Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JUMA S.NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kunipa nafasi hii, ili na niweze kuchangia kwenye Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kunijaalia kuwa na afya njema wa Bunge wote katika Bunge hili la Jamhuri ya Mauungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Dkt. Mpango na dada yangu Dkt. Ashatu kwa bajeti nzuri sana, bajeti ambayo inaonekana dhahiri kwamba ikitekelezeka nchi yetu itafikia hatua nzuri sana ya maendeleo. Bajeti ambayo inamgusa kila Mtanzania kwa nafasi yake, mkulima, mfanyakazi, mwanafunzi na Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, bajeti hii sasa iende kwenye maeneo yaliyodhamiriwa. Watanzania wengi tatizo kubwa maji, nashangaa leo Mbunge wa Pangani, Mto wa Pangani umepita katikati ya Mji wa Pangani lakini wananchi wanalia maji. Chemba kule tuna matatizo makubwa ya maji, fedha ziende kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji. Tukimaliza hili, twende kwenye tatizo la nishati ya umeme; wananchi wakiona mambo haya yanafanyika naamini kabisa kwamba nchi yetu itaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, ninasikitika kwamba kuna Mbunge mmoja hapa, nisingependa kumtaja jina, alisema barabara ya lami ya kutoka Dodoma kupita Chemba, Kondoa kwenda Arusha haina manufaa kwa wananchi wa Chemba.

Wananchi wameniambia nimsihi tu kwamba, kama yeye hapendi kupita kwenye barabara apite porini. Eeh! Lakini Wabunge wa Arusha, Manyara na kwingine kote, wanaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukitoka Arusha, Dodoma masaa manne, lakini mtu anabeza juhusi za Serikali katika kuhakikisha kwamba barabara hii imejengwa kwa kiwango cha lami. Mwenyekiti wewe ni shahidi ulipotoka Moshi kupita hapa, ulipokuja hapa ukasema hivi ile ni barabara ama kiwanja cha ndege. Vijiji vilivyoko karibu na barabara hii maisha yao yameanza kubadilika kwa wale wanaojishughulisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu hajishughulishi anasubiri barabara ile iende mpaka chumbani kwake, haiwezekani. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba ni vizuri tuunge mkono juhudi za Serikali zinazofanywa bila kujali tofauti yetu. Maslahi ya Taifa hayana mgawanyiko, maslahi ya Taifa lolote hayana mgawanyiko, ningeomba pia bajeti hii ijielekeze zaidi kwenye elimu. Pia ni vizuri mkafanya analysis kidogo kuhusu fedha zinazo kwenda kwenye shule hizi za msingi huko vijijini, zinafanya kazi iliyokusudiwa? Nina wasiwasi kwamba inawezekana fedha nyingine zina kwenda huko kwenye hili suala la elimu bure bado fedha zile hazifanyi kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri niliwahi kusema nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza hapa hebu lete kwenye financial bill ile tozo ya ving’amuzi ili TBC iweze kuendelea. Muache kutoa fedha kutoka Hazina kupeleka TBC ichukuliwe fedha ya ving’amuzi ambayo itakwenda kuendesha shirika la umma lile. Na mimi nitakuwa mwizi wa fadhila nisipompongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye hili suala la makinikia. Nitoe rai kwa Wabunge wenzangu kwa wana CCM wenzangu wote tunakadi za kijani hakuna mwenye kadi ya kijani zaidi ya mwingine, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wapinzani maslahi ya Taifa hayagawanyiki, tuungane sote, Mheshimiwa Rais ameonyesha jambo jema baada ya kuunda tume zile mbili.

Kwa mliosoma mambo ya negotiations, kuna aina mbili za negotiation baada ya jambo hili. Kwa kuwa sasa sisi kama Taifa tumekuwa na power kwenye negotiation itakayofuata kwenye compromise negotiation, nina amini kabisa tutafaidika na jambo hili. Jambo hili linahitaji umakini mkubwa sana, ni jambo linalohitaji akili ya kutosha Mheshimiwa Rais ameshaonyesha njia, nina wasiwasi kwamba inawezekana kabisa tusipate ile trilioni 1.08; kwa sababu ni suala la negotiations. Lakini tunapokuja kwenye mjadala huu automatically kwenye win win situation nchi yetu itafaidika. Ndio maana nikasema wapinzani, wana CCM tuungane pamoja tum-support Mheshimiwa Rais kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hawa wachimba madini wanakwenda kuweka mgodi mkubwa sana kule Chemba, endapo jambo hili litafanikiwa na tukawa na win win situation, automatically hata wananchi wa Chemba watapata mafanikio kwenye huo uwekezaji unaokuja kule Chemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni suala la kisheria, mimi sio mwanasheria, lakini kwa kuwa sio kuku na sitagi mayai lakini najua yai viza ni lipi? Tufike mahali, si rahisi na siamini hivyo kwamba mikataba ikusanywe na maroli iletwe hapa Bungeni siamini. Kinacholetwa Bungeni ni muswada wa sheria sisi Wabunge tusimame kuhakikisha kwamba tunabadilisha Muswada wa Sheria ili nchi yetu iweze kufaikika kutokana na madin haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nashangaa kusikia Mbunge anasema leteni mikataba hapa Bungeni, maana yake unazungumza maroli mawili/matatu na hilo sio jukumu la Bunge, jukumu la Bunge ni kutunga sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba endapo sheria hii ikija wote tuungane pamoja wapo wanasheria humu watusaidie tuone ni namna gani nchi yetu inaweza kupata mafanikio kwenye suala hili la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana nikasema Mheshimiwa Rais ameonyesha ujasili wa hali ya juu sana, lazima tumuunge mkono, lazima tushikamane wote wapinzani, wana CCM na ndio maana nikatoa mwanzoni nikasema sisi wote Wana-CCM hakuna mwenye kadi ya kijani zaidi kuliko mwingine lazima tuungane wote tu kwa sababu kadi zetu wote zinafanana. Niombe na wapinzani tuungane kwenye jambo hili na nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Msingwa aliposema suala la maslahi ya Taifa halina mgawanyiko mimi chama fulani, mimi chama fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bomba la mafuta kutoka Uganda linapita Singida, linapita Chemba linakwenda Tanga. Naomba ajira zitolewe kwa watu wa maeneo hayo, lakini pia wananchi waelezwe mapema litapita kwenye vijiji vipi? Sambamba na hilo ile barabara ya Handeni, Kiberashi, Kibaya, Chemba, Donsee, Lalta, Farkwa, Kinyamshindo hadi Misung’aa kule kwa Mheshimiwa Tundu Lissu ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami kazi ianze sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha.