Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika leo hii ambapo tunahitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu kwa kunipa nafasi ya kuhudumu katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Napenda pia kutoa shukrani zangu kwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi bora. Shukrani za pekee ziende kwa Waziri wangu Mheshimiwa George Simbachawene ambaye alikuwa akinipa maelekezo ya mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nachukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa Bunge wakiongozwa na Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri uliowezesha Bunge hili Tukufu kujadili bajeti hii. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wa kina ambao umesaidia sana kuboresha bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa kunipa fursa tena kwa nafasi hii kwa mara nyingine ya pili kuhudumu katika Bunge hili. Ndugu zangu wananchi wangu, nawapenda sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa umuhimu sana nipende kuishukuru familia yangu, wake zangu pamoja na watoto. Shukrani kubwa zaidi ziende kwa mama yangu mzazi aliyenizaa na kunilea vizuri pamoja na baba yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa naomba nijielekeze katika kujibu baadhi ya hoja zilizochangiwa na Waheshimiwa Wabunge kwa njia ya maandishi na kwa kuzungumza. Majina ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia watatajwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI atakapokuwa akijibu hoja mbalimbali za Wabunge. Kutokana na muda, hoja ambazo hazitajibiwa hapa tutaziwasilisha kwa maandishi ili Waheshimiwa Wabunge wote waweze kuzipitia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi walichangia katika maeneo yafuatayo:-
(i) Usimamizi wa mapato katika Serikali za Mitaa;
(ii) Maeneo mapya ya utawala;
(iii) Migogoro ya ardhi;
(iv) Usimamizi wa watumishi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa; na
(v) Kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianza katika hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ambazo kwa kiwango kikubwa zimeungwa mkono na Wajumbe wengi katika Bunge hili, lilikuwa suala zima la Halmashauri kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri zote zimeelekezwa kupitia mwongozo wa bajeti kutenga 10% kwa ajili ya mkopo wa vikundi vya wanawake na vijana. Aidha, katika uchambuzi wa bajeti agizo hili limezingatiwa na Halmashauri zote zimetenga 10% ya mapato ya ndani. Wakuu wa Mikoa wanaelekezwa kusimamia utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza hapa, sisi Wabunge wote ni Wajumbe wa Kamati za Fedha na Mabaraza ya Madiwani. Kwa sababu mwongozo wa bajeti umeshaeleza na Halmashauri zote zimeshatenga 10% katika bajeti zao za mapato ya ndani na ndiyo criteria iliyotumika kupitisha bajeti ya kila Halmashauri yake, tuna jukumu la kuhakikisha suala hili linatekelezwa. Kwa sababu hii 10% ni own source kwa maana kwamba ni mapato ya ndani yanayokusanywa katika Halmashauri husika, ina maana pesa zile zinaishia katika Halmashauri na kwamba Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani ndilo linafanya maamuzi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia yangu ni kusema kwamba kila Mbunge akitoka hapa atahakikisha kitachokusanywa kinagawanywa kwa wananchi ili mradi vijana na akina mama waweze kupata mikopo hiyo. Nisisitize pia tutakapofanya hivyo lazima tuangalie ni jinsi gani tunawagusa walemavu ili mradi nao waweze kushiriki katika shughuli za ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kulikuwa na hoja ya ukusanyaji wa ushuru wa minara ya simu na mabango ambapo suala hili limekuwa ni changamoto kubwa. Ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba ushuru wa minara ya simu na mabango hutozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali ya Mitaa, Sura Na. 290. Kuhusu malipo ya vijiji na watu binafsi, malipo haya hulipwa kwa mmiliki wa eneo ambalo minara huwekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, malipo haya hayahusiani na malipo ya ushuru ambayo Halmashauri inatakiwa iyapate. Hivi sasa Serikali inakusudia kuwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa ili kuweka mfumo mzuri wa malipo, ushuru wa minara na mabango kwa watu binafsi katika Serikali ya Vijiji ili mradi uwe sawasawa kwamba kila Halmashauri iweze kunufaika na mchakato huo tunavyoenda katika ukusanyaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa suala zima la matumizi ya mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri. Jambo hili tumelielezea katika vipindi mbalimbali na Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele kulisimamia hili na kutoa maagizo. Katika bajeti ya mwaka huu tunasema itakapofika muda ulioagizwa katika hotuba ya mwaka wa fedha 2016/2017 tuliyoisoma hapa ambayo inajiainisha katika ukurasa namba 13 na 16, kwamba kuanzia Julai 1, 2016 kila Halmashauri zote zinatakiwa kukusanya mapato yake yote kwa mifumo ya kielektroniki. Baada ya mifumo hii kuanza hakuna Halmashauri itaruhusiwa kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge, sisi ni Wajumbe katika Mabaraza yetu, kila mtu akachukue nafasi yake kuhakikisha kwamba katika Halmashauri yake anakwenda kuweka misingi imara ili mwaka wa fedha 2016/2017 twende katika mfumo thabiti wa kuweza kukusanya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumetoa maelezo sehemu tofauti kwamba tulipotumia mifumo hii mabadiliko ya ukusanyaji wa mapato yamekuwa makubwa sana. Sehemu ambayo walikuwa wanakusanya shilingi 200,000 mpaka shilingi 300,000 kwa siku, mara baada ya kuweka mfumo huu watu wanakusanya zaidi ya shilingi 3,000,000 mpaka shilingi 4,000,000. Ni jukumu la kila Mbunge kuhakikisha sasa anaenda kusimamia eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Ofisi ya Rais - TAMISEMI, tunatoa onyo kwa watendaji ambao wataenda ku-temper na mifumo hii. Naomba niwaeleze, watendaji wote ambao watathubutu kwa njia moja au nyingine kwenda kuhujumu mifumo hii, tutahakikisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaenda kuwashughulikia kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala zima la Halmashauri irejeshewe 70% ya kodi ya ardhi badala ya 30%. Majibu ya hoja hii ni kwamba utaratibu wa kugawanywa kodi ya ardhi ya asilimia 30 kwa Halmashauri na asilimia 70 kwa Wizara ya Ardhi umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya sheria hii yanayopendekezwa pamoja na wazo la kuwezesha Halmashauri kubaki na mgao unaostahili kabla ya kuwasilisha Wizarani, mchakato huu sasa unaenda ambapo marekebisho haya ya sheria yatakapokamilika, jambo hili tutaliangalia sote kwa pamoja kuona ni jinsi gani tuliweke ili mradi Halmashauri ziweze kukidhi kupata mapato halisi katika suala zima la Kodi ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna hoja imejitokeza sana kuhusu suala zima la Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) juu ya uhamishaji wa Mfuko wa CHF. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia na Mwenyekiti wa Kamati alilielezea hili katika taarifa yake. Kwa hiyo, ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoko sasa, imeweka utaratibu wa hiari kwa kila kaya kujiunga katika Mfuko huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Wizara ya Afya inaandaa Muswada wa Sheria ya kufanya Mfuko wa Afya ya Jamii kuwa lazima. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi katika ngazi zote, wataendelea na jitahada mbalimbali za kuwaelimisha wananchi ili kuhakikisha kwamba wale wadau mbalimbali kama waendesha bodaboda, mamalishe, watu wa pikipiki, wafanyabiashara wadogo, basi wote mwisho wa siku waweze kujiunga katika Mfuko huu kwa ajili ya kuimarisha afya ya Taifa letu na wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililojitokeza ni kwamba, Serikali itoe fedha za Halmashauri ili kulipa madeni ya Wazabuni na Wakandarasi, kuondoa usumbufu kwa Halmashauri kutoka kwa wadeni wao. Hoja hii imejadiliwa na Wabunge wengi. Kama nilivyosema, Waziri wangu wa Nchi akifika hapa atakuja kutoa ufafanuzi mbalimbali kwa Wabunge wote waliochangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya hoja hii ni kwamba Serikali inatambua madeni ya Wazabuni yaliyopo, waliotoa huduma mbalimbali katika Serikali kuu, Halmashauri na Taasisi zetu. Serikali itahakikisha kwamba madeni hayo yataendelea kulipwa kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Aidha, Halmashauri zinaelekezwa