Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuzungumza. La pili naomba niseme bajeti ni nzuri, naiunga mkono, nishauri tu kama ambavyo Wabunge wengi wamesema kwamba eneo la maji au fedha tulizotenga kwa ajili ya maji bado tatizo ni kubwa ni vizuri eneo hili likatizamwa angalau fedha zikaongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala hilo la bajeti, naomba nizungumzie suala la mapato ya Serikali. Kama tunavyojua bajeti unahusu mapato na matumizi na unapozungumzia mapato ya Serikali na hasa kwa Mbunge unayetoka Bulyanhulu huwezi ukaacha kuzungumzia suala la makinikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa hatua ambazo amezichukua kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi tumezungumza. Naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba kuna Mbunge mmoja amezungumza hapa kwamba kuna Tume nyingi zimewahi kuundwa na akasema tume hii ya Profesa Osoro na Profesa Mruma ni idadi tu ya nyongeza ya Tume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimfahamishe Mbunge huyo aliyesema hivyo kwamba pengine hajachukua muda wa kufuatilia naomba nifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba tume ya Bomani ambayo mimi nilikuwa mmoja wapo pamoja na wenzangu kina Dkt. Mwakyembe kazi yetu sisi tuliambiwa tufuatilie/tufanye mapitio ya sera na sheria kuangalia na nchi zingine wanafanyaje ili tutoe mapendekezo kwa Serikali kwa ajili ya kurekebisha maeneo ambayo hatufanyi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya kazi kwetu hatukua tunafanya uchunguzi (investigation) ndiyo maana tume yetu tulikuwa tunafanya kazi kwa kufanya mikutano ya hadhara tunatangaza tupo wapi wananchi wanakuja wanaeleza na hayo tuliyajumuisha kwamba wananchi wa maeneo wanayozunguka migodi wana mawazo haya. Kwenye eneo la usafishaji kwa mfano wa makinikia observation ya Kamati ilikuwa ni kama ifuatavyo naomba nikusomee tulisema hivi; “kukosekana kwa mkatakati wa kisera wa uanziswaji wa viwanda vya uchenjuaji na usafishaji wa madini hapa nchini kumesababisha madini na mchanga wa dhahabu kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya usafishaji na uchenjuaji, hali hii imesababisha Serikali kushindwa kudhibiti aina na kiasi cha madini kinachozalishwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia observation hii ya Kamati inaonesha kwamba kuna “smoking gun” inaonyesha kwamba kuna tatizo kwenye hili, ndio maana sasa Mheshimiwa Rais Magufuli sasa akaunda Tume ya kuchunguza kwa hiyo, tofauti ya hizi tume za mwanzo za ushauri na mapitio ya sera, Tume ya Profesa Mruma na Tume ya Profesa Osoro zilikuwa zinachunguza jambo hili mahususi kwamba kuna nini na kitu gani ambacho kinafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jipya amblo halijafanyika, kwa hiyo, Tume ya Osoro na Tume ya Mruma ni tofauti na Tume ya Bomani na kwa mara ya kwanza sasa tunapata tume mahsusi kwa ajili ya kuchunguza, na baada ya hatua hiyo matokeo ya uchunguzi yalipopatikana hatua zimechukuliwa very aggressively, very bold, very fame, very patriotic. Ni kwa approach hii niliwahi kusema hata kwenye kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwamba kampuni kama ya Acacia ndipo inapoweza kuja kwenye mazungumzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwa wawekezaji hawa ni arrogant, ni fedhuli katika hali ya kawaida si rahisi wakaja kwenye meza ya mazungumzo bila kuwabana na bila kuwa na data za kutosha za kiuchunguzi, ndio maana leo unawaona wanakuja kwa sababu uchunguzi umefanyika na imedhihirisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, na wananchi wa Kakola, wananchi wa Bulyanhulu wanampongeza sana na tayari wameshamuomba Mkuu wa Wilaya awaruhusu wafanye maandamano kama itawezekana kwa ajili ya kupaza sauti zao maana wamepoteza ardhi, wamepoteza wenzao na mambo mengine lakini amepatikana mkombozi ambaye hatua anazochukua zinagusa kabisa mioyo yao na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hilo naomba nizungumze local issues na hili nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini na Mheshimiwa