Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nitaanza kwa kuzungumzia suala zima la ripoti ya madini kwa ufupi, ili kuweka rekodi sawa.

Suala la wizi kwenye sekta ya madini ni suala ambalo wapinzani kwa muda mrefu sana wamekuwa wakilizungumza na endapo kama tungesikilizwa leo hii tusingekuwa tunazungumzia wizi wa takribani miaka 19 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkutano wa Bunge uliopita, niligusia pia suala hili kwa maana ya umuhimu wa kuweka mikataba wazi na pamoja na sababu nyingine nyingi nilizozitaja pia nilisema kuna umuhimu kwa sababu sisi ni member kwenye organizations ambazo zina-deal na masuala ya Open Governance mfano EITI, lakini pia na OGP yaani Open Governance Partnership.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza wale walio-initiate wizi huu kwenye makinikia wafikishwe kwenye vyombo vya sheria lakini pia wachukuliwe hatua, lipo jambo la msingi sana ambalo naomba nimshauri kwa upendo kabisa. Experience is the best teacher. Kwa sababu kuna uzoefu ambao umewahi kujitokeza mwaka 2012 ambapo kulikuwa kuna Balozi mmoja anaitwa Mahalu alipelekwa kizimbani kwa kosa la ufisadi wa bilioni 2.5 na alipofika kizimbani akajitetea kwa kusema kwamba yale yote ya ununuzi wa jengo lile ambalo alikuwa amelinunua yalikuwa ni maelekezo kutoka kwa mwajiri wake, na kesi ikawa imeishia hapo. Sasa huu ni uzoefu tu ambao umewahi kujitokeza. Napenda nimshauri Mheshimiwa Rais kwamba ili kuweza kuweka mbivu na mbichi hadharani ni bora atoe immunity kwa mapapa ili suala hili liweze kutendeka kwa haki, siyo kuonea vidagaa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la IPTL. Pamoja na kuwepo na ufisadi mkubwa sana kwenye madini na gesi, lakini bado kuna ufisadi mwingine mkubwa kwenye umeme. Wabunge wa awamu iliyopita watakuwa mashahidi na watakuwa wana kumbukumbu nzuri kwamba miongoni mwa maazimio ambayo waliwahi kuyaweka wakiwa kwenye awamu ile ni pamoja na mtambo huu wa IPTL kutaifishwa. Nasikitika sana mpaka hivi sasa mtambo huu wa IPTL bado Serikali inapiga danadana kuutaifisha.

Mheshimiwa Mwneyekiti, nataka Serikali itoe majibu ni kwa nini mnapiga danadana katika hili wakati mna baraka zote kutoka kwa Bunge, wakati mna baraka zote kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ambayo imehukumu kesi na tunadaiwa takribani bilioni 400 na huu ni mzigo wanaenda kuulipa walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni vema mkatambua kwamba Bunge ndiyo Supreme organ of the State. Pale Bunge linapofanya maamuzi au maazimio ni vema mkayatekeleza kwa sababu mnatengeneza mazingira ambayo tunashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna swali la kujiuliza hapa, hivi mnashindwa kutaifisha mtambo wa IPTL kwa sababu gani? Je, ni kwa sababu huyu mmiliki wa IPTL singasinga anawachangia kwenye kampeni zenu au ni kwa sababu gani? Ni huyu Singasinga amewaweka mfukoni? Ni sababu ipi inasababisha mtambo huu wa IPTL ambao unatupa wakati mgumu wananchi wa Tanzania, walipa kodi wananyanyasika kwa ajili ya mtambo huu na Serikali mnaendelea kupiga danadana kwenye mtambo huu? Kuna kitu gani ambacho kimejificha?

Mheshimiwa Rais kama ameweza kuzuia makontena ya mchanga, siamini kama anaweza akashindwa kuzuia IPTL au kuifungia IPTL, labda kuwe kuna sababu ambayo imejificha. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aseme sababu ni nini? Kwa nini IPTL mnashindwa kuifungia na wakati inatupa mzigo mkubwa sana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala la benki ya FBME, nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia ukurasa wa 15. Ni mambo ya aibu sana, nimeona sababu kubwa ya benki hii kufungwa ni uchunguzi uliofanyika kutoka Marekani. Karne hii unazungumzia uchunguzi kutoka Marekani toka mwaka 2012 benki hii imekuwa reported kwamba inatakatisha fedha, lakini mnakuja mnasubiri uchunguzi kutoka Marekani, Financial Intelligence Unit wako wapi? PCCB wako wapi?

