Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RICHARD P. MBOGO:Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa nafasi ambayo anatupatia na pili kwanza niunge mkono hoja ya bajeti hii ambayo Waziri amewasalisha nawapongeza kwa uwasilishaji mzuri, na pia kwa Waziri kuwa flexible na comments za Wabunge pamona na wadau mbalimbali ambao umeweka ndani ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitakuwa sina furaha kama nisipompongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ya pekee ambavyo amekuwa na jitihada katika kuendeleza Nchi hii, tumeona katika hotuba kuna maeneo ambayo yamepewa msukumo wa kipekee ambao ni msukumo tunasema wa Mheshimiwa Rais. Tukianzia na ujenzi wa reli ya standard gage, ni msukumo wa Rais, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Air Tanzania nimeshangaa sana kuona baadhi ya Wabunge na hasa rafiki zangu kule wanakandya juu ya kufufua Air Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani nchi yoyote ambayo inataka kukuza utalii lazima usafiri wa ndani uimarishwe, Ethiopia kuanzia mwaka 1963 waliweza kuanzisha Shirika la Ndege na wamelisimamia mpaka leo limekua na Addis Ababa ndiyo hub ya dunia nzima na wanaweza kukuza uchumi wao na sasa hivi wameongezea maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona juhudi za Rais pia kwenye Mchuchuma na Liganga. Tunaomba Serikali muangalie huyu mwekezaji ambaye yuko tayari kutoa huu mtaji tuharakishe aweke fidia kwa wananchi kazi ianze. Tukipata chuma pamoja na umeme tutapunguza gharama ya uendeshaji wa Shirika la TANESCO maana sehemu nyingine ambako hakuna gridi ya Taifa wanatumia majenereta na uendeshaji wa mafuta ni mgumu ndiyo maana kila siku tunataka bei zipande na inakuwa ni gharama kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ya uwekezaji na pia kwenye gesi ya kimiminika ambako Serikali imewekea mkazo yote ni maeneo ambayo ya msukumo wa kipekee ambayo bajeti hii imewapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nizungumzie kuhusu tozo ya shilingi 40 ambayo tumeweka kwenye mafuta. Mheshimiwa Waziri kama itakupendeza tubadilishe tu jina, hii tuite tu tozo kwa ajili ya Mfuko wa Maji Vijijini. Kwa nini nasema hivyo? Mwaka jana tulikulilia sana kuhusu Mfuko wa Maji Vijijini, lakini ukasema tusiongeze kwenye mafuta kwa mwaka jana wa fedha ambao tulikuwa tunaujadili 2016/17. Basi mwaka huu hii shilingi 40 iwe ring fenced kwenda kwenye maji ili makusanyo ya fedha hizi moja kwa moja tuwe na cash flow inayotosha kwa ajili ya maji vijijini na ile bajeti ambayo tumeikubali mliyoishusha ya Wizara ya Maji kutoka shilingi bilioni 900 mpaka shilingi bilioni 600 lakini kwa Wabunge wote tulisema kwamba bajeti hii ikamilike kwa asilimia 100. Sasa ili iweze kukamilika kwa asilimia 100 bajeti ya shilingi milioni 600 lazima tuwe na chanzo cha uhakika.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kwenye mabadiliko ya Sheria yako kwenye Finance Bill ambayo utaileta hii tuiwekee amendment na mimi nitakusaidia ku- lodge schedule of amendment ili fedha hii iwe ring fenced kwenye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nije kwenye tozo ambazo zinahusu Halmashauri. Tunajua nia kabisa ya Serikali ni kuondoa mzigo kwa wakulima, lakini naomba tu nikumbushe Bunge lako ni kwamba Halmashauri zilianzishwa kwa mujibu wa Katiba, Ibara 145 na 146 ni kwa ajili ya kushughulikia wananchi wetu huku chini. Sasa zimeathirika kwa namna tatu, namna ya kwanza kwa kubadilisha Sheria namba 290 ambapo tozo ya mazao inashusha kutoka asilimia tano mpaka tatu na mbili kwa mazao ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya pili ambayo Halmashauri zinaathirika ni kutokana na baadhi ya makusanyo kuchukuliwa na TRA ambapo ni mabango na property tax. Aina ya tatu, Halmashauri zinaathirika kwa mapato yao ya ndani ni kutokana na namna ya ujazo ambapo umeweka kwamba chini ya tani moja mtu asiweze kutozwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianzia kwenye tozo. Mfano Halmashauri yangu ya Nsimbo asilimia 50 ya makusanyo tunapata kutoka kwenye zao la tumbaku. Kwenye bajeti hii 2017/2018 kwenye tumbaku tunatarajia kupata milioni 440 ambapo fedha hii tulikuwa tunatarajia kwamba iingie kwenye miradi ya maendeleo. Sheria mnaijua kabisa, makusanyo ya ndani na asilimia 60 inapelekwa kwenye miradi ya maendeleo na ndani ya asilimia 60 kuna ile asilimia tano ya vijana na akina mama. Kwa hiyo, kwa kupunguza haya makusanyo ya Halmashauri na kwenye bajeti yetu hapa Halmashauri zetu ni shilingi bilioni 687 matokeo yake hizi zinaenda kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutaomba Waziri atuambie compensation ya hizi Halmashauri kutokana na kuathirika kwa mabadiliko ya sheria namna ya kutoza wana- compensate kiasi gani. Mimi nitaomba Mheshimiwa Waziri, kabla hatujaenda kwenye schedule of amendment na tukakubaliana kukubali mabadiliko yako au kuyakataa, tutaomba comfort yako ni jinsi gani Serikali inaenda kufidia Halmashauri zetu ambazo zinaathirika. Halmashauri nyingi hasa za vijijini wanategemea hizi tozo. Kwa mfano ukienda hapa Gairo ni mazao tu, hamna dhahabu hamna nini, wanategemea mazao haya. Ukienda Vwawa – Mbozi wanakusanya karibuni bilioni tatu, ni kwenye mazao, ukienda Nsimbo na Halmashauri nyingi. Sasa hapa Serikali naomba mjiandae, bila comfort kwakweli tutakutana kwenye schedule of amendment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu kilimo, Serikali ina nia nzuri kabisa.Tumeona tozo mbalimbali zimepunguzwa kwenye aina mbalimbali za mazao lakini kwenye mbegu Mheshimiwa Waziri hatujaona! Hujafuta VAT ili mbegu inayozalishwa humu ndani nchini iweze kushindana na ile ambayo inatoka nje ya nchi. Vile vile kwenye kilimo Mheshimiwa Waziri bado Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo hujaiongezea mtaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utalii; bajeti yako na tunajua nia kabisa ya Serikali ku-promote utalii lakini pia bado tunahitaji tuone juhudi zaidi ili utalii wetu uweze kufidia suala la mapato ndani ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu madini. Nashukuru sana umeongeza baadhi ya tozo kwenye madini, lakini watu wenye leseni za madini primary license, mining license they are always doing false declaration on their revenue. Hawasemi ukweli juu ya mapato, kwa hiyo Serikali ione namna gani ili soko liwe huru watu waje pale wauze kwa uhuru na Serikali iweze kupata mapato. Leo hii muulize mtu hata mwenye leseni sehemu zote za madini au leseni ndogo PML au ML, waulize kwa mwaka wanaingiza ngapi? Hawakuambii ukweli lakini tunaona maisha yao yanavyokwenda na Serikali tupate mapato. Mimi tu Halmashauri ya Nsimbo service levy hatupati! Wananunua, wanauza kimya kimya/kisiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niombe tena kuzungumzia kuhusu Benki Kuu ya Tanzania. Benki Kuu ya Tanzania inatanua huduma kanda mbalimbali. Tunaomba Kanda ya Magharibi Benki Kuu ijengwe tawi pale Katavi. Ukiangali Katavi pale kiusalama ni mbali na Ziwa Tanganyika na nchi zinazotuzunguka za majirani. Kwa hiyo, tawi la Benki Kuu lije lijengwe pale Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu kodi kwenye mafuta ya ndege. Umeongeza kodi kwenye mafuta ya ndege ne tunajua kila ndege inamaximum takeover weight kwa hiyo tutawafanya kwamba wasiweke mafuta mengi hapa kwetu wanaenda kujaza sehemu nyingine hasa ndege za transit kwa hiyo tunaomba kodi hii Waziri aisimamishe kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa upande wa Serikali yetu, bajeti yetu ya trilioni 31 kodi ni trilioni 17. Nimuombe Waziri, hapa TRA wamejifunga kitanzi. Ongezeko la mpaka Juni tunatarajia mtakusanya trilioni 14.2; lakini kwenye bajeti 2017/18 makusanyo ya kodi ni trilioni 17. Sasa mnaenda kufanyaje ili ongezeko la trilioni mbili na ushee liweze kupatikana.