Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kupata nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia bajeti hii ambayo mimi naiita ni bajeti sikivu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niungane na Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa dhati kabisa wametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua za dhati anazochukua kulinda raslimali za Nchi yetu ya Tanzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ujasiri na uthubutu wa Dkt. John Pombe Magufuli haupo tu ndani ya Tanzania bali umevuka mipaka ya Tanzania. Mimi mlinipa heshima mlinichagua kuwa Mbunge kuwakilisha Tanzania kwenye Bunge la nchi za SADC mara zote hivi karibuni nilipokuwa nikienda kwenye vikao vya Bunge la SADC, Wabunge wote wa nchi za SADC ambazo ni nchi kama 14 wakiwemo na Maspika wa nchi zao, tunapokutana, tulikuwa South Africa, tulikuwa Namibia, kila unapojitambulisha kama ni Mbunge umetoka Tanzania baada ya salamu tu, suala linalofuatia ni kuuliza how is Magufuli doing? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana shauku ya kujua wengine wanauliza huyu mtu kabla hajawa Rais alikuwa nani, wanataka kujua ni kwa sababu ya uthubutu na ujasiri ambao kwa kweli umevuka kiwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo naipongeza bajeti hii kwa sababu ni bajeti sikivu kwa maana ya kwamba imezingatia maoni ambayo kwa muda mrefu Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiyatoa na tumekuwa tukitaka yatekelezwe, sasa yamekubalika na ndiyo maana naiita bajeti sikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba ukiacha Madini eneo lingine ambalo kuna potential kubwa ya kupata mapato ni eneo la gesi asili. Ushauri wangu hapa ni kwamba Bunge lililopita Bunge la Kumi, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini tuliunda Kamati Ndogo ambayo tulipitia mikataba ya gesi na kuona loophole na mianya ambayo inaleta upotevu wa fedha kwenye sekta ya gesi asilia. Nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Mipango atafute report ya Kamati Ndogo ya Nishati na Madini iliyoshughulika na gesi ya mwezi Novemba, 2011.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mapendekezo mengi na ushauri ambao tumetoa ya namna ambayo Serikali inaweza kupata mapato mengi tu ya kutosha kutoka kwenye sekta asilia ya gesi, pamoja na kwamba gesi kubwa ambayo tumevumbua sasa hivi haijaanza kuzalishwa, lakini hiyo hiyo ya Songosongo kuna potential kubwa sana ya kupata mapato ambayo sasa hivi hatuyapati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha tafuta hiyo report upitie mapendekezo na ushauri nina uhakika utapata mambo mazuri tu hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu Jimboni kwangu kuna kero nyingi ambazo nataka zitatuliwe na mambo yote tunayoyahitaji, tunasema watu wetu wanahitaji umeme, wanahitaji maji, wanahitaji barabara, haya yote hayawezekani bila kupata rasilimali fedha na bajeti hii kwa kiwango kikubwa imekuwa very smart, imeainisha namna ambavyo wananchi watalipa kodi na watalipa kodi bila maumivu makubwa jambo ambalo litafanya tupate fedha za kutosha ili tuweze kushughulikia matatizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu kuna mradi mkubwa wa REA Phase III ambao zaidi ya vijiji 40 kwa mara ya kwanza haijawahi kutokea vinakwenda kupata umeme, lakini kuna vijiji ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikisubiri umeme vijiji vya Mwamala, Igusule, Lububu, Kasela, Kayombo, Karitu na Isagehe kwa kipindi kirefu mno, kila ninapokwenda kule kero yao ni nishati muhimu ya umeme na sasa hili linakwenda kutokea kwa vitendo. Kwa hiyo, ninaipongeza sana bajeti hii kwa kuzingatia hilo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalonifanya kifua mbele kabisa kupongeza bajeti