Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka nipongeze Serikali kwa kuleta mkataba huu, niseme tu kwamba mkataba huu umechelewa sana. Sisi kule Tanga tumepoteza vijana wengi sana kwa sababu ya kuchelewa kusaini mikataba kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wengi walikuwa wanajihusisha na shughuli za madawa ya kulevya wanapozamia kwenye meli kwa ajili ya shughuli za ubaharia. Kwa mkataba huu naamini sasa kwamba kwa kuwa kazi za ubaharia zinaenda kutambuliwa rasmi ndio utakapoona tofauti kwa kazi ambazo ni rasmi na zile kazi za kishoka utaweza kuona kwamba tukiwa na mikataba rasmi kama hii basi shughuli nyingi zitakazofanyika zinalinda pia maslahi mapana ya usalama wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kushauri Serikali kwamba kwa kuwa mkataba huu ni wa Kimataifa na pia tunayo maziwa katika mipaka yetu na mipaka hii tunapakana na nchi mbalimbali. Kwa upande wa Ziwa Victoria tuna Kenya na Uganda; Ziwa nyasa kuna Malawi na Zambia; na Tanganyika kuna Burundi na Congo na hapa nimeona Congo wameridhia mkataba huu mwaka 2015. Nitoe rai kwamba kwa kuwa nao kwenye maziwa haya pia kuna vyombo hivi vya usafirishaji basi tujaribu ku-harmonies na hizi sheria pia zitumike kwenye vyombo ambavyo vinasafiri katika maziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumejifunza kwenye Kamati kwamba wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wana chombo maalum cha kusajili vyombo vya majini, sasa huku kwetu tuna SUMATRA ambao wanasajili vyombo vya majini na vyombo vya nchi kavu. Ningependa sasa kuishauri Serikali kwamba ifikie mahali tutenganishe hivi vitu kwa sababu tunaona mara nyingi sana kwenye maziwa huku kunatokea maafa makubwa labda ni kutokana kwamba SUMATRA wako busy zaidi na vyombo vya nchi kavu kuliko vyombo vya majini. Kwa hiyo, nitoe rai kwamba kwa kutumia mkataba huu sasa tuweze kupanua wigo wa kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo niseme kwamba hii ni fursa nzuri sana kwa vijana wetu kupata ajira, lakini ni fursa nzuri pia kwa utambuzi wa Kitaifa kama alivyomalizia msemaji wa mwisho hapa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa inatumia wakala kusajili meli na ndiyo maana unakuta wakati mwingine hata hizi meli zinahusishwa na uharamia, lakini pia zinahusishwa na mambo mabaya ambayo yanachafua taswira ya Taifa. Sasa ni imani yetu kwa mkataba huu kila kitu kitawekwa katika utaratibu ambao ni mzuri kwa ajili ya kulitangaza Taifa letu katika Mataifa ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono azimio hili.