Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na pia namshukuru Mungu kwamba amenipa fursa na ametupa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa na mimi napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na timu yake kwa kazi nzuri, nasema ni kazi nzuri kwa vigezo vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ukisikiliza hotuba yake hata ukisoma kwa kiwango kikubwa utakuta mambo mengi ambayo ameyasema mule ni mambo ambayo sisi wenyewe Wabunge tulishauri hapa. Tuliyapigia kelele sana mwaka jana, tukayapigia kelele sana humo katikati na nataka kusema mimi ni mmoja ya watu ambao amethibitisha kwamba nilikuwa nakosea, Waingereza wanasema ameni- prove wrong. Mwaka jana nilitoka hapa na fikra kwamba Mheshimiwa Mpango hasikilizi, lakini mwaka huu ameni- prove wrong anasikiliza, kwa hiyo, hicho kigezo cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo cha pili, kwa sababu amesikiliza, utagundua kwamba mengi aliyoyasema kwa kweli hata wasikilizaji, wananchi wetu huko vijijini kabla hata hawajaona habari ya utekelezaji itakuwa vipi kwa sababu hiyo ni hatua nyingine lakini angalau kwa hatua ya kwanza wanaona bajeti hii ni ya kwetu. Akishindwa kutekeleza hiyo ni habari nyingine sisi tutamwambia kama Wabunge lakini kwa hatua ya kwanza wanaona kabisa hii bajeti ni ya kwetu sisi ndiyo walengwa. Kwa hiyo, nampongeza na timu yake kwa mambo hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wanasema kufanya vizuri haitoshi tunatakiwa kufanya vizuri zaidi. Yapo mambo ambayo bado sikubaliani na Mheshimiwa Mpango. Maisha ya binadamu ukijaribu kuweka vipaumbele ni jambo gani la kwanza ambalo hilo lisipokuwepo uhai wake hautakuwepo, la kwanza ni hewa ya kupumua ambayo kwa bahati nzuri ama mbaya hiyo haipo kwenye bajeti.

Pili, ni chakula na la tatu ni maji yaani ni afadhali Watanzania wote tutembee uchi hapa lakini tuna maji na tuna chakula. Hivyo ndiyo vipaumbele kwamba hewa ndiyo ya kwanza, huwezi kuongelea nguo wala viwanda kama hakuna hewa, imechafuliwa, ina gesi yenye sumu haiwezekani…

TAARIFA ....

MHE. OSCAR R. MUKASA: Haya, tuendelee Mheshimiwa Mpango na mambo ya msingi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, kwanza kabisa ni hewa ambayo haipo kwenye bajeti. Pili, chakula na tatu ni maji halafu mengine yote pamoja na umuhimu wake yanafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama ukurasa wa 8 mpaka wa 9 wa Kitabu cha Hali ya Uchumi, anasema hivi Mheshimiwa Mpango kwamba Pato la Taifa lilitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 lakini limekua kwa asilimia saba badala ya
7.2 na akafafanua kwamba ziko sekta ambazo ndiyo zimechangia tusifikie lengo hilo na sekta mojawapo ni kilimo ambayo ilitarajiwa kuchangia kwa asilimia 2.9 lakini ikachangia kwa asilimia 2.1, amesema vizuri pale. Ukiangalia vipaumbele vya bajeti sasa kilimo kimeguswa kwenye shamba moja la miwa. Sasa mimi nikakaa najiuliza pamoja na kwamba sipingani na shamba la miwa kwa sababu nadhani anakwenda kujibu ile habari ya ukurasa fulani hapo hapo anasema, moja ya mazao ambayo tulilazimika kuleta kwa wingi kutoka nje ya nchi mwaka jana ni sukari, nafikiri anakwenda kujibu hilo, lakini nilitarajia kilimo kwa ujumla wake kipate kipaumbele. Hata kama huwezi kuwa na majibu ya matatizo yote lakini lazima kwenye vipaumbele vya Kitaifa vilivyo kwa ngazi ya bajeti tofauti na ngazi ya Wizara moja moja lazima kilimo kitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukurasa wa 11 wa hali ya uchumi pia anasema; mfumuko wa bei wa mwezi wa Aprili, 2017 ulikwenda juu ya wastani ya mwaka wa mfumuko wa bei, ukaenda 6.4 badala ya 5.2 ambayo ni wastani kwa sababu kulikuwa na hofu ya upungufu wa chakula kwa sababu watu waliona msimu wa mvua unachelewa. Hii yote inakuonyesha namna gani tunahitaji kujikita siyo tu kwenye kilimo tunapaswa kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kama unavyofahamu hatujawahi kutumia potential yetu ya kilimo, uwezo wetu wa kilimo cha umwagiliaji kwa kiwango kinachostahili. Kwa hiyo, nilitarajia kwenye vipaumbele vya ngazi ya Kitaifa, vya ngazi ya bajeti kuu siyo ngazi ya sekta moja moja habari ya angalau kilimo cha umwagiliaji kionekane ni kipaumbele. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango nimeshangaa sana kutoona kipaumbele cha kilimo zaidi ya shamba moja la miwa kwenye bajeti kuu, naomba ufanye mapitio kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya maji sasa ambayo imepelekea mtu akatoa taarifa hapa, sina matatizo na taarifa hiyo lakini mimi nilikuwa najikita kwenye mantiki kama mantiki umeiona nakushukuru, kama huioni bahati mbaya nitakuelekeza baadaye. Biharamulo leo tunavyozungumza, katika vijiji 80 vya Wilaya ya Biharamulo huwezi kuhesabu vijiji zaidi ya 15 au 16 ambavyo ukienda kuongea ajenda

nyingine tofauti na maji watakusikiliza. Leo Mji Mdogo wa Kabindi pale mpaka watu jana nilikuwa nazungumza nao wanapanga kufanya maandamano wanasema kwamba sasa hali ni mbaya. Tunaomba Mheshimiwa Mpango hebu weka hii habari ya maji, Wabunge wamesema mengi sitaki kurudia, habari ya maji hebu tuifikirie Kitaifa na kimkakati. Hii habari ya kuiacha kwamba ni suala la kudonoadonoa kila Mbunge anakwenda anakimbizana na Waziri wa Maji anampa msaada kimradi kimoja, kisima kimoja na vitu kama hivyo haitatufikisha. Kwa taarifa za kitafiti zilizopo habari ya kutafuta maji inachukua zaidi ya asilimia 40 ya muda wa Watanzania wa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali kwa sababu wanahangaika kwenda kutafuta maji ya kutumia nyumbani kwao na kwa ajili ya maisha ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo kwenye hotuba yake ukurasa wa 31 na yeye aliorodhesha pale vipaumbele akavitaja, cha kwanza anasema, kuboresha mfumo wa utafiti wa utoaji wa matokeo ya utafiti kwa wadau, kuimarisha usimamizi kabla na baada ya mavuno, kuimarisha upatikanaji na utumiaji wa pembejeo, zana za kilimo na vitu kama hivyo, kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo, kuratibu na kuboresha matumizi endelevu ya ardhi, kuunda na kupitia sera, kuwezesha uwezeshaji wa sekta binafsi na kuimarisha uratibu, ufuatiliaji na tathmini. Nililazimika kwenda huku maana yake nilidhani inawezekana kwenye bajeti kuu tumesahau hii habari ya umwagiliaji kwa sababu ndiyo itatutoa, tunazungumzia hapa habari ya ukame mpaka mfumuko wa bei unapanda nikasema ngoja nirudi kwa Waziri wa Kilimo inawezekana yeye anaongelea umwagiliaji lakini na yeye hasemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna tatizo na tumuombe Waziri wa Fedha, uzito wa suala la kilimo kwa upana wake uliotolewa hapa hautoshi. Kwa hiyo narudia, moja, suala la muhimu kabisa kwa binadamu ni pumzi ambayo wewe huna mamlaka nayo kwenye bajeti isipokuwa kama itatokea uchafuzi wa hali ya hewa inawezekana ikakuhusu.

Pili, ni chakula tunaomba utoe uzito unaostahili kwenye chakula na tatu ni maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unasimama hapa kutujibu tunaomba utuambie mustakabali wa kilimo kwa upana wake na tusisahau hii ndiyo sekta ambayo inaajiri Watanzania angalau asilimia 65. Ninyi Kitaifa mnaongelea asilimia lakini Biharamulo unaongelea asilimia 90 mpaka 92 wote wanajihusisha na kilimo. Kwa hiyo, tunaomba utakaposimama hapa Mheshimiwa Waziri utuonyeshe ni namna gani unaingiza suala la maji na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye habari ya makinikia maana naona kwa wiki hii usipoongelea makinikia unaweza kuwa upo tofauti kidogo kwa sababu kuna statistical normality na ideal normality kwamba ukienda kule kwa watu wafupi Congo sijui wanaitwa kabila gani, wote ni wafupi wewe ni mrefu. Statistically pale wewe ni abnormal, wao statistically ni normal kwa sababu ndiyo wengi ila ideally wewe uko kawaida wao wako abnormal. Kwa hiyo, lazima niongelee makinikia na mimi nitayaongelea kwa sentensi chache tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vita kuna mambo kadhaa lakini makubwa matatu ambayo mimi nataka kuyasemea. Moja, kuna lengo (goal) yaani mnalenga nini, mbili, kuna mkakati (strategy), mnajipangaje kwa ujumla na kwa upana wake na tatu kuna tactics (mbinu). Sasa kwamba lengo letu ni kushinda hii vita ya kwamba tumenyonywa miaka mingi siamini kama kuna Mtanzania ambaye hana lengo hilo, lakini kwa ngazi ya mkakati hiyo ndiyo ngazi ambayo yuko Rais. Rais anachotaka kufanya, mimi nimemsikiliza, nimemfuatilia unamuona huyu mkakati wake ni kutafuta namna gani siku tukikaa meza moja na hao tushike upande wa mpini na wao washike makali au angalau tuwe na meza moja, ndiyo mkakati alionao ukimsikiliza na ukimfuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiwasikiliza wengine wanaochangia unaona kwamba kila mmoja anataka kuchangia kwa ngazi ya tactics (mbinu) ambalo ni jambo zuri lakini kwa bahati mbaya mtu anataka kuchangia kwa ngazi ya tactics (mbinu) lakini anafikiri ili mbinu yake ionekane imesaidia ni lazima abomoe mkakati, sasa hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana falsafa wanasema, ukiwa na mkakati mzuri bila mbinu utakuwa na mawazo mazuri bila utendaji, lakini ukiwa na mbinu nzuri bila mkakati ni vurugu. Ndiyo maana hapa unaona mwingine anasema haya tunajenga nyumba, wewe bomoa tofali hili badala ya wote kusema jenga. Kwa hiyo, tutambue kwamba lengo letu ni moja, Rais yuko kwenye ngazi ya mkakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko kwenye ngazi ya mbinu, kwa hiyo, kila mtu atoe mchango wake wa mbinu ambayo hailengi kubomoa mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.