hii ni namna ambavyo bajeti hii imepunguza ushuru wa mazao. Jimbo langu la Bukene asilimia 90 ni vijiji na shughuli kubwa ya wananchi kule ni kilimo cha mpunga, kilimo cha mahindi na hii hii mpunga na mahindi ni mazao ambayo kwetu sisi ni ya biashara, lakini hayo hayo pia ni mazao ya chakula. Kwa hiyo, wananchi wengi wamekuwa wakisafirisha mazao yao kwa ajili ya kuuza, lakini kulikuwa na kero hiyo ya kwamba hata gunia tano/sita chini ya gunia kumi watu walikuwa wanatozwa kwenye vivuko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti imezingatia hilo na kuanzia sasa chini ya tani moja ambayo kama ni magunia ya kilo mia mia magunia kumi hayatatozwa chochote kwenye mageti kwa hiyo nia jambo ambalo wapiga kura wangu wamekuwa wakinipigia simu wakifurahia na kusema kweli kwamba hii Serikali ya Awamu ya Tano kweli ni Serikali kwa ajili ya wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kodi ya majengo na tunafahamu Urban Authority Rating Act inazipa Halmashauri uwezo wa kutoza kodi za majengo, lakini ushauri wangu hapa ni kwamba namna ya utekelezaji ambao unafanyika huko ngazi za chini na niseme hapa kwamba ninafahamu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano siyo kuwanyanyasa au kuwasumbua wananchi na sisi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kwenye ngazi za Halmashauri ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba Wakurugenzi na wataalam hawakiuki au hawatekelezi jambo hili kwa namna ambayo inaleta madhara, ninafahamu maeneo mengine kwa mfano Nzega, tumeanza kuweka alama kwenye nyumba kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kwenye zoezi hilo, lakini maeneo mengine Watendaji wamekuwa wanakwenda kinyume wanaweka alama kwa ajili ya kutoza hadi kwenye nyumba ambazo zimeezekwa kwa nyasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba ambazo zimejengwa kwa matope ambazo sio nyumba za kudumu, na tunajua utaratibu na muongozo ni kwamba kodi ya majengo ilipwe kwenye nyumba za kudumu na nyumba ya kudumu ni nyumba ambayo imejengwa kwa matofali ya saruji au matofari kuchomwa na imeezekwa kwa bati. Lakini sasa maeneo mengine kwa makosa ambayo haya ni makosa ya Watendaji, siyo sera, siyo sheria, ni watendaji maeneo mengine ambako unakuta hata nyumba za nyasi, nyumba za matope ambazo sio za kudumu nazo wanazitosa kodi ya majengo. (Makofi)
Lakini hili ni jambo la sisi hatuwezi kutegemea Mheshimiwa Mpango aende kijijini kwangu kule Semembela akaseme hii nyumba inafaa ni sisi sasa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kwenye ngazi za Halmashauri tusimamie hilo ili kodi hii isiwe kero kwa wananchi. Lakin nishauri Halmashauri pia zianzishe mfumo wa kuzitambua hizi nyumba, ili uwe na uhalali wa kuitoza nyumba ushuru wa majengo ni lazima uitambue. Kwa hiyo maeneo ambayo nyumba zimeishajengwa na hauwezi kutoa hati basi angalua mfumo wa kutoa leseni za makazi, kama ambavyo Halmashauri nyingine zinafanya basi ufanyike ili nyumba itambulike na baada ya hapo ikionekana ina sifa za kuanza kutozwa kodi iweze kutozwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufanya majadiriano na kukubaliana na Serikali ya Uganda ili bomba la mafuta lipite kwetu, kutoka Uganda mpaka Tanga na hili bomba Jimboni kwangu litapita kwenye Kata kama tano; Kata ya Igusule, Kata ya Mwamala, Kata ya Kasela na Kata Mwangoye. Ushauri wangu yule Mkandarasi Mkuu atakayepewa kazi ya kujenga bomba, basi kazi ndogo ndogo atoe, agawe kwa wakandarasi wa ndani lakini maeneo ambayo bomba la mafuta litapita wale vibarua ambao wanatakiwa kufanya kazi zisizohitaji ufundi basi watoke maeneo hayo hayo ya vijiji, ambalo bomba linaweza kupita ili angalau wananchi waweze kunufaika na bomba hilo kupita kwenye maeneo yao. Naunga mkono hoja asilimia mia moja.