Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tu ninaunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana viongozi wangu Mheshimiwa Mbowe pamoja na viongozi wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa jinsi ambavyo wameendelea kutuongoza vizuri kuhakikisha kwamba tunaishauri Serikali na tunaisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kuanza kusikitika sana kwa sababu ya tukio la Mkuu wa Wilaya ya Hai kuongoza Mgambo katika Wilaya ya Hai na kwenda kuharibu Mashamba makubwa ambayo yana zaidi ya bilioni kwenye green house ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Tuna uhakika kabisa kwamba haya ni masuala ya kisiasa ambayo yamefanyika; na kwa sababu Mheshimiwa Mbowe alikuwa ameamua kuwekeza kwenye kilimo kama mwekezaji mwingine katika nchi hii lakini tumeona hakuna taarifa yeyote wala kemeo lolote la Serikali kwa Mkuu wa Wilaya ambaye amekwenda kuharibu mashamba haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linasikitisha sana, na leo katika Bunge hili tunazungumza kwamba tunataka utengamano wa kisiasa. Utengamano wa kisiasa hauwezi kuja kwa sababu kuna uonevu, kuna husda ambazo zinaendelea ndani ya nchi hii. Tumesikia baadhi ya viongozi wetu wanaendelea kuwekwa ndani. Jambo hili linaendelea kututengenisha na hatutaweza kuwa pamoja kwa sababu viongozi walioko madarakani wameshindwa kutuweka pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nijaribu kuzungumzia jambo lingine. Ninataka kuzungumza kwamba bajeti hii ya Mheshimiwa Mpango na niseme kwamba Mheshimiwa Mpango ndiye tatizo katika Taifa hili. Mheshimiwa Mpango kama Waziri wa Fedha ndiye anayelirudisha Taifa hili nyuma. Mimi nimeshangaa sana wakati anasoma bajeti yake hapa watu wamempigia makofi na anasoma kwa mbwembwe kali, lakini ukiangalia utekelezaji wa bajeti yake ya mwaka 2016/2017 unaona ametekeleza kwa asilimia 38. Kama nchi hii kungekuwa kuna uwajibikaji, Mheshimiwa Mpango angeshakuwa a meshaachia madaraka kwa muda mrefu asingeonekana katika Bunge hili la bajeti ambalo linaendelea. Hata Mawaziri wengine walioweza kuwasilisha bajeti zao wasingeweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia Serikali hii inasema kwamba inataka kupunguza umaskini wa Watanzania. Umaskini wa Watanzania hauwezi kupungua kwa sababu ya kununua Bombadier, umaskini wa Watanzania utapungua kwa sababu ya kuwahudumia Watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kutoa mfano; asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima katika nchi hii na asilimia 80 ni masikini; na kati ya asilimia 80 maskini hawa wanapatikana katika asilimia 75 ya Watanzania ambao ni wakulima, wavuvi na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika bajeti ya mwaka 2016/2017 katika Serikali ya Chama cha Mapinduzi tuliwaambia bajeti hii hamtaiweza kuitekeleza mkasema mtaitekeleza, hebu angalia, kwenye kilimo tulikuwa tumetenga shilingi bilioni 101 lakini utekelezaji na fedha zilizokwenda kuinua kilimo ili kuhakikisha kwamba viwanda vinakua katika nchi hii na umasikini unaondoka kwa Watanzania asilimia 75 imepelekwa shilingi bilioni tatu tu kati ya shilingi bilioni 101. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliamua kwamba tuendeleze pia kilimo cha umwagiliaji. Huwezi kuamini katika kilimo cha umwagiliaji tulikuwa tumetenga shilingi bilioni 35 kati ya shilingi bilioni 35 fedha iliyokwenda kwenye shughuli za maendeleo ni shilingi bilioni 1.2 ambayo ni sawa ya asilimia nane ya fedha ambazo zilikuwa zimetengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaendelea kuonesha ni jinsi gani ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijajiandaa katika kuondoa umaskini wa Watanzania. Na ninataka kusema Watanzania hawataweza kuondolewa umasikini wao kwa sababu ya Bombadier wala hawataweza kuondolewa umaskini wao kwa sabau ya standard gauge. Ni lazima tuwekeze kwa wafugaji, kwa wakulima na kwa wavuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Bunge hili wanafika mahali wanashangilia wanasema bajeti ya mwaka, bajeti ya msimu, bajeti haijawahi kutokea, wananchi wenu maskini, wakulima wako vijijini hawajapelekewa fedha kule mnasema bajeti ya mwaka ambayo haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe ndugu zangu Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, mwaka 2015/2016 wakati wa uongozi wa Mheshimiwa Kikwete alitenga shilingi bilioni 88 kwa ajili ya wakulima, hizo ni pembejeo peke yake leo mnatenga shilingi bilioni 10 mnasema hii ni bajeti ya mwaka haijawahi kutokea, haya ni mambo ya ajabu sana, mnaongoza watu gani? Sisi tunakaa mjini kwa wafanya biashara, pale Tunduma ni mjini lakini tunaendelea kuwatetea wakulima ili kuhakikisha kwamba maisha ya wakulima yanainuka na yanapanda juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnasema kwamba mnataka kuanzisha viwanda. Kwenye viwanda peke yake ilikuwa imetengwa shilingi bilioni 42 lakini kati ya shilingi bilioni 42 fedha ambayo imekwenda kwenye viwanda ambayo Mwijage ameipokea ni shilingi bilioni 7.6 peke yake. Leo mnasema Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba nchi inakuwa ni ya viwanda, huu ni ubabaishaji na ni utani kwa Watanzania. Nchi hii hamjajipanga kuanzisha viwanda na hamko tayari kuanzisha viwanda. Msifikiri viwanda vinakuja kwa maneno, msifikiri viwanda vinakuja kwa maigizo yanayofanyika ndani ya Bunge hili. Viwanda vitakuja kwa vitendo, kwa kutenga fedha na kuhakikisha kwamba fedha zinakwenda kwenye matumizi na zinakwenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema kwamba ni lazima tubadilishe mtazamio wetu. Tumefika humu ndani kila wakati ndiyoo, ndiyoo, ndiyoo! Hamjasema ni namna gani mtabadilisha maisha ya Watanzania. Tunataka maisha ya Watanzania yaweze kubadilika kwa vitendo, mnafanya usanii ndani ya nchi wakati mmepewa madaraka makubwa ya kuongoza nchi hii. Kwa nini mfanye usanii na maisha ya Watanzania? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyotekelezwa mwaka 2016/2017 mmetekeleza asilimia 38, leo hii mmetenga bajeti shilingi trilioni 31 wakati shilingi trilioni 29 mmeshindwa kutekeleza, haya ni maajabu makubwa ambayo yanaonekana katika nchi hii. Tunataka mabadiliko katika Taifa hili, na mabadiliko haya kama mtaendelea kucheka namna hii Watanzania mliowaona miaka iliyopita ya 2000 si Watanzania wa sasa hivi na ndiyo maana mnaona kura zenu zinazidi kushuka kwa sababu ya kutowatekelezea yale wanayohitaji Watanzania, na lazima mtang’oka tu. Endeeni kupiga ngonjera humu, endeleeni kushangiliana, endeleeni kusema kwamba ndiyo mzee, tutawakuta humu mnaendelea kusua sua, tutawang’oa katika viti vyenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine nililoshangaa, Mheshimiwa Mpango eti kuanzisha vyanzo vipya amekwenda kuwaorodhesha Wamachinga, wauza ndizi, wauza mbogamboga eti wajiorodheshe wakishajiorodhesha, wakitambulika waanze kulipa kodi, hii nchi iko namna gani? Haijaweka mipango thabiti ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo ili wawe na mitaji mikubwa na baadae waje wawe wafanyabiashara wakubwa, lini Mmachinga kalipa kodi? Hii itakuwa ni nchi ya kwanza katika dunia hii Mmachinga kumlipisha kodi, itakuwa ni nchi ya kwanza mtu ambaye anauza mbogamboga na matunda kulipishwa kodi katika nchi hii. Ni lazima tufike mahali tufikirie mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango hata Buhigwe kule wananchi wameshatoa imani kwako kwa sababu inaonesha wale wanaotumia vibatari umewawekea pia ushuru, wanalipa kodi katika Taifa hili leo unataka wananchi wa Buhigwe wakuamini kwanza unaweza kuwa Mbunge wa Buhigwe, haitawezekana kabisa. Wewe ndiwe unayeshindwa kumshauri Mheshimiwa Rais, unalirudisha Taifa nyuma na ni lazima tufike mahali tukwambie, tuiambie Serikali kwamba imeshindwa kutekeleza wajibu wako sawa sawa ili kuhakikisha kwamba…

