Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nijielekeze, kama wengine wote walivyosema, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Wana haki ya kupewa hongera kwa sababu kazi wanafanya na nchi inajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi sana lakini nina hoja kama tatu. Hoja yangu ya kwanza ni juu ya National Housing; National Housing kwa sheria iliyoiunda kwa miaka hiyo mingi iliyopita iliundwa kwa sababu kubwa, watu wa hali ya chini waweze kupata makazi ambayo bei yake ni nafuu. Hata hivyo inawezekana kwa sababu limekuwepo la muda mrefu tunawapongeza leo wanajenga nyumba nyingi zenye nafasi nyingi lakini zenye uwezo wa watu wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana anayetoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akaajiriwa kazi mahali fulani hana uwezo wa kupanga nyumba ya National Housing, ingawaje pamoja na kwamba msingi wake ulikuwa ni kutoa unafuu kwa wale wanaoanza maisha, wenye kipato cha chini. Ombi langu Mheshimiwa Waziri chini ya National Housing, hebu wafanye mara mbili basi, wajenge nyumba zenye uwezo wa watu wa vipato vya juu lakini wajenge nyumba zenye uwezo wa watu wa vipato vya chini. Kwa sababu Watanzania hawa wa vipato vya chini bado wanaishi mijini. Mfano mdogo Dodoma hapa, TBA ni Idara ya Serikali, National Housing ni idara ya Serikali, ukienda TBA nyumba yake, kwa Dodoma, Sh.150,000/= mpaka Sh.250,000/=. Ukienda National Housing pale Medeli, Sh.500,000/= mpaka Sh.600,000/=, ni walewale tu, na wote ni Mji huo huo wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ombi langu kwa National Housing, sitaki kuharibu kazi yao kubwa na nzuri wanayoifanya, lakini sisi wanyonge tunakwenda wapi mjini, tutapanga wapi, tunawekwa wapi? Mheshimiwa Waziri hilo anaweza kulifanya, wala halitaki maelezo marefu. Akiamua kufanya… (Makofi)

TA A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa. Ngoja nimpe faida tu. TBA ni shirika ambalo lipo chini ya hao na National Housing. Hebu nenda pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uone yale majengo ya kulala wanafunzi, amejenga TBA, kwani yeye hakununua saruji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba National Housing, basi taarifa yake kama inalenga kule, Mheshimiwa Waziri, pale Dar es Salaam tuna nyumba Upanga, Tabora zipo, Bukoba zipo, tulizorithi mwaka 1967, hazina ukarabati zinaongezekaje bei? Kwa nini? Kwa sababu iko wazi kabisa, zipo nyumba za asili zilizoanzishwa National Housing hata ukarabati haufanyiki ingawaje wanazikopea kujenga nyumba nyingine. Kwenye ile mikopo wanayokopa si warudishe na huku ndani basi nyumba angalau ziwe nzuri na wote tunaoishi mjini tunazijua. Kwa hiyo, bado natetea hoja yangu; tunavyosihi mjini bado kuna watu uwezo wa kupanga ni wa shida lakini wana haki ya kukaa kwenye nyumba za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; huyu amenitoa kwenye mood; suala la kibenki. Mheshimiwa Waziri, mtu yeyote anapokwenda kukopa benki kwa kawaida lazima apeleke hati benki na anapokwenda kukopa benki, kama ni mke na mume watasaini wanakubali mkopo. Wakishamaliza kukopa, Wizara ya Ardhi inasajili ile hati kwamba hii hati iko benki kwa sababu ya mkopo; tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anashindwa kulipa mkopo wa benki, nyumba inaenda mnadani, watu wanakimbilia mahakamani. Tatizo langu linaponipata, wanatoka tena mahakamani wanakwenda kuweka caveat kwenye nyumba ambayo walienda kukopa, benki imeuza, inakuwaje sasa? Kwani ile hati huwa inakwenda pale Ardhi mnahalalisha kwamba ana haki ya kukopa kwa nini? Nyumba ina mkopo, inawezaje tena kwenda kuwekewa caveat?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linasumbua benki zisikopeshe watu wanaofanya biashara kwa sababu sasa wanakuwa hawaaminiki. Maana unakopa, kurudisha umeshindwa, mali yako inauzwa unakwenda kuzuia isiuzwe mahakamani, unakwenda kuzuia ardhi na ardhi mnapokea, lakini picha zipo, kila kitu kipo. Kwa nini sasa ardhi hii badala ya kuwalinda benki kama wafanyabiashara inawaingiza kwenye matatizo kwa kutoa hati ya kwanza ya akope na hati ya pili mtu akaweke caveat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, Mheshimiwa Lukuvi, tunaposema kupima, halmashauri zinapima lakini asilimia 30 hairudi kwenye halmashauri hizi. Wakishakusanya ile kodi wawarudishie, kwa sababu wakiwarudishia ile kodi watawapa msingi wa kuendelea kupima ili viwanja viwe vingi. Halmashauri inapima, pesa inalipwa ila asilimia 30 hairudi, sasa hii halmashauri wanaisaidiaje na tunasema tupime maeneo mengi? Wakati mwingine sehemu nyingine hela ya miradi inapatikana, lakini tunazo halmashauri za vijijini ambazo uwezekano wa ku- expand kuendelea kupima, hela ile isiporudi hawawezi kupima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo hoja yangu na ushauri wangu katika Wizara hii, kazi kubwa wanafanya, wala haitakiwi kutiwa doa, lakini wawaarudishie hizi halmashauri ili ile asilimia 30 iweze kuwapa nguvu ya kuendelea kupima katika maeneo yao. Nina uhakika suala hili nina imani ataamua, siyo akiamua, anaweza tu, hata akisema kwenye majibu yake kesho watatekeleza tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niligusie hilo walilosema wengi. Ni kweli tusipokuwa na sababu za kuwa na maeneo maalum ya kilimo na yakalindwa na yakatunzwa yasibadilishwe matumizi, kizazi kinachokuja kulima itakuwa shida sana. Itakuwa shida kwa nini, kama kuna mtu anataka kujenga nyumba si aende maeneo kavu kule ajenge? Hata hivyo, sehemu hii ina maji inaweza kumwagiliwa. Mheshimiwa Waziri, kama walivyosema wengi, hebu aangalie eneo la kisheria fulani. Otherwise, kwa sababu hali ya tabianchi inabadilika, mambo yanabadilika, tutakuja kujikuta sehemu ya kulima sasa kwenye mito na nini haipo, watu wamejenga kwa sababu wana hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hapo kwa kuunga mkono hoja, nawapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ahsanteni sana.