Usalama wa Taifa na wengine mko humu ndani mko wapi? Kama mnashindwa ku-deal kwenye vitu sensitive kama hivi tunaachaje kuamini kwamba kazi yenu kubwa Usalama wa Taifa ni kuudhoofisha upinzani? Tunaachaje kuamini kama kazi kubwa ya Usalama wa Taifa ni kufanya mambo ya ajabu ajabu ambayo yanaendelea kwenye Taifa letu. Haya mambo ni ya aibu sana na si mazuri sana kuyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kuhusiana na suala hili, kama tatizo lipo kwenye hii kikundi cha Financial Intelligence Unit kuna mambo mawili ya kufanya, moja ni kukiondoa kikundi hiki na kukiweka kingine, kama hiyo haiwezekani basi muandae programu maalum kwa ajili ya kuwapa watu wetu hawa mafundisho waweze kuwa na uwezo mkubwa wa ku-deal na vitu kama hivi ambavyo ni muhimu sana. Ni aibu sana kwa Taifa letu leo hii tunakaa tunasubiri uchunguzi kutoka Marekani, karne hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na FBME, hivi mnasubiri nini kufungia Benki ya Stanbic? Nini kinawafanya mchelewe kuifungia Benki ya Stanbic au mnasubiri pia uchunguzi kutoka Marekani? Wakati PCCB wame-prove kwamba Benki ya Stanbic ilifanya miamala ambayo ni ovu, na wakati CAG ripoti yake ime-prove kwamba Stanbic ilifanya miamala ambayo ni haramu. Serikali inasubiri nini? Kwa nini msichukue hatua? Kwa nini mnakuwa mnategemea tafiti na uchunguzi kutoka sehemu nyingine? Kuna mambo ambayo kwa kweli hata ukiyazungumza yanatia aibu, ni vema tukajitathmini upya, tunakosea wapi? Tunakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka sana nimalizie kwenye suala la kodi. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake kuna page fulani amezungumzia kuhusiana na easy of doing business kwamba Tanzania tumefanya vizuri sana, your right, uko sahihi, lakini unaangalia tumefanya vizuri ukilinganisha na akina nani? Ukiangalia kwenye nchi washindani mwekezaji anapokuja au mfanyabiashara kuna vitu anavizingatia anapokuja kuwekeza. Tanzania ndio nchi inayofanya vibaya katika nchi za East Africa kwenye suala la access of financing na kwenye suala la tax rates, viwango vya kodi ni vikubwa. Haya ndiyo mambo ambayo mfanyabiashara Mwekezaji akija kuwekeza kwenye Taifa ni mambo makubwa anayoyazingatia na ndio mambo ambayo tunayafanya vibaya kuliko mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri pale mnapokuwa mnajidai na kujitutumua kwamba tumefanya vizuri, ukilinganisha na mataifa mengine, kwa kweli sisi siyo Taifa la kuendelea kujilinganisha na Mataifa kama ya Burundi, tunafanya vibaya kweli na nina taarifa hapa kutoka PriceWaterHouseCoopers ndio takwimu hizi zinaonyesha tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema sasa Serikali kupitia hotuba yake nzima na mambo ambayo imepanga ikajitathmini upya. Hivi ni vitu gani ambavyo nyie mnavipa kipaumbele? Ni vitu gani ambavyo hamvipi vipaumbele? Kile ambacho mnakihubiri kila siku, kile ambacho mnakisema kila siku, siyo kitu ambacho mnakipa kipaumbele. Ukiangalia kila siku mnahubiri uchumi wa viwanda lakini mnaelekea kwenye maeneo mengine ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na uchumi wa viwanda ambao mnaouhubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ni msingi na ni muhimu sana katika kwenye uchumi wa viwanda ni pamoja na umeme. Tuna megawati 1,051 ni aibu, tuna makaa ya mawe yamerundikana Liganga na Mchuchuma takribani milioni 480 lakini hakuna kinachofanyika hapa, mnahubiri viwanda, viwanda vinatoka wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yanasikitisha sana, naomba nimalize kwa kukushukuru.