Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nachukua nafasi hii niungane na Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mheshimiwa Spika, kutoa pole kwa mwenzetu kwa jambo ambalo limempata na tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie ili afya yake iweze kurejea katika hali ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nitoe mchango mbele ya Bunge lako Tukufu juu ya Azimio la Bunge kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa Kamisheni ya pamoja ya Bonde la Mto Songwe sambamba na kuridhia Azimio la Itifaki ya Amani na Usalama kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya hivi karibuni suala la maji limekuwa ni suala ambalo linaelezwa kuweza kusababisha Vita Kuu ya Tatu ya Dunia. Maji yamekuwa ni tatizo, lakini chanzo kikubwa cha ukosefu wa maji ni uharibifu wa mazingira. Pamoja na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kimsingi yanashahibiana moja kwa moja na mabadiliko ya tabia za binadamu hasa pale ambapo tunaharibu mazingira, basi maazimio kama haya yakija kwenye Bunge letu Tukufu, hakuna namna zaidi ya kuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwamba pamoja na nia nzuri ya Serikali kuridhia hili, lakini sasa iwe ni mwanzo wa changamoto pia kuhifadhi mabonde mbalimbali yaliyoko katika Taifa letu. Kwa mfano, tumeona hivi karibuni kulikuwa na wadau wa Bonde la Mto Ruaha Mkuu lakini pia kule Mkoani Rukwa na Katavi kuna bonde pia, nimeona Mheshimiwa Waziri anayehusika na mazingira walikuwa wanafuatilia pia uhifadhi wa lile bonde; na kuna mabonde mengine kama Malagarasi, bonde la Mto Pangani nayo pia bado hayako katika hatua nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwamba tunapokwenda kuridhia mikataba hii ya Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kwa maana kwa nchi ya Tanzania na Malawi, basi pia tuone umuhimu wa kuangalia kwa mapana haya mabonde mengine ambayo yanazunguka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai, kama ambavyo kwenye Kamati wameshauri kwamba nchi yetu haikuwa na mahusiano mazuri sana na Malawi hasa katika eneo hili la ziwa, lakini nadhani kwamba itifaki hii iende pia kuamsha ari mpya katika kutengeneza mahusiano, siyo tu ya kidiplomasia lakini ya kiuchumi, ya kijamii na ya kimazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba mkataba huu ukiridhiwa utoe tija ambayo inategemewa kwa wananchi wa pande zote mbili. Pia ni kipaumbele kwamba kwa kuwa hata Mkoa huu wa Songwe ni mkoa mpya, tunaamini kwamba fursa mbalimbali zitakazopatikana kupitia uanzishwaji wa hii Kamisheni utasaidia hata kusukuma maendeleo mengineyo hasa katika Sekta za Kilimo na uzalishaji wa umeme; tumeona hapa takriban megawatt 180 zinaweza zikazalishwa kupitia bonde la Mto Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo naiona ni suala zima tu la eneo kwa wananchi juu ya utunzaji wa jumla wa mazingira hasa tunavyoona kwamba mto huu unatiririsha maji kuelekea katika Ziwa Nyasa na mara nyingi shughuli za kilimo wakati mwingine zinachangia kusababisha uharibifu na kusababisha vina vya maziwa kupanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwamba pia wananchi waelimishwe ili wale ambao wanalima pembezoni mwa mabonde haya, wawe waangalifu kiasi kwamba tuweze kulinda siyo bonde peke yake, lakini pia hata mtiririko wa maji kuelekea katika Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nizungumzie kuhusu kuridhia kwa Itifaki hii ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Napenda kupongeza kwa hatua hii. Pia natoa rai kwamba naunga mkono moja kwa moja Azimio hili, kwa sababu tumeona kwamba sasa hivi nchi hizi za Afrika Mashariki tuna tatizo la ugaidi. Tumeona mara nyingi kule upande wa Kenya hasa eneo la Garissa na Mombasa mara kwa mara wamekuwa wakishambuliwa na magaidi hasa hawa wanaotokana na wenzetu wale wa kutoka Somalia, Al-Shabaab.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni, mwaka mmoja uliopita, hata katika Mkoa wa Tanga katika maeneo ya Mapango ya Amboni kulipatikana vikundi ambavyo vilikuwa na dalili zote kwamba ni vikundi vya kigaidi na hata hali inayotokea pale katika eneo la Kibiti, Mkuranga ni viashiria ambavyo siyo vizuri sana kwa ustawi wa amani na usalama katika nchi zetu za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme wazi kwamba protocol hii itatusaidia ili tuwe na ulinzi wa pamoja kama ambavyo tunafanya na hata juzi hapa, tuliona kule Tanga kulikuwa na zoezi la pamoja kwa nchi za SADC. Kwa hiyo, tutafarijika sana kwamba zoezi hili sasa nje ya SADC lifanyike pia kwa nchi hizi za Afrika Mashariki hasa kwa kuzingatia kwamba sisi mipaka yetu hii karibu nchi zote tano ukiondoa Sudan Kusini ambayo ni mwanachama mpya, lakini nyingine zote tunapakana nazo kila mahali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii itasaidia kama hapa ambapo wamezungumza pia kwamba wakati mwingine kuna minada ya mifugo inafanyika katika hizi nchi, hata mimi katika Jimbo langu la Mlalo pia ni mwathirika wa hii minada. Ni kwamba katika Bonde la Mkomazi ambako kuna wafugaji ambao wanapatikana katika Wilaya za Same, Lushoto Mkinga na Korogwe, mara nyingi kule hatuna minada katika haya maeneo kwa upande wa Tanzania. Kwa hiyo, hawa wafugaji huwa wanapeleka kuuza mifugo katika upande wa Kenya. Kwa hiyo, kwa kupitia itifaki hii, naamini kwamba suala hili litaimarisha mahusiano haya na tunaweza hata tukawa na masoko mazuri yenye amani na usalama na kusaidia biashara hizi ziweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nitoe rai kwamba ipo mipaka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo siyo mipaka rasmi, lakini kwa Serikali hizi kwa kushindwa kuirasimisha, inachochea sasa hata vitendo vya uhalifu kufanyika na biashara za magendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kwenda kusaini Azimio hili la Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini pia Serikali sasa ione pia chachu na ione pia mwanya wa kwenda kurasimisha ile mipaka, hata isiwe katika ngazi za Kimataifa lakini angalau katika ngazi zile zile za ujirani mwema kwamba tuwe tunaweza kubadilishana mazao ambayo yanapatikana katika nchi hizi tunazopakana. Tofauti na hivyo, bado unabaki mwanya kwa wananchi wa kawaida kuitumia kuvusha kwa njia za magendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwamba tunapokuwa na maazimio mazuri kama haya ni vizuri pia tukayatumia haya haya kuongeza tija nyinginezo za kiuzalishaji, isibaki tu kwa ulinzi na usalama, lakini pia za uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono Maazimio yote mawili. Ahsante sana.