Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuzungumza jioni hii. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye aliyetupa uzima na uhai, ametupa muda mwingine tena wa kuweza kumtumikia. Pili, naomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo aliyoifanya jana kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa nzuri ambayo anaifanya katika Wizara hii pamoja na Naibu Waziri. Wanafanya kazi kubwa ambayo inaonekana kihalisia, tunaomba tuwapongeze sana na Mungu aendelee kuwasimamia ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Mkoa wangu wa Katavi nikiongelea kuhusu masuala ya Wilaya mpya ya Tanganyika. Wilaya ya Tanganyika ina vijiji vingi sana ambavyo mpaka leo havijafikiwa kupata hati miliki ya kimila. Wananchi wengi wanaoishi maeneo haya hawana faida na rasilimali zao walizonazo. Kwa sababu tumeona Wizara hii ni sikivu, tunaomba basi wanavijiji wale wa Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi wafikiwe ili waweze kupata hati miliki za kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya Mkoa wa Katavi ni pori, asilimia 30 ndiyo maeneo wanayoishi wananchi; na siku hadi siku ndani ya Mkoa wetu wa Katavi wananchi wanaongezeka na maeneo yetu ya kufanyia shughuli za kibinadamu ni machache. Naomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii; kwa kuwa Wizara ya Maliasili wana sehemu kubwa sana ya hifadhi; na ukizingatia sasa hivi siku hadi siku tunazaana. Sasa binadamu tumeongezeka, mapori yamekuwa makubwa mno, tunaomba Wizara hizi zitutazame kwa hali ya ukaribu zaidi Mkoa wa Katavi kuweza kutupunguzia maeneo ili tuweze kupata sehemu ya kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kata nyingine hawana kabisa sehemu za kulima, wakiingia tu wanaingia kwenye hifadhi, wakienda huku mapori ambayo yanahifadhiwa na Serikali, sasa wanashindwa jinsi gani ya kufanya shughuli za kibinadamu. Tunaomba Wizara hii ya Ardhi pamoja na Maliasili waweze kutuona kwa ukaribu zaidi kwa ajili ya kutuongezea maeneo ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupata maeneo ya kufanyia shughuli zao kibinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Mpanda Manispaa ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, alifika katika Wilaya ya Mpanda, alijionea mwenyewe hali halisi. Katika Wilaya ya Mpanda Kata yetu ya Kashaurili ambayo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Mpanda katika zile nyumba za wenyeji hakuna mtu mwenye hatimiliki mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama Wizara itusaidie kutokana na hali halisi. Kwa upande wa ardhi Manispaa hatuna kabisa wafanyakazi. Wafanyakazi ni wachache sana; wafanyakazi ambao wameajiriwa ni watatu tu, wengine wote ni vibarua. Sasa wale vibarua wanakuwa hawafanyi kazi yao kimakini kwa sababu, wanajua wenyewe ni vibarua. Sasa naomba kama Wizara itusaidie sasa kutuletea watumishi ambao wameajiriwa ili waweze kufanya kazi vizuri pale Manispaa, Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Mpanda. Katika Kata ya Ilembo kuna migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Jeshi. Najua Mheshimiwa Naibu Waziri alielezwa, basi tunaomba suala hili liweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo kwa sababu, wananchi wa Mpanda pale Kata ya Ilembo pamoja na Kata ya Misunkumilo kila wakiingia kidogo tu Jeshi linasema eneo lao. Sasa tunaomba huu mgogoro uweze kwisha, ili wananchi waweze kupata fursa ya kuweza kufanya kazi zao za kijamii wakiwa katika hali ya usalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilipongeze Shirika la National Housing, limefanya kazi nzuri sana kiasi kwamba hatimaye na sisi wananchi ambao tunaoishi katika wilaya mbalimbali tumeona jitihada za National Housing. Tunaomba tumpongeze sana Mkurugenzi wa National Housing, Mchechu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Ameweka alama kubwa sana katika nchi yetu, ameweka alama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mpanda Mjini tumejengewa nyumba za National Housing. Nyumba zikijengwa zinatakiwa zitumike na binadamu, zisipotumika na binadamu zile nyumba zikishafungiwa miaka miwili, ama mitatu lazima zinakuwa na ufa. Ina maana kuwa binadamu akiishi ndani ya nyumba zile nyumba zinaendelea kuishi, lakini kama ndani ya nyumba haishi mtu nyumba nayo inapata uharibifu, inaweka ufa matokeo yake inaonekana kama nyumba nzee (iliyozeeka). Sasa pale Mpanda mmetujengea nyumba nzuri sana, tunaomba tuwashukuru, lakini zile nyumba bado hazijapata wanunuzi, zile nyumba zinakaa bure, zimefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, sasa hivi Wilaya ya Mpanda ni Mkoa wa Katavi, kuna wafanyakazi mbalimbali wa kisekta, wa Wizara, wa maeneo mbalimbali wamekuja maeneo yale, hawana sehemu ya kuishi. Tunaomba hizi nyumba ambazo zimejengwa Wilaya ya Mpanda, Ilembo, zipangishwe. Zikishapangishwa hapo badaye wale wafanyakazi wanaweza kuzinunua kuliko kuzifungia, zile nyumba hazina mtu wa kuishi, matokeo yake zinakuwa kama vile maboma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara pamoja na Shirika letu la National Housing waangalie upya hizi nyumba ambazo hazijaweza kununuliwa basi wazipangishe ili ziweze kupata wanunuzi mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie tena kwenye masuala ya migogoro ya ardhi. Naiomba Serikali, tunajua Awamu hii ya Tano kusema kweli imejitahidi sana, migogoro ya ardhi imepungua, lakini bado kuna kazi kubwa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, migogoro ya ardhi ni mikubwa sana ndani ya maeneo yetu husika. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, ifike kipindi sasa tutafute maeneo ya wafugaji na maeneo ya wakulima, maana wengi unakuta wakati mwingine wanatetea wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna wakulima ambao nao wanapaswa wapate stahiki yao. Tunaomba Serikali kwa ujumla wake, sasa hivi kifike kipindi cha kuwapangia wafugaji maeneo yao na wakulima maeneo yao, ili nchi yetu ya Tanzania iendelee kuwa na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana na naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.