Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hoja iiyopo mbele yetu. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa ofisi yake kwa kazi nzuri wanayoifanya nchi yetu. Kipekee Mheshimiwa Waziri amekuja Mkoani kwetu Manyara, ametusaidia migogoro mingi na kwa kweli Mungu aendelee kumwongoza na kumpa afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye sekta ya ardhi, rasilimali ardhi hakuna asiyejua umuhimu wake na uhitaji wake sasa hivi katika nchi yetu. Uhitaji wa ardhi miaka 30 iliyopita na leo, mwaka huu tuliopo na miaka 30 ijayo ni tofauti kabisa kuashiria kwamba nchi yetu inanyemelewa na ufinyu wa ardhi. Hili ni jambo la hatari kama hatutaweka mipango madhubuti katika kuiweka ardhi yetu iweze kutusaidia katika mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana jioni tulikuwa na mjadala mzito baina ya Wabunge wanaotetea wakulima na wengine wanaolaumu wafugaji, lakini hakuna mshindi hata wangetumia lugha namna gani kusema kwamba wafugaji ni wabaya, wakulima ni wabaya wanafanya hivi na vile kwa sababu wakulima ni Watanzania wale wale na wataishia kuwa Watanzania na wataendelea kulima na wafugaji hali kadhalika ni Watanzania wataendelea kufuga na wataendelea kuwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la maana ni kuhakikisha kwamba tunabuni mipango madhubuti ili kuhakikisha kwamba jamii zote mbili hizi na hata watumiaji wengine wa ardhi wanaishi vizuri katika nchi yao bila kuwa na migogoro ya hapa na pale na bila ya kuwa na migogoro ya kuvamia ardhi na kusababisha maafa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ninaloona ni kubadilisha mindset, ni lazima tubadilishe mindset yetu. Huwa natumia mfano wa mkoa mdogo wa Kilimanjaro kulinganisha na Mkoa wetu wa Manyara, ukiangalia Mkoa wa Kilimanjaro mnisamehe wananchi wa Kilimanjaro na Wabunge wa huko. Mkoa wa Kilimanjaro una eneo dogo sana lakini una watu wengi, Mkoa wa Manyara una eneo kubwa sana watu ni wachache, lakini utakuta katika eneo dogo hilo hakuna migogoro inayolingana na migogoro iliyoko Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu wananchi wa Kilimanjaro toka mwanzo waliona kwamba ardhi yao ni finyu kwa hiyo lazima waweke mikakati madhubuti, wameweka mindset yao kwamba ni lazima ardhi yao finyu wanaitumia kwa busara ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wao. Kwa hivyo eneo kubwa linaleta udanganyifu kwamba bado ardhi yetu ni kubwa kwa hiyo tunaweza tukavamia hapa tukaitumia kwa ajili ya matumizi ya mashamba au kufuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima tubuni kama nilivyoeleza, kwamba ardhi inanyemelewa na ufinyu wa ardhi na ongezeko kubwa la watu, kwa hivyo lazima kuwe na ubunifu. Jana nilikuwa nasoma mipango ya miaka mitano yaani 2015/2016 na 2016/2017. Tuna mipango mizuri sana, tuna mipango madhubuti kuhusu sekta ya ardhi, lakini cha kushangaza bado hatuwezi kutamba leo kusema mipango tuliojiwekea imeweza kuleta impact hii hasa katika sekta ya ardhi, hivyo bado tuna safari ndefu kuhakikisha mipango yetu tunayopanga lazima iwe real, iende sambamba na hali halisi, kama kuna ongezeko kubwa la watu ni lazima ardhi yetu iende sambamba na ongezeko kubwa la watu na kuhakikisha kwamba inatumika madhubuti na inatutosha kwa matumizi yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujizatiti na matumizi bora ya ardhi. Naishauri Serikali kwamba to pull resources zote sasa hivi kwa sababu kilio hiki ni kikubwa. Tangu niingie Bungeni hapa kilio cha wakulima na wafugaji kiko pale pale, sijaona tofauti, kilio kinazidi kila siku na kwa kilio hicho, tukiangalie sasa mipango yetu iweze kutupa ahueni. Tuhakikishe resources tulizonazo tuweze kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi yetu ili tuondoe kilio cha wakulima wetu na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali pia kutoa elimu hasa kwa jamii ya wafugaji. Jamii yetu ya wafugaji bado hawajawa na upeo wa uelewa katika matumizi ya ardhi. Sheria ni jambo ambalo lazima tujizatiti nalo liweze kusaidia katika kuhakikisha ardhi yetu tunaiwekea mikakati
