Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo jioni hii. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kusimama hapa yote hii ni rehema zake na wala sio lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwanza kwa kusema ninashukuru kwa bajeti tuliyoletewa hapa na kwa sababu kuna mengi ya kuzungumza nataka kutoa na mimi mawazo yangu kama yataonekana ya maana naomba Mheshimiwa Waziri uyazingatie. Katika bajeti hii limezungumzwa sana na katika Bunge hili na awamu hii na Serikali yetu tumezungumza sana habari ya viwanda. Mimi nataka nikupe maeneo matatu ambayo binafsi nahisi kwamba tukienda sawa tunaweza kupiga hatua kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumza habari ya kiwanda cha General Tyre, Arusha. Lakini cha kusikitisha ni kwamba tunaishia kwenye kuzungumza. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara. Binafsi tumefanya ziara kule siyo chini ya mara tatu kwa kuona umuhimu wa kiwanda kile kufufuliwa. Sote tumefika hapa kwa kutumia gari na ili gari lizunguke au litembee lazima litumie tairi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kile kingefufuliwa yale matairi, magari ya Serikali na mashirika ya umma tu wakawa yanatumia matairi yanayozalishwa na General Tyre ingekuwa tayari ni soko moja kubwa. Lakini kwa bahati mbaya sana imekuwa ni hadithi, hakuna utekelezaji katika jambo hili. Naomba sana leo hii ukichukulia idadi ya tairi za piki piki zinavyotumika nchi hii, tena tairi kutoka China sizizo na viwango, ajali sizizo na msingi zinatokea, magari yanapata ajali kwa matairi ambayo yanaingizwa, kwa hiyo, soko la matairi ndani ya nchi hii, wacha kiwanda cha General Tyre hata vikizaliwa vitatu bado Tanzania tuna demand kubwa ya matairi, hebu fikirieni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka nizungumzie kuhusu Kiwanda cha Tanga Fresh. Kiwanda cha Tanga Fresh kimekuwa kikiandamwa na majanga mara kwa mara nilimsikia Mheshimiwa Kitandula akizungumzia kuhusu vikwanzo ambavyo wanavipata, Waheshimiwa wale wa Kiwanda cha Tanga wameshindwa hata kupata mikopo ya benki kwa sababu eti kuna waliowauzia majengo yale kwamba TRA wanawadai wale wahusika. Anayedaiwa siyo wanunuzi, wanaodaiwa ni waliouza. Leo iweje kiwanda kile kinakuwa kila siku kiko ndani ya taabu. Mkumbuke kiwanda cha Tanga ni tegemeo kubwa sana kwa watu wa Tanga, wafugaji wa Tanga wanakitegemea kiwanda kile kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba kimetoka kwenye mdomo wa FCC wakikishutumu kwa muda mrefu sana kuhusu kukiuka kwa baadhi ya mambo kikawa kiko ndani ya matatizo, wamekuja sijui ni TBS sasa hivi wamekuja TRA.

Mheshimiwa Waziri unajua kwenye meza yako iko barua ya kiwanda kile kutaka kusaidiwa kufanya kazi zake kwa uzuri, tuvilee viwanda vyetu. Naelewa kwamba kuna viwanda vya Kenya, Brooklyne ambao hawapendi kuona Tanga Fresh ni washindani wao wakubwa. Leo Tanzania tuna kiwanda cha Tanga Fresh na Asas ndiyo viwanda vikubwa vya maziwa. Lazima tuvilee, uzalendo uanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie A - Z na mnaelewa kuna tatizo gani. Kuhusu rate yao ile ambayo wamewekewa. Nawaomba sana Malaria ni janga la kitaifa na lazima tulikuwa kwenye semina pamoja na Naibu Waziri alisikia malalamiko ya kiwanda kile ambayo ina hatarisha kwenda kufungwa na kupunguza idadi kubwa ya wafanyakazi katika kiwanda kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani michango hiyo mitatu kwenye kusaidia bajeti yetu inatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kauli ambazo zimekuwa zikitawala sana kuhusu makanikia. Kiongozi mwenza wa UKAWA Mheshimiwa Francis Mbatia aliongea kwamba katika sisi hakuna anayepinga jitihada za kunusuru mali za Taifa hili. Kama limesemwa hilo na Mwenyekiti wetu na hakuna aliyempinga maana yake ni kwamba hayo ndiyo mawazo yetu. Wasijitokeze wengine wakatulisha maneno kuonekana kwa Watanzania kana kwamba tunapinga juhudi za kulinda mali zetu. Hiyo ndiyo ajenda yetu siku zote na tumekuwa tukiwaambia hivyo. Lakini kwa sababu yalitoka upande huu mliyaona siyo. Sasa mme-prove ndiyo twendeni mbele, tusiangalie nyuma tena, tuko pamoja katika hili la kulinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani kila mtu ana-style yake ya kulipokea jambo. Wenzetu mnakimbilia sana sherehe celebrate festivals. Sisi kwanza tunapima upepo kuona mambo yanaendaje.

