Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi naomba nimalizie fursa ya kuchangia kwa dakika kumi halafu tutaendelea na huo mfumo wa dakika tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nichukue fursa hii kuipongeza Serikali, nimpongeze pacha wangu hapo Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Ashatu, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango, lakini pia nimpongeze Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake nzima ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia labda huenda dakika tano zikawa hazikutosha basi mimi nasema naanza na kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongelea mambo makubwa matatu ama manne, kwanza ni suala lile la shilingi milioni 50 kila kijiji. Unajua ile ni ahadi yetu kwenye Ilani na tumefika kule tumejitangaza vizuri na kila mtu anasubiria. Kwenye bajeti hii hakuna lililoongelewa. Mwaka jana tuliambiwa na pesa kiasi cha shilingi milioni 59 zitatengwa, mwaka huu kimya kabisa. Hebu tusaidieni tunaenda kujibu nini na ni ahadi ambayo tumeitoa, hii nafikiri haijakaa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, itabidi niende haraka ni zile shilingi milioni 40 ambazo kwenye hotuba tumezungumzia kwa maana ya suala zima la road license. Mimi nataka nishauri badala ya kusema road license ambayo itapeleka mzigo mkubwa sana kwa wananchi wengi ambao hawatumii hayo magari, ile shilingi 40 ifanywe tuiweke kwenye mfuko wa maji, wengi wamezungumza hiyo. Isiwe shilingi 40 turudishe iwe shilingi 50 badala ya shilingi 40 iingie kwenye Mfuko wa Maji, kama tutatenga kidogo katika hicho kisehemu ika-cover kwenye suala la road license sawa lakini maji hata ukiweka, najua mafuta yanaongeza gharama kwenye kila kitu lakini kama yanaongeza gharama halafu unaenda kuwapatia wananchi wa kawaida maji umefanya jambo jema kabisa na jambo kubwa. (Makofi)
Nafikiri hiyo itakuwa imeondoa sintofahamu ambayo Wabunge wengi wameongelea hapa. Nawaomba sana tulitafakari hilo na tulielekeze huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nimeona kwenye hotuba yako viashiria vya uchumi jumla; takwimu zote zinaonesha uchumi upo vizuri na tunakwenda vizuri kadri ya taarifa yako sawa, lakini hali halisi kwa wananchi huku ni kitu tofauti kabisa hasa wananchi wale wenye hali ya chini, wa kati na hata wale wa juu, hali halisi ya mzunguko ile tumezungumzia mzunguko wa fedha kuwepo ni ngumu kweli. Nakuomba Mheshimiwa Waziri hebu tufafanulie, huenda sisi labda upande huu wa masuala ya fedha hatuko vizuri sana lakini tuelezee hivi hii hali unaielezaje. Viashiria vyote viko vizuri sana na tunaelekea vizuri, lakini uhalisia hauko sawa, hauko vizuri ni kilio kila mahali, mfanyabiashara wa kati na chini kila mmoja analia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne nimeona tunafanya kuboresha kwenye kuondoa kodi za bidhaa kwenye bidhaa ambazo tunataka walau tu-promote, kwa mfano kazi zetu kama lile la upande wa vyandarua na hasa vyandarua vilivyowekwa viuatilifu vya malaria. Tuna dhamira ya kwenda kuondosha malaria moja kwa moja, vyandarua vinavyotengenezwa ndani vina Kodi ya Ongezeko la Thamani wakati vinavyotoka nje huenda havina, hivi una mfanya vipi huyu mtu aweze ku-compete na wale wa nje? Ili tuweze kuwapa incentive hawa wetu wa ndani wanaoweza kuzalisha hivi waweze kwenda kutusaidia kuondoa malaria basi vyandarua vile vyenye viuatilifu vya kuua wadudu wa malaria basi vifanyiwe utaratibu na vyenyewe viondolewe Kodi ya Ongezeko la Thamani ili waweze kuvizalisha kwa wingi viwanda vyao vikue na viweze kuwa endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nafikiri kwa ufupi ningependa kugusia hayo matano, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.