Profesa Kabudi ambaye wanazungumza au wanasimamia suala hili wananchi wa kule ambako makinikia yanatoka wanaona kabisa kwamba na wanaomba issue zao zizingaiwe, zitizamwe na ziwepo katika majadiliano yatakayo fanyika baina ya Serikali na mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo tunaomba litizamwe pamoja na kuibiwa huku kwenye Serikali Kuu na Halmashauri tumeibiwa, kwa takwimu za Profesa Osoro Halmashauri ya Wilaya ya Kahama na Wilaya Msalala tunadai kati ya shilingi bilioni 795 hadi shilingi trilioni mbili bilioni 283 za service levy kwa takwimu za Profesa Osoro kwa uzalishaji wa Bulyanhulu na Buzwagi kati ya mwaka 1998 hadi 2017. Tunaomba jambo hili halmashauri fedha hizi ziwemo katika majadiliano na Halmashauri tuzipate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili uchunguzi ufanyike kuangalia makampuni mengine ambayo ni related companies ambazo zinafanya biashara kwa sababu zimekuwepo na hii tunaita transfer price bills, makampuni yanayotoa huduma kule hayalipi service levy, kwa hiyo, tunataka kujua yamefanya biashara kiasi gani ili Halmashauri tuweze kutoza service levy. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tunaomba sana katika mikataba na practice za kimataifa, mwekezaji anatakiwa kutumia angalau asilimia moja ya mapato yake kwa ajili ya huduma za kijamii. Kwa kutumia takwimu za Profesa Osoro toka mwaka 1998 hadi 2017, Kahama tunapaswa tuwe tumewekezewa au tumesaidiwa kwenye miradi ya kijamii asilimia moja ya uzalishaji wa Acacia ambayo ni sawa na shilingi trilioni 1.320. Kwa hiyo tunaidai cooperate social responsibility tufanye reconciliation kile walichofanya na trilioni 1.320 ili tuweze kulipwa kinachohitajika kingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaomba lifanyiwe uchunguzi ni kwa kuna madai ya wafanyakazi wanaugua, wako wafanyakazi wengi nilikuwa nikiongea sana na Waziri wa Kazi wafanyakazi wanaopata madhara ya kiafya, kwa hiyo, ufanyike uchunguzi kuhusu afya za wafanyakazi na waliokuwa wafanyakazi na wengine ambao wamekwisha kuathirika walipwe fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna wananchi 4,600 waliondolewa kwenye lile eneo hawakulipwa fidia yoyote, kwa hiyo, katika majadiliano suala la compensation nalo lizingatiwe na likumbukwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapendekeza kwa kuwa haya yameonekana kwenye makinikia peke yake tunaamini hata kwenye vitofari vya dhahabu nako kuna matatizo. Kwa hiyo, uchunguzi uongezeke tuangalie kwenye vitofali na kwenye migodi mingine, haiwezekani TMAA wakawa wachawi kwenye Bulyanhulu halafu wakifika Geita Gold Mine wakawa watakatifu, practically na kule kuna matatizo uchunguzi ufanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho wote tunajua kwamba mwekezaji huyu amekubali kujenga smelter na tunajua makinikia yanatoka Bulyanhulu na smelter itajengwa Tanzania, niombe Wizara na waratibu wa suala hili basi wafahamu kwamba economically na mazingira yote smelter tunaomba ijengwe pale ambapo makinikia yapo, tunaomba smelter ijengwe Bulyanhulu, naomba mtufahamishe mtuambie inatakiwa ardhi kiasi gani na maandalizi ya namna hiyo yaanze tutenge ardhi, muweze kujenga smelter. Sitaratjii kusikia kwamba smelter inajengwa sehemu nyingine yoyote tofauti na Kahama kwa sababu za mazingira hayo ambayo tunayajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba niseme napongeza sana bajeti hii namuunga mkono sana Mheshimiwa Waziri na bajeti yake lakini kubwa zaidi wananchi wa Bulankulu, wananchi wa Msalala wanampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua anazochukua tunaomba haya maeneo ya uchunguzi yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi yafanyiwe uchunguzi, madai ya wananchi mbalimbali ambayo wananathirika na jambo hili yajumuishwe katika majadiliano baina ya Serikali na mwekezaji ili wakati Serikali inalipwa zile trilioni 108 na sisi Kahama tunalipwa bilioni 795 service levy tunalipwa vile vile trilioni 1.320 kwa ajili ya cooperate social responsibility.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja.