Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia angalau dakika tano ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya dakika tano yale ya kitaifa nitayaandika kwa maandishi, naomba nijielekeze kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime. Kwanza niwapongeze kwa kuanzisha Kanda ya Simiyu ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma ya hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kiasi kikubwa sana ardhi yetu haijapimwa. Kwa hiyo ningependa niiombe Wizara iweze kuzingatia haya ambayo nitayasema ili waweze kuharakisha na kuhakikisha kwamba tunapata upimaji kwa kiwango kikubwa sana ambapo tukipima ardhi yetu inaongeza thamani na hata wale wananchi wanaweza kuitumia kuweza kukopa na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi, hatuna Afisa Mipango Miji, tuna surveyor mmoja tu, hatuna Maafisa Wasaidizi wa Ardhi. Kwa hiyo naomba Wizara, kuna vijana wawili ambao wametoka Chuo cha Tabora wameletwa pale kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa ajili ya ile kazi ya mfumo wa kodi wa ardhi na walikuja kwa mkataba na mkataba unakaribia kwisha; naomba kabisa Mheshimiwa Waziri waweze kuwaajiri wale vijana wabaki katika Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kupunguza hii adha ya wafanyakazi na kurahisisha upimaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ukosefu wa vifaa vya upimaji. Halmashauri ya Mji wa Tarime tunakodisha vifaa kutoka katika Halmashauri zingine kuja kufanya upimaji. Kwa hiyo naomba Wizara iweze kutupatia angalau set moja ya vifaa vya upimaji, kwa mfano differential GPS au hata total stations, tukipata set moja ya hivyo itaturahisishia upimaji katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na tuache kukodi kutoka kwenye Halmashauri nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, ningeomba Wizara iweze kutusaidia fedha ili tuweze kuandaa Master Plan kwa sababu Halmashauri ya Mji wa Tarime hatuna fedha za kutosha. Tukiandaa Master Plan itatusaidia, maana kuna miradi mingine tunaikosa, kwa mfano ya World Bank, kama hatuna Master Plan hatuwezi kupata hiyo misaada. Kwa hiyo, Wizara ione kwamba ni muhimu sana kutusaidia tuweze kupata. Halmashauri nyingi sana zinakosa miradi ya World Bank. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali kulikuwa na Mfuko ambao ulikuwa unaitwa Plot Development Revolving Fund (PDRF), tulikuwa tunaomba uweze kurejeshwa. Watukopeshe fedha tuweze kuzitumia kupima viwanja ambapo itarahisisha; maana yake kama nilivyosema awali, unakuta Halmashauri zingine hazina fedha za kutosha. Kupitia huo mfuko tunaweza tutakopa fedha, tukapima na kuweza kulipa fidia kwenye viwanja na itasaidia sana kuweza kuweka mji wetu uwe vizuri na hata Bunda nao wana changamoto kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho kwa kweli ningependa Wizara ya Ardhi iweze kuingilia ni mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Tarime wanaotoka Kata ya Nyamisangura na Nkende kwa maana ya Bugosi na Kenyambi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Jeshi la Wananchi wa Tanzania walichukua ile ardhi kinyume kabisa na sheria za ardhi; lakini mbaya zaidi tumeshuhudia zaidi ya miaka kumi hawapati fedha za kulipa fidia. Mheshimiwa Waziri ningependa kabisa na kipindi kile cha Wizara ya Ulinzi alisema atakuja Tarime, aje na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi ili aangalie uhalisia, wale wanajeshi warudi kule kwenye kambi yao na wananchi waweze kurudishiwa ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa kweli na mimi nichukue fursa hii kuwapongeza National Housing, wanajitahidi sana na wanastahili pongezi. Tunaona ni wapi wametoka na wapi walipo kwa sasa hivi. Kuna changamoto ambazo zipo na tumekuwa tukiziongea ambazo kama Wizara au Serikali wakizifanyia kazi tutaweza kupata zile nyumba ambazo tunasema za bei nafuu. Kwa sasa hivi walivyo ni kazi kwa kweli maana Serikali hawawapi ruzuku, wanajiendesha zaidi kama kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto zingine ambazo tumekuwa tukiongea kwenye kupata ile miundombinu ya kwenda kwenye makazi husika; waweze kupata urahisi kwa hapo maji, umeme na miundombinu ya barabara ambayo itaenda kuwarahisishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa ndugu zangu wa Mbarali na wenyewe wana mgogoro wa ardhi kati ya hifadhi na wananchi wale wakulima wa Mbarali. Mwaka 2007 walienda wakachukua vijiji 21, sasa hivi tena Serikali imeenda imeongeza beacon inachukua Vijiji 32 yaani wale wa Vijiji 21 walihamia kwenye Vijiji vingine na sasa hivi wanaondolewa tena. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba awazingatie na hao watu wa Mbarali nao waweze kupata haki yao ili hatimaye tuondoe hii migogoro ambayo unakuta kwa kweli haina tija na inakatisha tamaa; na tukizingatia wakati wa uchaguzi Chama Cha Mapinduzi kiliahidi kwamba watawajengea barabara ya lami sasa msiwahamishe hapo hawa wananchi. Ahsante sana