Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mada iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimwa Rais alipokuwa anapokea ile ripoti ya makinikia ya pili aliomba sisi Watanzania tumuombee, hasa na mimi nikaona nitayarishe vifungu ni nukuu kidogo hapa katika Bunge letu ili wale ambao wanakuwa hawasomi Biblia waweze kusoma na naomba nisome Timotheo wa Pili Mlango wa Kwanza mpaka wa Tatu; “Basi kabla ya mambo yote wataka dua sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya Wafalme na wote wenye mamlaka ili tuishi maisha ya utulivu na amani.”

Lakini ukisoma Waibrania 13 mpaka 17 inasema; “Watiini viongozi wenu na kuwa wanyenyekevu maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu kama watu watakaotoa hesabu ili kwamba wafanye kazi yao kwa furaha na kwa manufaa yenu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magufuli ni zawadi kwa Watanzania ni Mussa wa Watanzania kwa vile Mungu alivyosikia kilio cha watu wa Taifa la Israel kuwakomboa toka utumwani na kuwapeleka Kanani vivyo hiyo Mungu amesikia kilio cha Watanzania wanyonge amemleta Rais Magufuli ili awe mkombozi wa kututoa katika utumwa, umaskini na kutupeleka katika neema kwa kudhibiti wizi wa madini na rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitumie fursa hii sasa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika nchi yetu na niombe Watanzanila bila kujali itikadi zetu tuunge mkono kwa yote anayo yafanya kwa ajili ya Taifa letu. Nawapongeza Watanzania wote waliomuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu na hatua wanazozichukua kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali katika sekta ya madini, nawapongeza Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa azimio lao ambalo walilitoa juzi kuunga mkono juhudi hizi za Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri katika Ofisi yake Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde kwa kuaamua kuupatia heshima Mkoa wetu wa Iringa kuja kuzindua mafunzo ya ufundi kwa vijana wetu katika Chuo cha Don Bosco; mafunzo ambayo yatawanufaisha vijana karibu 3,440 na yataendelea kwa nchi nzima tena bure kabisa. Vijana 1,000 Mwanza, vijana 1,000 Morogoro, vijana 2,000 Dar es Salaam na vijana 4,000 ambao wamekuwa wakifanyakazi bila kupata mafunzo watapata vyeti vyao. Kwa hiyo, ni jambo jema ambalo Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inatakiwa iungwe mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeza sasa katika madaa nimpongeze Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kijaji na watendaji wote wa Wizara kwa hotuba yake ya bajeti nzuri na yenye mashiko, na ambayo imejali watu wote wakulima, wafanyakazi, wote imewajali kwa kweli. Lakini naomba kabla sijaanza kuchangia kabisa na mimi ni nukuu katika hotuba ya msemaji wa Kambi ya Upinzani ukurasa wa tatu maneno ya hayati Nelson Mandela “No easy walk to freedom.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie wenzangu Wapinzani kuwa nchi hii ilikwisha pata uhuru kwa njia ya amani na utulivu. Sasa sijui wenzetu wanapigania uhuru wa nchi gani maana nchi yetu ilikwisha kombolewa kutoka kwa wakoloni kwa jitihada za TANU na sasa hivi ndio CCM na hao hao NAC tuliwasaidia Watanzania kupata uhuru kutoka kwa makaburu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali katika bajeti hii kwa kuwatambua rasmi wafanyabishara wadogo wadogo wasio rasmi na wanafanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kama mama lishe, wauza mitumba wadogo wadogo, wauza mazao ya kilimo kwa kuwapatia vitambulisho maalum kazi wanazozifanya. Lakini nilitaka kujua je kuhusiana na vijana wa bodaboda na wenyewe wako maana yake kwenye kitabu kile hawajasema maanake nao wamekuwa wakitoa kodi naomba na wenyewe labda watakapokuwa wanajibu watuambie kama na bodaboda na wenyewe wapo.

