Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa utendaji wake na mipango yake ya kushughulikia tatizo la maji nchini kwetu, pamoja na utendaji wa Mawaziri wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa maandishi utajielekeza kwenye Mradi wa Maji wa Chalinze - Wami uliopo katika Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali juu ya kusuasua kwa mkandarasi wa mradi huu wa Wami - Chalinze na kupelekea hali ngumu ya upatikanaji wa maji Jimbo la Chalinze, wananchi wa Chalinze wangependa kupata ufafanuzi katika maeneo yafuatayo:-

(i) Kwa kweli mradi wa maji Wami – Chalinze Awamu ya Tatu unasuasua, mpaka sasa kuna maeneo ndani ya Jimbo la Chalinze ambayo hayana maji ya bomba kwa zaidi ya miezi sita sasa.

(ii) Tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kutembelea mradi huu wa Wami - Chalinze mwisho wa mwezi Machi, tatizo lishughulikiwe mara moja na maji yawe yanatoka ndani ya siku 100 na mkandarasi alipewa siku 100 ya kuonesha kas yake ya utekelezaji. Je, mpaka sasa ni kiwango gani cha tozo kwa kuchelewesha mradi?

(iii) Je, Wizara baada ya siku 100 alizotoa Waziri Mkuu kuisha na kasi ya mkandarasi kuwa ndogo, Wizara itakuwa tayari kufikiria upya juu ya mkandarasi wa mradi huu wa maji wa Wami - Chalinze Awamu ya Tatu, kwani kama sitakosea kuna kumbukumbu zinaonyesha mkandarasi huyu ana rekodi zisizoridhisha kwenye miradi mingine ya aina hii katika maeneo mengine.

(iv) Uendeshaji wa mradi huu wa maji wa Chalinze, Menejimenti ya CHALIWASA inaonyesha kushindwa kabisa. Uendeshaji wa mradi uko tofauti sana na wakati ukiwa chini ya mkandarasi toka China. Wananchi wengi wa Chalinze wanalalamika sana na bill zinazotolewa. Utokaji wa maji yenyewe usafi wa maji ni shida, waliokatiwa huduma ya maji bado wanachajiwa service charge.

(v) Mamlaka ya Maji Chalinze (CHALIWASA) wamejitoa kuagiza vifaa vya kuunganisha maji hususan mabomba badala yake wameliacha jukumu hili nyeti kwa wateja wa maji wasio na uelewa kitalaam wa ubora wa vifaa vilivyo sokoni hususan mabomba. Je, taratibu na sheria zinaruhusu?

(vi) Kwa kuwa Mji/Halmashauri ya Chalinze sasa ni mji wa viwanda na kuna ujenzi wa viwanda, mfano ujenzi wa Kiwanda cha Tiles Chalinze, ujenzi wa Kiwanda cha Kusindika Matunda, Mboga cha Sayona kinachotarajiwa kukamilika hivi karibuni. Hata hivyo kutokana na tatizo la maji Chalinze linaweza kuathiri kabisa ufanisi wa uzalishaji wa viwanda hivi.

Kutokana na shida hii ya maji Chalinze uongozi wa kampuni hii ulikutana na uongozi wa CHALIWASA kujua tatizo ni nini, hasa moja ya tatizo walisema uchakavu wa pump na machujio ya maji na baadhi ya vifaa. Serikali kwa sasa haina fungu kwa ajili ya kazi hiyo. Kupitia mazungumzo hayo mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Sayona Fruits ilionesha utayari wa kuagiza hivyo vifaa nje ya nchi ili uweze kufungwa na hatimaye gharama hiyo ijumuishwe na kukatwa kwa awamu kutoka kwenye bill ya maji ya kiwanda itakayopelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, menejimenti ya CHALIWASA inashauri iandikwe barua kwa Mawaziri wa Maji na Viwanda ili watoe ridhaa ya mwekezaji aendelee na utaratibu wa kuangiza hivyo vifaa. Mpaka sasa Wizara ya Maji haijatoa mwelekeo au maelekezo yoyote, jambo hili linaweza kufifisha ari za wawekezaji wetu. Kiwanda hiki kinatarajia kuzalisha/kusindika tani 60 kwa siku na kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya bilioni 150, na rasilimaji kubwa ni upatikanaji wa maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara kutoa msimamo wake kwenye barua ya maombi iliyoandikwa na mwekezaji Kampuni ya Sayona Fruits kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa maswali ya sera ya Serikali ya viwanda na wananchi wa Chalinze ambao watafaidika kwa uboreshaji wa miundombinu ya mradi huu wa maji Chalinze wa awamu zilizopita za kwanza na pili ambayo ni chakavu.

(vii) Suala la tatizo la maji katika Majimbo ya Kisarawe na Bagamoyo ni kubwa na moja ya sababu ni kumezwa na mipango ya Jiji la Dar es Salaam. Haiwezekani Kisarawe au Bagamoyo huduma za maji ziendeshwe na DAWASCO/ DAWASA ambayo wenyewe wamezidiwa kiutendaji kutokana na mahitaji ya Dar es Salaam na maelezo yake kutokana na wingi wa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali/Wizara kuunda Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Pwani kama ilivyo kwa mikoa mingine na kuziimarisha kuzifufua Mamlaka za Maji za Wilaya ili ziwe na mamlaka kamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera ambapo ukikamilika unatarajiwa kuzalisha lita milioni 260 kwa siku ambapo maeneo yafuatavyo yatafikiwa; Gongo la Mboto, Chanika, Pugu, Ukonga na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maeneo haya yapo karibu na Kisarawe, naishauri Serikali kuona uwezekano wa kuweza kupata huduma ya maji kutokana na tatizo kubwa la maji maeneo ya Kisarawe.