Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na inawezekana nikawa msemaji wa mwisho kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze tu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri na za msingi ambazo anaendelea kuzifanya. Lakini natakata tu niwakumbushe ndugu zangu tulioko humu ndani na ndugu zangu Wabunge wa CCM wala msipate shida msishangae. Ni ajabu sana leo tunazungumza masuala ya bajeti ya kuwasaidia Watanzania watu bado tunawaza uchaguzi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana baada ya uchaguzi 2015 Wananchi waliamua kutenganisha. Kuongoza nchi si sawasawa na kuongoza SACCOS. Wananchi wa Tanzania walipoamau kuichagua CCM waliamini Mheshimiwa Magufuli atakwenda kuongoza Serikali. Serikali tunayoizungumza ni Serikali yenye mifumo inayoweka utaratibu wa kuwasaidia wananchi wanyonge maskini na wahali ya katikati. Sasa leo ndiyo maana yako makundi haya, uwezo wa kuongoza SACCOS na uwezo wa kuendesha nchi ni vitu viwili tofauti. Tunachangia bajeti mwaka 2017/2018 naomba niwakumbushe tunapokwenda kwenye utaratibu wa ukusanyaji wa kodi, ziko kodi ambazo zimeandikwa kwenye schedule ya leseni ziko biashara ambazo hazijatambulika. Biashara hizi zinazifanya Halmashauri zinazokusanya kodi ziwe na tabia tofauti tofauti. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, mnapokwenda kwenye kipengele hiki tuangalie ili kuweka uwiano ambao utakuwa unafanana karibu kwenye Halmashauri zote nchini. Lakini nikumbushe hapa, nimshukuru tena Waziri pamoja na Mheshimiwa Rais na sisi Wabunge sote wa CCM ambao tulikaa hapa kupanga kuhakikisha wafanyabiashara ndogo ndogo wanatambuliwa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo rafiki yangu Comrade Mwakajoka amenishangaza sana, anataka kuwatisha umma wa wafanyabiashara ndogo ndogo nchi kwamba wataanza kulipa kodi, kodi ambayo ukikisoma kitabu hiki hakuna popote ilipoandikwa Mmachinga, mama lishe, mama ntilie, anayeuza mitumba, anayeuza hiki kwamba anakwenda kutambulika na kulipa kodi. Wakati tunasimama hapa tunawapigania wanyonge hawa na mimi najua ndugu yangu Mwakajoka hili kwenu ni pengo upande mwingine hili ni pengo, kwa sababu hawa wafanyabiashara ndogo ndogo ndiyo walikuwa wanatumika isivyo kuhakikisha wanakuwa mbele kusaidia watu kupita mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezunguka nchi nzima ameona machinga wanavyopata taabu, kaona mama lishe wanavyopata taabu, leo amewatambua na wao watambulike na wao wawe rasmi waache kufukuzwa na mabomu, waache kupigwa, waache kunyanyasika leo tunasema wanatengenezewa kodi ili waanze kuogopa mapema. Ni lazima tuwe na shukrani kwenye mambo yasiyokuwa yanafaa, na mimi nilitegea sana kaka yangu Sugu hata Waitara wangekuwa wakwanza kupongeza kwenye utambuzi wa wafanyabiashara ndogo ndogo maana wao ndio wanaathirika pale sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda ni mfupi lakini nizungumze suala la kodi ya majengo. Wakati Serikali ilipoingilia suala la kukusanya kodi za majengo mwaka wa jana; zilipoondolewa kwenye Halmashauri haraka haraka wote tulifikiria kwamba Serikali imekosea. Nataka niwaambie, Mheshimiwa Rais alitazama mbali na akafikiria jambo la mfano mzuri sana.
Leo tunawaza habari ya vyanzo vipya vya mapato, ninyi nyote ni mashahidi nyumba ambazo zilikuwa hajafanyiwa evaluation zilikuwa hazilipi kodi ya pango zilikuwa hazilipi kodi hii muda mrefu. Leo pigia hesabu nyumba ngapi ambazo hazijafanyiwa evaluation katika nchi hii zitalipa kodi? Na leo zinakwenda kulipa kodi ambayo itakuwa inakwenda kusaidia kwenye nyanja mbalimbali tunazosema kuongeza dawa, barabara lakini kuimarisha vituo vyetu vya afya na kadha wa kadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana ilikuwa ni lazima hii kupigiwa kelele, Halmashauri zimetumia vibaya sana fedha hizi na mfano mzuri ni Arusha. Arusha imekuwa Jiji ililokuwa na tofauti Diwani akienda kwenye kikao kimoja analipwa zaidi ya shilingi 800,000; lakini ukienda Mwanza na maeneo mengine anambuliwa shilingi 200,000 iliyoko kwenye utaratibu. Ni lazima tusimame kuikusanya fedha ya Serikali ikawasaidie wananchi walio wanyonge. Kwa nini tusiipongeze Serikali? Sote tunafahamu na mimi niwakumbushe huwezi kuwa ndani ya nyumba hii kikiamuliwa kitu wewe ukasimama pembeni, wewe ni sehemu ya maamuzi yote yanayofanyika kwenye nyumba hii na Watanzania wanalijua hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukubali. Tunafahamu, kodi ya mabango pia imekwenda Serikalini na mimi niwashukuru Mheshimiwa Mpango naamini mmetengeneza utaratibu sahihi ambao fedha hii mtakapoikusanya kwa pamoja itakuwa inarudi kwenye Kata kwa wakati, kwenye Halmashauri zetu, kwenye Miji, Majiji na Manispaa ili iweze kufanya kazi yake sawa sawa. Tunafahamu jukumu la kupeleka asilimia tano kwa wanawake na vijana ni la Serikali ambao iko chini ya Chama cha Mapinduzi na hii iko kwenye Ilani tutatekeleza. Limejadiliwa suala la milioni hamsini hapa; wenye Ilani Chama cha Mapinduzi milioni 50 tumeahidi ndani ya miaka tano kwa nini mnataka tupeleke leo? Mimi ninayoimani kwamba fedha hizi zitakwenda, na zinatengenezewa utaratibu ili tuweze kufikia malengo tuliyokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, suala la kuongoza nchi lina tofauti kubwa sana na kuongoza kitu kingine cha kawaida ili kufikia malengo ya Watanzania. Mungu awabariki sana, ahsanteni kwa kunisikiliza. Naunga mkono hoja asilimia 100.