Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya mimi kuungana na Wabunge wenzangu katika kuchangia bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau, naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya. Sote tunafahamu kwamba Rais wetu Magufuli ni binadamu kama binadamu wengine. Kila binadamu anapofanya jambo jema anapenda kupongezwa na kwa kufanya hivyo tunampa nguvu katika kutekeleza majukumu yake. Naomba niungane na Wabunge wenzangu lakini niungane na wananchi wote kwa ujumla, kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na niseme binafsi naendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili afanye kazi yenye kuleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Halmashauri. Kwa bahati nzuri mimi ni Mjumbe wa ALAT- Taifa. Kama tunavyofahamu kwamba Mkutano wa ALAT-Taifa unaunganisha Wenyeviti wa Halmashauri, Mameya, Wakurugenzi lakini wamo na Wabunge kutoka katika kila Mkoa. Mimi ni Mbunge ambaye nawakilisha ALAT-Taifa kutoka kwenye Mkoa wangu wa Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu kupitia kikao ambacho kilifanyika tarehe 22 - 24 Septemba, 2016 mkutano ambao ulifanyika Mkoa wa Mara, kupitia Halmashauri zetu mambo mengi sana waliyazungumza. Miongoni mwa mambo ambayo yalizungumzwa ni pamoja na Halmashauri nyingi kukosa watendaji walioajiriwa wa kada mbalimbali. Jambo hili limezungumzwa sana na Wabunge wenzangu na mimi nimeona ni bora nisisitize kwamba wakati sasa umefika kuhakikisha tunaajiri watendaji katika kada mbalimbali ikiwemo Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata na wale wakuu wa idara ambao wanafanya kazi moja kwa moja katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilizungumzwa ni kuchelewa kupelekwa kwa peza zile za vyanzo vilivyofutwa. Tatizo hili limekuwa sugu, nimeona ni bora nisisitize jambo hili kwamba wakati sasa umefika wa kuhakikisha vyanzo vile ambavyo tulivifuta tunapeleka pesa kwa wakati. Kwa kufanya hivyo, tutazisaidia Halmashauri zetu kutekeleza majukumu ambayo yamepitishwa kupitia bajeti za ngazi ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuchelewa kupelekwa kwa OC. Hili jambo naomba nilizungumze na naomba nitolee mfano kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, toka mwaka jana mwezi Julai OC katika idara zile mbalimbali hazijaenda. Naomba kuisisitiza Serikali tupeleke OC katika zile idara kwa kufanya hivyo tutazisaidia idara zetu kutekeleza majukumu yake kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba niliseme tena kabla sijasahau na kwa umuhimu wake, naomba nizungumzie barabara kwa kiwango cha lami inayotoka Mbinga-Mbamba Bay. Napozungumzia Mbamba Bay maana yake naigusa Wilaya ya Nyasa. Sote tunafahamu kwamba Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa Wilaya zilizoko mpakani. Wilaya hii inapaswa sasa kuona umuhimu wa kutengenezewa barabara kwa kiwango cha lami. Tunafahamu matatizo ambayo yanaweza yakajitokeza kwenye barabara za mipakani.
Kwa hiyo, ni vizuri kuhakikisha tunatengeneza barabara hiyo kutoka Mbinga mpaka Nyasa kwa kiwango cha lami. Nimeona niliseme hili nikiwa nafahamu kwamba mara nyingi hata watumishi wanaopelekwa kwenye barabara hizi za mpakani wamekuwa na wasiwasi na hasa wakiangalia masuala ya miundombinu. Naomba nisisitize Serikali yangu katika kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa barabara ya lami kwa kiwango cha lami kutoka Mbinga mpaka Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba nilizungumzie ni suala la shilingi milioni 50. Wenzangu wengi wamelisema na wengine wamekuwa wakifananisha na mamilioni ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Mimi naomba niseme hizi shilingi milioni 50 zilikuwa ahadi kutoka kwa Rais wetu aliahidi baada ya ushindi wa chama chetu na sina shaka kwamba tulishinda kwa kishindo na mimi nachofahamu utamaduni wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni kutekeleza kile tulichoahidi, niombe sana tutekeleze kwa kupeleka hizi shilingi milioni 50. Nafahamu tunapozungumza Serikali za Vijiji ni mamlaka kamili zina Wenyeviti, Halmashauri za Vijiji na zina Wenyeviti wa Vijiji, tupeleke hizi pesa wao sasa wataona ni nini kifanyike kupitia hizi shilingi milioni 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo mimi naomba nilizungumze hapa, ni suala la vifo vya akina mama wajawazito, naguswa sana