Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa ya kwanza ya kuwa mchangiaji katika hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri Mheshimiwa William Lukuvi, Naibu Waziri Mheshimiwa Angeline Mabula, Katibu Mkuu Dkt. Kayandabila na safu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika Wizara ya Ardhi. Kwa mara ya kwanza nitaanza kuiongelea vizuri Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitano ambayo nimekuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sijawahi kuunga mkono bajeti ya Wizara ya Ardhi, inawezekana leo ikawa ndiyo mara yangu ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la kwanza ambalo nilitaka niligusie ni suala la premium. Mheshimiwa Waziri ameongea katika hotuba yake kwamba amepunguza premium kutoka 7.5 percent kwenda asilimia 2.5. Tunatoa pongezi nyingi sana kwa Serikali, lakini bado tunaamini kwamba kiwango hiki bado ni kikubwa sana. Waende wakaliangalie tena. Katika suala la mashamba makubwa ambayo wamekuwa wanayahimiza wananchi wayapime, kikwazo kimoja cha kupanga Miji na upimaji imekuwa ni premium. Kwa hiyo, naomba waende wakaiangalie upya ili kama ikiwezekana tuipunguze zaidi na itatoa hamasa kwa wananchi kupima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni viwango vya land rents; kodi za ardhi nazo bado kuna wakati walipandisha, nadhani sasa wamefanya marekebisho. Suala hapa siyo kupandisha viwango, suala hapa ni kuhamasisha wananchi waweze kuwa wanalipia. Tukiongeza viwango vikawa vikubwa sana, ulipaji nao utakuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nataka sana Wizara nayo itusaidie, asilimia 30 ya mapato yale ya land rent yanayotakiwa kurudishwa katika Halmashauri, mpaka wakati tunatengana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke tulikuwa tunaidai Wizara ya Ardhi takribani Sh.3,000,000,000/=. Ni fedha nyingi sana ambazo zingeweza kutusaidia katika maendeleo ya Halmashauri zetu. Sasa nadhani ifike mahali kama inashindikana fedha ile kwenda na wao wakaturejeshea 30 percent, kwa nini sasa tusipitishe sheria tufanye mabadiliko tu-retain ile 30 percent na sisi tuwapatieni ile hela nyingine iliyobaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nataka kuligusia ni master plan ya Mkoa wa Dar es Salaam. Dar es Salaam inakuwa kwa kasi kubwa sana, lakini utengenezaji wa master plan umekuwa unakwenda muda mrefu sana. Nimeona katika ripoti yao wanaongelea mwezi Agosti, naamini Agosti itakuja nayo itakwisha. Tungependa kuona ifikapo mwisho wa mwaka huu tuwe na master plan ya Dar es Salaam, ujenzi holela unatapakaa kwa kasi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ambalo ninataka kuligusia ni mradi wa viwanja 20,000 katika Jimbo langu la Kigamboni, hususan katika eneo la Kibada. Wananchi walionunua viwanja vile, walilipa premium ambayo inaendana na utengenezaji wa miundombinu. Mpaka sasa hivi tunavyoongea kuna wananchi wa Kibada wanaelea, kuna viwanja wamewapa kwenye mabonde, sasa hivi kuna wananchi wa Kibada wanashindwa kufika majumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kibada hawana miundombinu ya kufika katika makazi yao na nitamwomba sana Mheshimiwa Waziri baada ya bajeti yake twende Kibada akawaone wananchi wale ambao walilipa fedha na wanalipa kodi ya ardhi, wanaishi kwa shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo nataka kuliongelea ni suala la Kigamboni. Serikali ilikuja na mpango wa Kigamboni mwaka 2008 tunavyoongelea sasa hivi ni mwaka wa tisa, wananchi wale hawajengi, hawakarabati, hawauzi wala hawakopesheki. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri tangu ameingia katika Wizara ile, tumeweza kufanya kazi kubwa sana mimi na yeye na namshukuru sana chini ya uongozi wake, yale ambayo wananchi wa Kigamboni tuliyokuwa tumesimamia, ameweza kuyasimamia na kuyatekeleza kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana yeye na safu nzima ya Wizara yake. Hatua tuliyofikia ni nzuri sana na ndiyo maana mnaona Mbunge wa Kigamboni sasa hivi ametulia, la sivyo siku za nyuma hapa pangekuwa hapatoshi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna lile ombi ambalo tumeleta kwenu Serikalini na ambalo nashukuru Mheshimiwa Waziri ameligusia kwa kidogo. Kuwepo mamlaka mbili za kupanga mji inaleta kero na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuvunja CDA. Sisi pia sasa
tunasema KDA hatuitaki. Tunaomba mradi ule uletwe chini ya Halmashauri mpya, chini ya uongozi mpya wa Kigamboni ili sisi wenyewe tukausimamie. Mheshimiwa Waziri akiweza kulitekeleza hilo, tutakuwa marafiki wa kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, machache nakushukuru sana na kwa mara ya kwanza naunga mkono bajeti ya Wizara ya Ardhi. Ahsante sana.