Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia uchumi wa Taifa hili. Tunampongeza Mheshimiwa Rais na tunasema Watanzania wengi tupo nyuma yake, aendelee na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii wakiwemo pamoja na wataalam waliosaidia kwa njia moja au nyingine hadi kukamilika kwa bajeti hii ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti pia niwapongeze wananchi wa Tanzania waliopongeza au wanaoendelea kupongeza bajeti hii ya Serikali, bajeti hii ni nzuri na ina matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nithubutu kusema kwamba wananchi wa Tanzania wengi ni wa kulima na wameipongeza bajeti hii kwa sababu imeweza kuwafutia kodi mbalimbali katika ushuru mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji wamefutiwa kodi za mazao, wamefutiwa kodi kwenye chakula cha mifugo, wamefutiwa kodi katika vifaranga lakini pia nithubutu kusema kwamba wananchi hawa wameendelea kupongeza Serikali hasa pale mkakati wa Serikali wa usambazaji wa mradi wa umeme vijijini.

Lakini pia wananchi hawa, wamekuwa wakipongeza Serikali kwa kufutiwa gharama za service charge katika gharama za umeme, kwahiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa jitihada zake za kuleta au kwa kuwarahisishia wananchi uchumi ulio nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali kwa vile wananchi wengi ni wa kulima katika Taifa hili, na Serikali kupitia sekta yake ya kilimo au kupitia sekta ya kilimo imekuwa ikiandaa mikakati mbalimbali ya kukuza kilimo lakini pia imekuwa tofauti katika kufikiwa malengo ya kilimo kutokana na uchache wa fedha.

Kwa hiyo, basi niiombe sana Serikali kupitia sekta ya kilimo kuingiza fedha haraka au Hazina wapeleke fedha haraka ili sekta yetu ya kilimo iweze kukua na ile mikakati iliyopangwa ya kukuza kilimo iweze kufikiwa na tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende katika Benki ya Wanawake. Katika vitabu vya Serikali vile vya mpango pamoja na vya bajeti vimekuwa vikieleza kwamba sasa hivi Benki hii imekuwa ikiendelea katika maeneo mengi katika Tanzania Bara, na imeshafungua vituo na imeshaanzisha vituo karibuni 252 katika maeneo ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nithubutu kusema kwamba benki hii uanzishwaji wake tulishiriki wananchi mbalimbali na wafanyabiashara mbalimbali waliopo Tanzania Bara na Zanzibar. Lakini pia kuna hisa walizonunua au walizowekeza katika Benki hii, hadi leo benki imekuwa ikiendelea kufungua vituo au matawi katika maeneo ya Tanzania Bara lakini Zanzibar wamekuwa wakichelewa kuhusiana na suala la ufunguaji wa vituo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kuendelea pamoja na kuwa inaendelea Tanzania Bara lakini pia iendelee kufungua vituo Tanzania Zanzibar kwa sababu Zanzibar kuna wananchi wajasiriamali, Zanzibar kuna wakulima, Zanzibar kuna wafugaji na wao wanahitaji mikopo kupitia benki hii na benki hii haianishi wanawake tu inakwenda moja kwa moja kwa wananchi wote katika jamii. Kwahiyo, niiombe sana Serikali kujielekeza kule Zanzibar kufungua vituo Unguja na Pemba ili nao waweze kufaidika na hisa walizoziweka viongozi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nilitaka nizungumzie kuhusu shilingi 40 zilizowekwa katika lita ya mafuta, wananchi hawajaona tatizo kuwekwa shilingi 40 kila lita moja ya mafuta kwa sababu kodi mbalimbali walizokuwa wanalipa ilikuwa ni zaidi ya shilingi 40. Kwa hiyo wamefurahi na hawana tatizo ya lita ya mafuta kuongezeka shilingi 40, shilingi 50 haitumiki hata ukienda dukani basi huwezi kutumia shilingi 50 wala hawaoni tatizo shilingi 40 kwa kila lita ya mafuta kuongezwa katika suala la ulipaji wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe sana Serikali pamoja na kuwa imewajali wakulima, lakini pia iwajali na wafanyabiashara, kuna wafanyabiashara wakubwa, kuna wafanyabiasha wadogo. Pia wafanyabiashara hawa wamekuwa na utitiri wa kodi, utitiri wa kodi kwanza kulipia mzigo bandarini, wanaposafirisha mizigo yao kupeleka dukani, wanapofikanao mzigo huu dukani na kila wanapouza bidhaa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na kuwa Serikali au Mheshimiwa Rais amefikiria suala la wakulima lakini pia lifikirie na wafanyabiasha kwa sababu wafanyabiashara wengi kodi zimekuwa kubwa, imekuwa wamefunga biashara zao na walikuwa wanaajiri watumishi mbalimbali, kundi kubwa la vijana sasa hivi halina kazi wafanyabiashara wamekuwa wakifanya kazi wenyewe na kuwaacha wafanayakazi wao. Kwa hiyo, wengi wa vijana hawa baada ya kukosa kazi wameingia katika masuala ya ubakaji na hujuma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, niiombe sana Serikali pamoja na kuwa katika bajeti hii tumewafikiria sana wakulima lakini tuwafikirie na wafanyabiashara kwa sababu ndio wanaongeza uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusiana na suala la mapato ya fedha yanayotokana na watumishi wa Jamhuri ya Muungano walioko Zanzibar. Mpaka leo hii na suala hili limekuwa muda mrefu sasa, kusanyo la shilingi bilioni 1.75 hili ni suala la muda mrefu, kwa hiyo, mishahara hii imekuwa ikikuwa siku hadi siku wamekuwa watumishi hawa wakiongezewa mishahara, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kufanya tena mchakato au tathimini ya wafanyakazi walioko Zanzibar kutoka kipindi cha nyuma hadi sasa hivi wameongezeka kwa kiasi gani, lakini pia mapato yanayotakiwa kuingia sasa hivi Zanzibar kuhusiana na watumishi hawa income tax ni kiasi gani tusiendelee tu na asilimia 1.7 kama tunavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nipewe elimu kuhusiana na suala la asilimia 4.5 inayoendelea kwa sababu asilimia hii 4.5 ni ya muda mrefu kwa upande wa Zanzibar wananchi wamekuwa wakituuliza maswali mengi, kwa hiyo niiombe sana Serikali kutoa elimu zaidi kwa sababu uchumi toka tulipo ingia katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwa Tanzania ni muda mrefu, uchumi wetu umekuwa ukikua siku hadi siku, tofauti na uchumi ulivyokuwa nyuma, kwa hiyo, asilimia 4.5 naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atupe elimu kuhusiana na asilimia 4.5 ili wananchi wa Zanzibar waweze kuridhika na wasiwe na maswali kuhusiana na maswali kuhusiana na kero za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.