na jambo hili nikiwa mimi ni sehemu ya wazazi. Tumelisema sana akina mama kupitia kwenye vikao hivi lakini kinachosikitisha zaidi hata ukiangalia kwenye bajeti zetu jambo hili linaonekana halipewi kipaumbele. Mimi nimeona niliseme hili kwa huzuni kubwa sana nikiwa nafahamu kwamba ninapozungumzia suala la vifo vya akina mama wajawazito ziko sababu nyingi zinazosababisha vifo. Sababu mojawapo ambayo mimi nimeiona ni ukosefu wa vifaa tiba. Mpaka hivi tunavyozungumza kwenye zahanati zetu akina mama wanatakiwa waende na mabeseni na vifaa vya kujifungulia. Sisi kama Serikali wakati sasa umefika mama anapokwenda kwenye kituo vile vitu anavikuta hapo hapo kwenye zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni suala la wataalam. Tumezungumza sana suala la kuajiri watumishi wenye ujuzi wa kutosha katika zahanati zetu. Ni jukumu langu kama mama kusisitiza kwamba sasa wakati umefika wa kuona tunakuwa na wataalam wa kutosha kwenye maeneo ambayo wakina mama wanajifungulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni maeneo ya kutolea huduma. Napozungumzia maeneo ya kutolea huduma nagusa zahanati na vituo vya afya. Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakuwa mashahidi tuliahidi kujenga zahanati kila kijiji na kujenga kituo cha afya kila kata. Naomba sana wakati sasa umefika wa kutekeleza na ni vizuri sasa kwa kuwa Serikali hii sikivu basi ni bora na wananchi wetu waone inasikia kwa vitendo, itekeleze vile vitu ambavyo imeahidi na mimi naamini kwa kufanya hivyo itaturahisishia hata katika kipindi kijacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo mimi naomba niliseme na kweli wenzangu wengi wamelisema ni suala la miradi ya maji. Tunayo miradi ya maji ambapo mpaka hivi tunavyozungumza haileti tija kwa wananchi wetu. Kama tunavyofahamu wahanga wakubwa wa jambo hili ni akina mama. Tumtue mama ndoo, tukaribishe huduma hii kwa mama, hivi tunavyoona akina baba wanapendeza, wamevaa suti nzuri ni kazi ya sisi akina mama katika kuhangaika kutafuta maji. Kwa hiyo, mimi kama mama, kama mwanamke ambaye na mimi ni miongoni mwa waathirika wa jambo hilo ninalazimika kusisitiza Serikali kwamba wakati umefika wa kuhakikisha tunatenga bajeti za maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi iko mingi lakini miradi mingine ni viporo na kwa kuweka miradi viporo tunaisababishia ile miradi kuongezeka gharama za uendeshaji. Kwa hiyo, kupitia kikao hiki nisisitize sana, iko miradi mingine mpaka hivi tunavyozungumza ilikabidhiwa kwa wananchi, lakini haitoi maji, wakati sasa umefika kwa Serikali yetu kuona uwezekano kupitia Halmashauri zetu kubaini miradi yote ambayo haijatekelezwa ipasavyo lakini kuitengea pesa miradi mipya ya maji kuhakikisha tunaondokana na hili tatizo la miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake. Katika kipindi ambacho nimekaa hapa Bungeni, miongoni mwa Wizara ambazo zimetulia ni pamoja na Wizara hii. Dalili ya kuonyesha Wizara hii imetulia ni kusikilizana kwa Waziri na Naibu wake lakini kama hiyo haitoshi kusikilizana kwa Waziri, Naibu na watendaji katika Wizara. Mimi naamini kwenye Wizara mkiwa na wimbo mmoja kila kitu kitafanikiwa. Mnafanya vizuri, binafsi nawapongeza sana na naendelea kuwatia nguvu, endeleeni kufanya kazi, endeleeni kuchapa kazi sisi tunawatumaini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana kwa suala la kuondoa ushuru wa mazao ya chakula. Miongoni mwa vitu ambavyo vilikuwa vinawagombanisha viongozi na wakulima ni suala la ushuru ilikuwa shida sana katika Halmashauri yetu. Mimi naona katika vitu ambayo mmeitendea haki Serikali yetu, mmewatendea haki wakulima wetu ni katika kuondoa suala la ushuru kwamba sasa wakulima wameruhusiwa kusafirisha tani moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hili eneo naomba tusije tukasahau, kwamba kupitia hapo hapo Halmashauri zilikuwa zinapata pesa. Nalisema hili kwa sababu nina uzoefu nalo, mimi kama mkulima naweza nikawa na tani zangu kumi, nitakachokifanya ili nisafirishe kwa kutimiza huu wajibu wa tani moja ni kuandika jina la mwanangu, mjomba wangu, shangazi ili kuhakikisha tani kumi zote zinasafirishwa. Kwa kuwa Serikali imeamua kuwarahisishia kusafirisha tani moja ni vizuri tuweke mkakati mzuri na tuziagize Halmashauri zetu ni mbinu gani zitatumika …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.