Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na siha njema sisi sote katika Bunge lako Tukufu. Pili, nipende kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali na watendaji wote hasa wa Wizara hii muhimu ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kujitahidi kumtua mwanamke ndoo kichwani kama ilivyo ahadi ya chama chetu cha CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri shahiri hakuna asiyejua umuhimu wa maji katika muktadha mzima wa afya bora, uhai na maendeleo endelevu ya kila familia. Hii ni kutokana na kwamba hata mwili wa binadamu tu una asilimia 75 ya maji, hivyo maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Serikali inafanya kila iwezalo ili kumaliza kero ya maji katika maeneo mengi nchini. Binafsi ningeshauri tozo ya mafuta ifikie sh.100/= kwa kila lita moja ya diesel/petrol; iongezwe kwenye Mfuko wa Maji ili wanawake waweze kuondokana na kero ya kutafuta maji kwa masaa mengi, hali inayosababisha ndoa zao kuvunjwa, kukosa muda wa kufanya shughuli nyingine za ujasiriamali ili waweze kujikimu kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisikitike tu kuwa pamoja na bajeti ya maji iliyotengwa katika bajeti ya 2016/2017 kufikia zaidi ya bilioni mia tisa, bado fedha zilizopelekwa hadi Aprili mwaka huu kuwa asilimia 20 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote wanaomba kuongezwa fedha hizo zilizopungua hadi bilioni mia sita katika bajeti hii ya mwaka 2017/2018. Naomba nitofautiane nao kimtazamo kwani hata hizo bilioni mia tisa zilizotengwa hazikupelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali yangu Tukufu kwamba, kwa kuwa kuna Halmashauri takriban 185 nchini, basi haidhuru kila Halmashauri ingetengewa shilingi bilioni moja ili kupunguza makali ya kero ya maji katika kila Halmashauri, halafu bajeti tengwa ya zaidi ya bilioni mia nne zielekezwe kwenye miradi maalum (mikubwa). Hii itaondoa malalamiko mengi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie hali ya maji katika Mkoa wangu wa Manyara. Naomba kwa moyo wa dhati kabisa niishukuru Serikali yangu kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji kwa kuupatia fedha Mradi wa Maji wa Mto Ruvu katika Wilaya ya Simanjiro ambapo wakandarasi wapo site na kazi inaendelea vizuri sana. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba ahakikishe fedha zinaendelea kupelekwa na pia kuhakikisha mkandarasi anafanya mradi huu kwa umakini mkubwa na (value for money) thamani halisi ya fedha inayolingana na mradi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua wananchi wa Simanjiro kwa aina ya jiografia ya wilaya, pamoja na mkoa wetu kuwa ni mkoa wa wafugaji bado tuna mahitaji makubwa ya maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na wanyama pia. Wakati Waheshimiwa Wabunge wakiomba Wizara hii kuongezewa fedha, ndipo na mvua kubwa inaendelea kunyesha kiasi cha kusababisha madhara makubwa kwa wananchi pamoja na miundombinu hapa nchini. Binafsi najiuliza ni kwa nini Wizara isijiongeze na kuchimba mabwawa wakati wa kiangazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, mabwawa hayo yangeweza kutega maji hayo yanayopotea bure kipindi hiki cha masika. Haiwezekani tunalia ukame majira yote ya mwaka wakati tungeweza kuepuka baadhi ya kero isiyo ya lazima kwa kukusanya maji ya mvua kwenye mabwawa na majosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshauri pia Halmashauri zetu zitengeneze Sheria Ndogo (bylaws) zitakazowezesha kila nyumba, kaya yenye paa la bati kuwa na mfumo wa kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kupunguza makali ya kutafuta maji mbali kipindi cha kiangazi. Naomba niendelee kushauri kuwa katika sh.100/= hii, asilimia 70 iende vijijini na asilimia 30 iende mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyejua adha kubwa wanayoipata akinamama wa vijijini ambao wanatumia asilimia 80 ya muda katika kutafuta maji ya ndoo moja au mbili kwa kutwa nzima. Ni imani yangu fedha hizi zikielekezwa kwa kiasi kikubwa vijijini tutakuwa tumewaokoa akinamama hawa na majanga mengi wanayoyapata wanapokuwa kwenye harakati za kutafuta maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchache niseme tu Wilaya ya Kiteto katika Mkoa wetu wa Manyara asilimia zaidi ya 65 ni eneo kame sana ambapo hata wakichimba visima virefu bado wanakosa maji. Naiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji iangalie ni mbinu gani mbadala itakayotumika katika kuwasaidia akinamama hawa wa Kiteto waondokane na adha ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niishauri Serikali yangu sikivu kuanzisha Mfuko wa Maji Vijijini ili kusaidia katika suala zima la monitoring. Mfuko huu pia utasaidia kwa kiwango kikubwa kutambua maeneo yenye kero iliyopitiliza na kuweza kuyatatua kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, adha ya maji safi na salama ni chanzo kikubwa sana cha maradhi yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama (waterborne diseases) kama kipindupindu, kuhara, kutapika na kadhalika. Serikali yetu inapoteza zaidi ya fedha za kimarekani dola milioni 72 kila mwaka ili kutibu magonjwa hayo. Je, si vyema tukakinga kuliko kuponya kwa kuthubutu kupeleka fedha nyingi kwenye bajeti hii ili kuepukana na matumizi makubwa ya kugharamikia matibabu ya wagonjwa hao na hata vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo (Waterborne diseases)?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.