Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kutoa mapendekezo yangu kuhusu Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Ni ukweli usiopingika kuwa suala la maji bado ni changamoto hususan kwa Watanzania waishio vijijini. Hivyo ni lazima kama Serikali kuja na mipango kabambe inayotekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha kwamba Bajeti ya Maji ambayo imekuwa ikitengwa haitoshelezi kulingana na mahitaji halisi ya Watanzania lakini tatizo kubwa ni kuwa fedha hiyo huwa haitolewi yote kama inayoidhinishwa na kupitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kupitia Wizara ihakikishe kuwa fedha inatolewa kama iliyoidhinishwa na hii kwa sababu maji ni uhai na kwamba bila maji hakuna maisha. Ni vyema Serikali ikabuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni vyanzo vya ndani na ambavyo ni vya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo naungana na maombi na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi juu kuongeza tozo ya sh.50/= na kuwa sh.100/= kwenye kila lita moja ya mafuta ya diesel na petrol ili kuwezesha miradi mbalimbali ya maji kuweza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuonesha kuwa Serikali iko committed katika kumaliza tatizo la maji hususan vijijini ambako ndiko hasa changamoto ya maji iko kubwa, nashauri katika hayo makusanyo yatakayopatikana baada ya kuongeza tozo ya sh.50/= ni vyema asilimia 70 ya fedha hiyo ikaenda vijijini na asilimia 30 ikaenda mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri kuwa ile sera ya uvunaji maji ni vyema Serikali sasa ikalitilia mkazo na kuhakikisha kwamba kila Halmashauri inatoa maelekezo ya kuhakikisha wananchi wetu wanapojenga nyumba wakumbuke kuweka system ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niombe itakapoongezwa tozo ya sh.50/= Wizara iangalie pia Mkoa wa Songwe ambao ni mpya na unakabiliwa na upungufu wa maji hususan kwa vijijini. Wanawake wanapata shida sana, mfano Wilaya ya Mbozi, Kata ya Vwawa na Mlowo, shida ya maji ni kubwa mno. Mheshimiwa Waziri wa Maji alituahidi kutuletea mradi mkubwa wa maji lakini mpaka sasa hatujui mpango huo umefikia wapi. Pia, naomba watukumbuke kutuletea mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Tunduma, lakini pia Wilaya ya Ileje na Wilaya ya Songwe.