kutoanzisha madeni mengine mapya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine iliyojitokeza kuhusu suala zima la ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Hii ilikuwa moja, lakini nilivyofuatilia nimeona ni watu wengi wamekuja na hoja hii kuhusu maeneo yao. Kwa hiyo, nijibu kwamba tuna Halmashauri zipatazo 44 ambazo ujenzi unaendelea na tumetenga kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850. Naomba nizitaje Halmashauri hizo kwa faida ya Bunge hili kwa sababu kila mtu atataka kujua katika eneo lake ni eneo gani limeguswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ambazo zimetengewa mgao huo kati ya Shilingi milioni 500 mpaka Shilingi milioni 850 ni Kalambo DC, Kyela DC, Bumbuli DC, Kaliua DC, Nkalama DC, Ikungi DC, Ushetu DC, Nyasa DC, Ilemela MC, Masasi DC, Gairo DC, Busokelo DC, Momba DC, Uvinza DC, Kakonko DC, Buhigwe DC, Mbogwe DC, Nyang’hwale DC, Njombe TC, Wanging’ombe DC, Makambako TC, Mlele DC, Msimbo DC, Mpanda DC, Simanjiro DC, Kiteto DC, Mkinga DC, Kilinda DC, Mpangani DC, Magu DC, Mtwara DC, Chamwino DC, Mafia DC, Kibaha DC, Msalala DC, Kahama TC, Butiama DC, Tarime DC, Chemba DC, Kibaha TC, Geita TC, Busega DC, Itirima DC na Bariadi TC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna Halmashauri mpya ambazo zimeanzishwa zipatazo 20 na ambazo zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambazo ni Busocha DC, Bunda TC, Chalinze DC, Handeni DC, Ifakara TC, Itigi DC, Kasulu TC, Kibiti DC, Kondoa TC, Madaba DC, Mafinga TC, Malinyi DC, Mbinga TC, Mbulu TC, Mpindwa TC, Nanyamba TC, Newala TC, Nzega TC, Songwe DC na Tunduma TC. Hizi zimetengewa Shilingi bilioni 2,140 ambayo inaenda kuanza ujenzi katika harakati hizo. Nimeamua kuzitaja hizi kwa sababu kila Mbunge hapa alikuwa anazungumza suala zima la ujenzi wa Halmashauri mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maeneo ambayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa nafasi niliyopata kidogo naomba niendelee kufafanua. Vile vile kuna suala zima la Chemba ambapo Mheshimiwa Felister Bura alikuwa anazungumzia kuhusu ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi wa majibu yetu unasema, Halmashauri ya Chemba imetenga eneo la ekari nane kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kupima eneo ili maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali hiyo yaanze.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala kwamba mradi wa umwagiliaji wa Gawaye, Manispaa ya Dodoma na Mradi wa Maji, Bahi ukamilishwe. Katika ufafanuzi wa hoja hii ni kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeendelea kukamilisha ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji katika Kijiji cha Gawaye kwa gharama ya Shilingi milioni 631.68. Kazi hii ya uwekaji mifumo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2016, ambapo jumla ya eneo la ukubwa la ekari 97 umekamilika kati ya ekari 100. Inatarajiwa kuwekewa mifumo hiyo ya umwagiliaji na kuwezesha wananchi kulima zao la zabibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile watu wamechangia katika eneo la elimu hasa katika suala la elimu bure. Kulikuwa na mawazo ambayo wengine wanasema suala la elimu bure halikuleta tija. Kikubwa zaidi naomba niwashukuru Wabunge wote. Karibu asilimia 99, kila Mbunge aliyesimama hapa alikuwa ana-appreciate suala zima la elimu bure. (Makofi)
MheShimiwa Naibu Spika, ni lazima tukiri, kuna wenzetu ambao ni maskini kabisa, hali ilikuwa ni ngumu. Leo hii ndiyo maana hata tulipoanzisha suala hili, kuna watoto ambao tumewasajili mwaka huu wana miaka 10 mpaka 11. Nini maana yake? Maana yake watoto hawa walikuwa wanakosa fursa ya kwenda shule kutokana na hali ya maisha yao. Leo hii tumekumbwa na tatizo la madawati kwa sababu idadi kubwa ya watu waliokuwa wanakosa elimu, sasa wameenda shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo la kuishukuru sana Serikali na Chama cha Mapinduzi na mtazamo wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekubali kutenga Shilingi bilioni 16.77 kila mwezi kwa ajili ya ruzuku katika eneo hili. Kwa hiyo, tunashukuru sana. Naamini kwamba jambo lolote lina changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.