T A A R I F A....

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa yake kwa sababu najua anajikosha, sasa hivi ana adhabu ya mwaka mmoja ndani ya Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo, anaendelea kuipunguzia punguzia makali, kwa hiyo, siipokei kabisa taarifa yake huyu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza tu kwamba liko suala lingine, kuna suala linalozungumzwa sasa katika Bunge hili. Wakati watu wanaendelea kujadili bajeti limekuja jambo la mchanga wa madini kwenye nchi hii. Ni vizuri Serikali ya Chama cha Mapinduzi pia ikakumbuka jinsi Wabunge wetu walivyopiga kelele ndani ya Bunge hili, wakakumbuka ni jinsi gani Wabunge wetu walivyoshauri Bunge hili kwamba ndugu zangu tunaibiwa, lazima tufike mahali tubadilishe mikataba hii, mikataba ni mibovu, ni mikataba ya kifisadi, wakasema hapana ni lazima mikataba hii ipite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlishangilia kama mlivyokuwa mnashangilia hapa, leo nashangaa mnatuona sisi ni wachawi katika Bunge hili. Sisi si wachawi, wachawi ni ninyi ambao tayari milipitisha mikataba na Watanzania.

Wachawi ni ninyi kwasababu mlipitisha mikataba hii, tena mikataba ya kifisadi ambayo Watanzania wamepoteza fedha nyingi sana, wameingia hasara…

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nataka niseme…

T A A R I F A .....

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona ana matatizo yake binafsi, hiyo lugha, na yeye ndiye Mbumbumbu pale. Mimi niko vizuri na ninajitambua na ndiyo maana niko Bungeni humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema mikataba haipitishwi humu, tuliishauri Serikali ilete mikataba Wabunge wetu waipitie, wajaribu kuishauri Serikali mikataba iko vizuri au haiko vizuri mkasema hapana, leo nyie wenyewe mnasema mikataba italetwa humu, inaletwa kuja kufanya nini? Inakuja kufanya nini? Mnaleta wakati watu wameshakula imebaki mifupa ndiyo mnatuletea mikataba hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka kusema ni kwamba ni lazima tufike mahali tukubaliane, Wabunge wetu walifanya kazi ya ziada kuishauri Serikali, kwamba mikataba hii ni mibovu mkasema mikataba ni mizuri, mkagonga meza, wakasema sheria hizi ni mbovu, mkasema hapana. Zikaletwa hati za dharura hapa mkapitisha sheria tatu hapa kwa haraka haraka, kwa mkupuo siku moja, lakini mnataka kuniambia kwamba eti Chenge ana matatizo, sijui Ngeleja ana matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali tafsiri yake umeshitaki Serikali ya kipindi kilichopita, ndiyo tafsiri yake. Mwanasheria Mkuu wa Serikali hafanyi kazi kwa jina lake kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anafanya kazi kwa mujibu wa maagizo ya Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wake walioko juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kama mtatuambia kwamba hawa watu ambao wanatajwa, Mawaziri, sijui Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakwenda kujibu kwa nini alisaini, mimi nina uhakika kabisa hata Mzee Masaju hapa hawezi kusaini mkataba kama Mheshimiwa Rais hajamwambia asaini mkataba, lakini je, akisaini huo mkataba kesho tuje tumwambie Masaju mkataba huu ulikwenda vibaya kwa hiyo tunakufungulia mashitaka? Hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mwanasheria Mkuu atakuwa amefanya makosa haya ni makosa ya Serikali nzima ya Chama cha Mapinduzi kwa kipindi hicho kwahiyo kama ni kuwajibika Serikali nzima ya Chama cha Mapinduzi ndiyo inatakiwa kuwajibika kwa jambo hili ambalo limejitokeza. Kwa maana hiyo waombeni msamaha, msijibaraguze kwamba mnawa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)