Waheshimiwa Wabunge niwape mfano, Bunge la Katiba mlisherehekea sana. Wengine wakakata viuno humu ndani lakini Katiba iko wapi mpaka leo. Hamkutosheka mkaenda jamhuri mkacheza na mkaimba, Katiba iko wapi mpaka leo. Kwa hiyo, si hoja awali, ni heri hatima. Hayo sisi wengine tunaota ndoto kubwa kwa pesa zile zilizotajwa tunatamani yatokee na Tanzania inufaike na yale yaliyozungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tunapozungumza haya wengine mnatupa majina mabaya. Yuko Mbunge mmoja kule alinyanyuka akatuita sisi UNITA akamfananisha Kiongozi wetu na Savimbi. Lakini nawaonya wanasiasa wenzangu, majina mabaya tusiitane kiasi hicho, kwa sababu leo upo huko inaweza ika-change ring ukaja huku. Wako viongozi wakubwa walikuweko huko leo tunao huku na wako wengine tulikuwa nao huku leo wako huko. Haya ni mambo ya mbadilishano tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu anatuita sisi UNITA, lakini mimi nakumbuka Bunge la Katiba alikuwemo Mheshimiwa mmoja anaitwa Ibrahimu Lipumba aliwaita ninyi Intarahamwe. Leo Intarahamwe katafute Intarahamwe mwenzio wamekwenda kukaa nao. Ni suala la muda la muda tu kwa sababu anakamilisha kazi aliyopewa ni rasmi tu atakuwa Mkuu wa Mkoa, atakuwa Mkuu Msaidizi wa Gavana tunayaelewa hayo. Tunamwombea safari njema. Akamilishe kazi yake aliyotumwa arudi akaye na Intarahamwe wenziwe. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuhusu misaada ya wahisani. Hili nisingetaka kulizungumza kwa sababu ninapozungumza wahisani nitaigusa Zanzibar na nikigusa Zanzibar nitagusa uchaguzi wa Zanzibar na najua kuna watu hawataki nizungumze uchanguzi wa Zanzibar, lakini hili haliepukiki. Mwanzo nilisema Uchaguzi wa Zanzibar ni chozi la mbwa mmelikosea kulinywa moto, halitaweza kunyweka tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hivi, kwenye bajeti yako hii asilimia 12.5 umetegemea fedha za wahisani. Fedha za wahisani kwenye bajeti iliyopita unatuambia haikutoka na ndiyo ukweli. Leo umerudi umeandika tena humu kwamba unategemea asilimia 12.5 ni fedha za wahisani. Wahisani wamegoma kutoa pesa na sababu mnaijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi uliofanyika Zanzibar na Sheria ya Mtandao yanainyima nchi hii fursa ya kupata fedha zile za kuisaidia bajeti. Nisingeshughulika sana kama ingekuwa ni pesa ambayo haimo kwenye bajeti ningeacha kusema hilo. Hasa mimi nawashauri Wahisani wanaozuia kutoa pesa zile wazungumza na ninyi lakini ninyi mnashindwa kufika point. Mnashindwa kufikia makubaliano nawaomba sana, fursa hii wa sababu ya kumlinda Daktari Mohamed Ali Shein.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limeshafutika hilo halipo. Ahsante sana nawaambia Waziri wa Mambo ya Nje anajua masuala anayokumbana nayo
msaidieni. Kubalini na eleweni nini kimetokea. Uchaguzi ulifanyika tarehe 25 Oktoba, ndiyo huu uliomuweka Rais John Magufuli madarakani tunamtambua, wala hatupingi kwa hilo, lakini uchaguzi mwingine ule, uchaguzi wa Zanzibar umefanyika matokeo ndiyo yametuweka sisi Wabunge humu. Eti chakula kimepikwa jungu moja wa chini umeiva wa juu haukuiva mmeyaona wapi. Haya ni maajabu ya dunia, uchaguzi uliisha na matokeo wahisani yote wanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ilikuwa inaangazia uchaguzi wetu na waliona, leo Mheshimiwa Jecha maana afadhali ingekuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilifuta uchaguzi ule, lakini Tume ya Uchaguzi haikufuta, Jecha alitoka pale akaenda akakaa kwake sijui siku hiyo aliwekewa kikuba gani na mkewe akakinusa akaenda chafya, akafuta uchaguzi wa Zanzibar. Huu ni upumbavu ambao unatutesa ndani ya nchi. Unatutesa kwa sababu sisi tunaumia sana. Nchi hii inayo bajeti yetu ni high jump, hatukufikia asilimia 29 tumeweka 30 na leo mchezo wa high jump mrukaji anaanzia chini kwenda juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mara hii ya Mheshimiwa Mpango sasa pale alipokuwa hakufika kapandisha ule mti juu zaidi ili aruke, sasa sijui maajabu ambayo yatatumika. Sielewi maajabu gani yatatumika, mimi nakuombea dua sana. Lakini nakuomba kaaeni mtafakati suala la Zanzibar dunia inatuangalia. Suala la mitandao dunia inawangalia, tumalizeni tufaidike, za makanikia bado zina muda. Mimi yalaiti ingekuwa zile za makilikia zinatoka katika kipindi hiki ningesema tuwaache Wazanzibar waendelee wanavyokwenda, maamuzi yao yadharauliwe. Lakini kwa sababu ya tunategemea wahisani lazima muukubali ukweli hata kama ni mchungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yuko mwanafalsafa mmoja alisema usiyempenda akisema maneno mazuri yakubali, na unayempenda anaposema mabaya uyachukie.