madhubuti ili liweze kwenda kusaidia wananchi wake na hatimaye tuweze kuwa na maisha bora na harmony baina ya jamii zetu za watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna migogoro ya wakulima na wafugaji lakini na watumiaji wengine wa ardhi kama wawindaji, warina asali, waokota matunda, nao itafika mahali watahitaji ardhi ya kuitumia. Tumeweka mipango madhubuti ya kupanua kilimo chetu bila kuzingatia kwamba kilimo hicho hicho kinahitaji ardhi madhubuti ambayo tutakwenda kuitumia kupanua kilimo ili tuweze kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu na kadhalika ili tuweze kuinua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sheria ni suala muhimu sana katika kudhibiti matumizi bora ya ardhi, naomba kutoa mfano wa Wilaya ya Kiteto katika Mkoa wa Manyara. Wilaya ya Kiteto ilivamiwa na wakulima toka nje ya Wilaya na hii ni kwa sababu ilionekana kwamba Wilaya ile ilikuwa na ardhi prime, haina mwenyewe sana, kwa hiyo walikuja wakulima kutoka nje wakapasua pori wakalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu mmoja ambaye amekuja kama kibarua, msimu unaofuata hawi tena kibarua anafyeka pori anakuwa yeye ndiye mmiliki wa shamba. Kwa hiyo, anafika mahali anawaita watu wengine 200 zaidi, analima msimu mmoja kama kibarua msimu unaofuata anawaleta 200, kwa hiyo ni 200 x 200x 200 ardhi inakuwa imekwisha kulimwa kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze kwamba, sheria huwa inafanya kazi kwa sababu wavamizi wote waliovamia mbuga mbalimbali katika Wilaya yetu tuliweza kuwaondoa kwa kutumia sheria. Kwa hiyo, sheria inafanya kazi kuhakikisha kwamba tunadhibiti matumizi bora ya ardhi kama ambavyo tumefanya kule Kiteto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, bado Kiteto kuna matatizo kadhaa. Kwa bahati mbaya Tume mbalimbali ambazo zimeundwa ili zituletee majawabu tuweze kufanyia kazi, bado hatujapata majawabu yake, naomba basi tuweze kupata maelekezo ili wananchi nao wapate utulivu katika Wilaya yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano, kwa nini naipongeza hasa Mawaziri wake? Wakati nikiwa Kiteto kama kiongozi miaka yangu mitatu ambayo nimekuwa nikipambana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, hakuna ambaye hajasikia Kiteto kulikuwa na mauaji ya wakulima na wafugaji lakini bahati mbaya wala simteti mtu, hakuna Waziri aliyekanyaga kusaidia kutatua migogoro ile ama kuona ni namna gani tunaisaidia Serikali kuhakikisha kwamba migogoro inakwisha na watu wanaacha kupigana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi. Hapa Mvomero wamekatwakatwa ng’ombe usiku, asubuhi Mheshimiwa Mwigulu yupo pale, alipokuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia migogoro ya ardhi, Awamu hii Mheshimiwa Lukuvi ametembelea pale mara nyingi, sikumwona Waziri wa Ardhi wala wa Kilimo na Mifugo wakati ule kwa miaka yote mitatu na ndiyo maana naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano wakiongozwa na Jemedari wao Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua migogoro ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti nimeona nichangie haya machache katika sekta ya ardhi, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi.