Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami niungane na wachangiaji wenzangu waliopita kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri sana wanayofanya katika Wizara hii ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi ni Waziri wa mfano na hili wala halina kificho, kwa hiyo nimwombe tu Waziri Mheshimiwa Lukuvi pamoja na timu yake basi ile speed ambayo wanayo ikiwezekana waongeze kwa sababu ardhi ndiyo kila kitu, maeneo mengi inatakiwa watu wapimiwe ili wakae kwenye makazi salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Kitendo alichokifanya jana cha kuwaonesha Watanzania na dunia kwa ujumla katika sakata kubwa la usafirishaji wa mchanga. Kazi ile imefanywa kitaalam na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, wa vyama vyote, hata mdogo wangu pale Mheshimiwa Ester Bulaya, kwa sababu bahati nzuri wenzetu upande wa kule mlikuwa kila siku mkisema kwamba tunaibiwa sasa ule ni mwarobaini, sasa tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa hatua hii ambayo ameichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kuhusu kuivunja CDA. Mheshimiwa Lukuvi mimi ni mmoja wa wahanga niliyedhulumiwa kiwanja changu na bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, nafikiri kwa hali ya sasa tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara mwaka huu imepanga kukusanya maduhuli, tozo shilingi bilioni 112, nilikuwa najaribu kuangalia ile trend, mwaka 2015/2016 Mheshimiwa Waziri alipanga kukusanya bilioni 70, akakusanya bilioni 74, mwaka uliopita 2016/2017 alipanga kukusanya milioni 111.7 mpaka Mei ana bilioni 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua yeye pamoja na timu yake ni wachapakazi wazuri na mimi kama Mjumbe wa Kamati hiyo tungependa zaidi ile bajeti ambayo wameipanga wakaitekeleze, kwa sababu ili apate fedha za kuweza kufanyia kazi kwenye maeneo ambayo ameyapanga lazima makusanyo, ikiwemo na tozo ziweze kupatikana. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake speed iongezeke, lakini pia kuzuia mianya ya pesa zinazotumika vibaya kwa sababu bila kuzuia mianya hawezi akakusanya vizuri. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimwombe, Halmashauri zetu huko tuliko bila kuficha Mheshimiwa Waziri hatuna uwezo wa pesa wa kupima kila kitu, tunayo Miji, lakini nianzie upande wa taasisi za Serikali, shule za msingi, shule za sekondari, zahanati, vituo vya afya, tukiacha kwa jinsi ilivyo sasa taasisi za Serikali zinavamiwa, inawezekana hata kwa Mheshimiwa Waziri zipo shule za msingi na shule za sekondari zinavamiwa na watu, wanajenga karibu na shule. Unakwenda kujenga karibu na shule ya sekondari pale kuna wasichana, kuna vijana, kuna nyumba ya makazi pale, kwa hiyo mtajikuta kwamba hakuna kitakachokuwa kinaendelea kwa sababu mji na shule ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili alitazame vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri mipaka ya Kimataifa na anasema kwa mwaka 2017/2018 Wizara itaendelea na uimarishaji wa mpaka wa Tanzania na Kenya ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa ramani za msingi pamoja na kupima kipande cha mpaka kuanzia Ziwa Victoria hadi ziwa Natron. Akaendelea, Majadiliano kati ya Tanzania na Zambia, Tanzania na Uganda kwa ajili ya uimarishaji wa mipaka yanaendelea.

Mheshimiwa Waziri, Watanzania tunaweza sisi tukawa watulivu lakini huwezi ukajua nchi zingine kwenye mipaka yetu hiyo, nakumbuka vizuri kwenye mpaka wetu wa Zambia lakini bado tuna tatizo na Kenya na Uganda. Nashauri kwamba, najua kuna kazi nzuri inafanywa tusiishie tu kwenye maneno, twende kwenye vitendo zaidi, ni vizuri tukaainisha mipaka yetu inaishia hapa. Tukiacha wenzetu wanaweza kwa sababu huwezi kujua anaweza akaja Rais mwenye mfano huo unaofanana na wengine huko, akasema hili ni eneo la kwangu akalazimisha, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri hili alitazame vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni huduma za upangaji Miji. Tuna utaratibu wa kujisahau tunaacha miji inajengwa, inakua bila kupimwa na baadaye ndiyo tunakwenda kupima, kinachofanyika ni kwenda kuweka “X” kwenye nyumba za wananchi, kitendo hiki sio kizuri sana. Kwa nini sasa kusiwe na uratibu mzuri wa kupima na kuweka mipango miji ikakaa vizuri iliyopimwa ili kusudi watu waweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Malya, Sumve, Kabila, Nyambiti, Nhungumalwa, Mvomero, maeneo haya Mheshimiwa Waziri ni maeneo yanayokua. Mheshimiwa Naibu Waziri wewe anafahamu pale Sumve ni Mji unaokua, sasa tusipoupima leo na tukisema tutegemee Halmashauri, Halmashauri hazina kitu, nafikiri zote ukiachia labda zile za mjini, lakini ukisema Magu iende ikapime yenyewe, Kwimba, Mvomero hatuwezi kutimiza yale ambayo Mheshimiwa Waziri ameandika humu. Kwa hiyo, nimwombe sana kwenye maeneo mengine kule kama Halmashauri zenye uwezo zikafanye lakini Halmashauri ambazo hazina uwezo kwa kweli nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ziweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nipongeze utendaji kazi mzuri wa Shirika letu la Nyumba National Housing, niwaombe sana kwa sababu wanafanya kazi nzuri na mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili kwa kweli kazi yao ni nzuri sana, tuwatie moyo, kazi wanayofanya ni nzuri sana, bahati nzuri na mimi niliishawahi kuwa Mjumbe wa Bodi wa Shirika la Nyumba kazi tuliyoiacha sisi ndiyo wanayoiendeleza, naomba moto tuliouacha basi mwendeleze lakini niwatakie kila la kheri katika shughuli zenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri upande wa mipaka ya Tanzania nimelisema hili nalirudia tena, tunaweza tukaliona kama ni jambo dogo, lakini mbele ya safari lina athari kubwa tukiliacha. Nasema tena tukiacha tukasema kwamba kwa sababu majirani zetu ni wazuri mno wanaweza wakafika mahali wakatugeuka. Nimshauri sana Mheshimiwa Waziri hili kwa sababu ameshalianza, naomba waendelee nalo, nawatakia kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante sana.