wa maji taka na mabweni uko karibu lakini pia mradi huu umekwama, mabweni hayapati maji wakati Serikali imewekeza pesa nyingi sana. Je, nini mkakati wa dharura kukinusuru Chuo Kikuu UDOM?
Mheshimiwa Naibu Spika, Ufisadi katika Miradi ya Maji; kwa kuendelea kuona miradi ikisimama na bado wananchi hawapati maji na wananchi kukosa majibu ya maswali yao kuhusu ukosefu wa maji inaonesha ni namna gani hawa wakandarasi wameamua kuwatesa wananchi. Serikali itoe majibu ili wananchi wajue mbaya wao ni nani kati ya Serikali au mkandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyanzo vya Maji Kuharibiwa Vizibo. Naishukuru Serikali kwa kuchukua hatua ya kuvunja vizibo ambavyo havijafuata utaratibu wa kupata leseni na kufuata utaalam katika ujenzi katika Mkoa wa Katavi. Sasa nini kifanyike? Kuvunja vizibo hivi kusiwe na ubaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ni Ndogo, iongezwe. Uhitaji wa maji ni muhimu kuliko kitu chochote. Ukosefu wa maji safi na salama umeleta usumbufu, magonjwa na vifo kwa watoto wachanga kuharisha kwa kunywa maji machafu, homa ya matumbo, kuugua typhoid na kufariki kwa rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, nini hatua ya dharura Wizara ikishirikiana na mamlaka husika za maji katika mikoa ili kunusuru maisha ya Watanzania huku mkishirikiana na Wizara ya Afya ili tuondoe kero hii kwa wananchi?