Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nitoe masikitiko yangu kwa Mbunge mwenzetu kushambuliwa na majambazi. Kwa kweli, tunampa pole sana na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kumsaidia apone haraka aje afanye kazi zake za Kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wenu kwa namna mlivyochangia, hakuna hata mmoja aliyepinga kwamba tusiianzishe hii Kamisheni ya kuendeleza Bonde la Mto Songwe. Nashukuru kwa sababu siyo kawaida, mara nyingi kuna wengine wanapinga tu hata mazuri, lakini kwa leo angalau kwa namna moja au nyingine wote wameunga mkono kwamba hii Kamisheni ni muhimu ianzishwe kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu walioko kwenye Wilaya tano. Katika Wilaya hizi tano vijiji 48 vitanufaika na miradi hii ambayo imeibuliwa kwa manufaa ya nchi zote mbili upande wa Tanzania na upande wa Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kwa maoni ambayo yametolewa na Kamati ya Bunge, yote haya katika mkataba huu ambao tumesaini kati ya Malawi na Tanzania, vifungu hivi vyote viko very flexible kwamba hakuna kifungu ambacho hakina namna ya kurekebisha. Madaraka yote ya kurekebisha vifungu hivi tumeipa lile Baraza la Mawaziri. Baraza la Mawaziri la pande zote mbili watakuwa na uwezo wa kuongeza jambo lolote jema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba mambo mengi mazuri haya ambayo mmeyaleta Waheshimiwa Wabunge, tutaangalia namna ya kuyapeleka katika kuboresha mkataba wetu ili uweze kuleta manufaa zaidi ili tuweze kuendeleza bonde hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu hawa wananchi wa vijiji 48 ambao ni zaidi ya 315,000, kwanza watapata umeme wa uhakika. Kwa awamu ya kwanza ambayo tunajenga Bwawa la Songwe Chini ambalo litaweza kutoa megawati 180 Tanzania tutaanza na mgawo wa Megawati 90 ambazo tutaziingiza kwenye gridi ya Taifa. Kwa sababu azma yetu ni kupeleka umeme vijijini kwa sehemu kubwa, hivi vijiji 48 nina hakika kwa mpango huu watapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hizi hekta 6,000 za kilimo cha umwagiliaji. Wakati madhara ya mto huu ulivyokuwa unafurika mara kwa mara, hata hiki kilimo cha umwagiliaji kilikuwa kinakuwa tatizo kwa sababu mashamba ya wananchi maeneo ya Kyela na Ileje, yalikuwa yanajaa maji kiasi ambacho iliathiri sana kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yale. Tukija kuboresha sasa tukajengea miundombinu ambayo imeboreshwa, nina hakika sasa kutakuwa na kilimo endelevu na tunainua uchumi kwa ajili ya wananchi wanaoishi maeneo haya. Kwa hiyo, ni kama wengine walivyosema, kwamba mkataba huu umechelewa, ungekuja mapema zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tujue kabisa kwamba tumeanza kuzungumza uanzishwaji wa kitu cha namna hii toka mwaka 1976, lakini tumekuwa tunapanda ngazi kidogo kidogo. Tulipofika mwaka 2001 ndiyo tukaanzisha ile Kamisheni ya Mpito au Interim Secretariat ambayo nayo imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kujenga hii Ofisi ya Makao Makuu hapo Kyela. Kwa hiyo, ofisi tayari ipo imeshajengwa; na tutaanzia pale katika kusimamia sasa miradi hii iliyoibuliwa itakayoleta manufaa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lissu alikuwa na mashaka, alifikiri kwamba katika kusaini mkataba huu alienda Lwenge peke yake. Naomba nimtoe wasiwasi kwamba hakwenda Mheshimiwa Lwenge peke yake, ilikwenda kama Serikali ikiwa na wataalam wote waliobobea katika sheria, akiwepo Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, masuala ya sheria yote yamezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Olenasha amefafanua vizuri namna ya kutekeleza miradi inayokuwa inashirikisha zaidi ya nchi moja, lakini katika kutatua migogoro, hili suala la kwenda kwenye SADC au UN, hiki ni kitu cha mwisho kabisa. Tumeweka hatua ya kwanza na kwa maelewano tuliyokuwanayo katika miaka yote hii hatufiki huko, kwa sababu kazi tunayoifanya ni ya manufaa kwa nchi zote mbili. Ndiyo maana nasema kwamba sasa tunaimarisha uhusiano wetu kwa nguvu zaidi kwa ku-develop miradi inayotunufaisha Malawi na Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata hili suala la mgogoro wa mpaka au mgogoro wa Ziwa Nyasa nina hakika tumeanza vizuri kwa sababu hiki kitakuwa ni kichocheo kimojawapo ambacho kimetuunganisha zaidi Malawi na Tanzania katika kufikia muafaka wa jambo hili ambalo linazungumzwa la matumizi au rasilimali za Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wetu una namna ya kutoka kama nchi moja ikionekana inakiuka makubaliano, tumesema kwenye Kifungu cha 18 kwamba nchi moja inaweza ikavunja mkataba inapoona mwenzie hatekelezi yale tuliyokubaliana kwa kutoa notice ya miezi sita kwa maandishi, kwa hiyo, kuna namna ya kutoka, lakini sitaki tukifike huko kwa sababu hatuwezi kutoka na kwa sababu pia, hii miradi ambayo imeibuliwa ya kujenga umeme na miradi mingine, tayari wafadhili wameshaonesha nia, kama nilivyowasilisha pale mwanzo. Wameshaonesha nia ya kutusaidia ili tuweze kuendeleza Bonde hili la Mto Songwe kwa manufaa ya nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme tu kwamba maoni yote ambayo Waheshimiwa Wabunge mmetoa, tutaendelea kuyaboresha. Kwenye Council, katika zile Wizara sita, kuna Wizara ya Fedha pia ipo. Kuna mmoja alikuwa anataka kuhakikishiwa kama kuna wataalam wa fedha watakuwepo. Wizara ya Fedha ni mojawapo katika Wizara ambazo zinaingia kwenye Council, kuna Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na Wizara ya maji. Ila kwenye Mkataba wetu tumeweka nafasi ya ku-opt advisor yeyote au Wizara yoyote ambayo tunafikiri kwa muda ule tunapokuwa tunajadili tunaweza tukamwingiza kwenye Council ili kusudi aweze kusaidia, kutegemea ni jambo gani tunalolishughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkataba uko vizuri, uko flexible. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyochangia, niwashukuru tena kwa maana kwamba sasa tunakwenda kuanzisha hii Kamisheni ambayo itatusaidia kwa maendeleo ya wananchi wetu wa pande zote mbili. Pia, tutaondoa huu wasiwasi wa wananchi wetu ambapo mto kila mara ukifurika walikuwa mara wanakuwa Malawi, mara wanakuwa Tanzania; ili kusudi waweze kufanya maendeleo endelevu, sasa watakuwa na uhakika wako Tanzania na wameshaendelezwa, wameshapata mahitaji mengi ya kuwainua kiuchumi. Kwa hiyo, nina imani kabisa baada ya utekelezaji wa mradi huu, tutakuwa na jambo la kujivunia kwa kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Songwe kwa faida ya nchi zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, nirudie tena kukushukuru wewe kwa namna ulivyoendesha mjadala huu. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili kwa namna walivyochangia; na nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wengine ambao pia wameweza kuchangia na kuunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwa heshima kubwa naomba kutoa hoja ili Kamisheni hii sasa iweze kuanzishwa, ya Ushirikiano Kati ya Malawi na Tanzania kwa ajili ya Kuendeleza Bonde la Mto Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.