Pia nilikuwa naomba Halmashauri zetu ziandae sasa mazingira rafiki kwa hawa wafanyabiashara waweke miundombinu rafiki, kuwepo na maji, kuwepo na umeme na waangalie sehemu ambazo hawa wanaweza wakafanya biashara zao na wakapata faida. Kwa sababu utakuta Halmashauri zetu zimekuwa zikitenga maeneo ambayo sio rafiki na biashara na kuwasababisha vijana wetu kushindwa kufanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi pia niungane na wote waliochangia kuhusiana na tozo ile ya shilingi 40 katika mafuta mimi nilikuwa naomba kweli ipelekwe moja kwa moja katika mradi wa maji. Kwa sababu maji vijijini ili dhamira ya kumtua ndoo kichwani mwanamke iweze kutimia kwa sababu ukiangalia katika Mkoa wetu utakuta miradi hii ya maji mingi sana imekwama, visima vingi vimechimbwa lakini havitoi maji na vilevile unakuta kuna vyanzo vya maji vingine ambavyo bado sio salama, kwa hiyo, kuna maziwa na mito mingi lakini bado hatujaweza kupatiwa maji vizuri katika Mkoa wa Iringa maji vijijini ni tatizo kubwa sana. kwa hiyo nilikuwa naomba ile tozo iende moja kwa moja kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuchangia kuhusiana na hoja hii nafikili tunaelekea katika uchumi wa viwanda lakini bila kutoa kipaumbele katika barabara zetu za kiuchumi bado tunapatashida sana, kwa sababu ndizo ambazo zenye malighagfi, utakuta katika Mkoa wetu wa Iringa barabara nyingi sana za kiuchumi hazina lami. Kwa hiyo, utaona kwamba zile malighafi wakati wa mvua malori yanakuwa yanakwama ukienda kule Mufindi, Kilolo unakuta kwamba yale malori yanakwama kule kwa hiyo mimi nilikuwa naomba Serikali itoe kipaumbele ihakikishe kwamba barabara zote za kiuchumi zinawekewa lami ili kusaidia hata kukuza uchumi huu wa viwanda kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipochangia mara ya kwanza nilichangia kuhusiana na Benki ya Wanawake; kwa kweli hii Benki ya Wanawake sisi kwa Wanawake ni mkombozi na nilisema kwamba imeshafungua baadhi ya madirisha katika baadhi ya Mikoa ambayo sio ming, ningeomba Serikali kwa kweli iangalie kwa karibu ili iweze kuipatia ile pesa ambayo ruzuku ambayo ilikuwa Serikali imeamua kuwapatia ili Wanawake wote wafaidike kwa sababu Wanawake wengi sana walikuwa wanaaibishwa, ndoa nyingi sana zimevunjika kwa sababu wanaenda kuchukua kwenye taasisi za fedha nyingine ambazo zinawafanya wanawake wanadhalilika wanawake ndoa zimevunjika, wanauziwa mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naamini kwamba kwa sababu Serikali na tulikaa kwa pamoja na tukaamua kwamba Benki ya Wanawake iwanufaishe Wanawake wote basi Serikali iweze kutoa pesa ambayo ruzuku ilikuwa imeahidi kwamba ingeweza kuwa inatoa kila bajeti ili madirisha mengi sana yaweze kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kinu chetu cha Iringa pale National Milling, nililisema siku ile kwenye swali, kile kinu tuna imani kwamba NSSF walisema kwamba wangetusaidia ili kile kinu kiweze kusaidia wakulima wa Iringa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwa kweli hili nalo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwamba makinikia yetu sisi Iringa ni vinyungu, utaona Wabunge wengi sana wamechangia hapa wakizungumzia kuhusu vinyungu. Vinyungu ndio mkombozi wa wana Iringa sasa nisipozungumza sasa hivi wanawake wote wanashindwa, maana yake ilikuwa mwaka mzima unalima, mwaka mzima unafanya biashara kupitia vinyungu vile, hata mimi mwenyewe nimesomeshwa kwa vinyungu. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi naomba Serikali iangalie upya hili suala la vinyungu maana yake hata kwa Wasukuma kule wanaita majaruba maana mimi nimeolewa na Wasukuma wanaita majaruba kwa hiyo kila nchi wanaita kwa majina yao, kwa hiyo ningeomba hivi viangaliwe upya ili wananchi waendelee kutumia maana yake naona Wabunge wengi wa Iringa pia wamezungumzia kwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza haya kwa kweli kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na niseme kwamba Waziri wa Fedha kanyaga twende, fanya kazi, tunajua kwamba tunakuamini, wewe ni Waziri ambaye umekuwa ukitusaidia sana, kwa hiyo, endelea na Naibu wako, fanyeni kazi leteni bajeti na niombe sasa pesa zifike kwa wakati kwenye Halmashauri zetu ili ile miradi ya muda mrefu iweze kumalizika kwa wakati kwa sababu tumekuwa na miradi mingi ya muda mrefu ambayo sasa mkichelewesha pesa gharama inakuwa inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nikushukuru na ninaunga mkono hoja kwa asilimia 150.