Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupewa nafasi hii. Naanza kabisa kwa kutoa pongezi na kuunga mkono hoja hii, bajeti iliyo mbele yetu kwa kweli imetayarishwa kwa umakini mkubwa na inahitaji kuungwa mkono. Kwa hiyo ninaposimama hapa nataka kuboresha sehemu mbalimbali ambazo nadhani Mheshimiwa Waziri akiendelea kuzifanyia kazi bajeti hii itakuwa bora zaidi kabla haijakamilishwa.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuokoa muda nina vipengele mbalimbali ambavyo nitaviwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri kwa maandishi, Ibara kwa ukurasa, lakini kwa ufupi tu nianze kabisa na ukurasa wa pili, Ibara ya 4. Mambo yote aliyoorodhesha na matukio makubwa yametokea na namuunga mkono, hiyo nadhani Mheshimiwa Waziri na nimewaambia wapiga kura wangu hii si kwa hila bali kwa kusahau, tukio kubwa sana lilitokea tarehe 10 Septemba, 2016, Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tetemeko kali. Katika tetemeko hilo watu wakapoteza maisha yao na watu wakapoteza mali zao.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru sisi wa kutoka Kagera kwamba Waziri Mkuu hakuchelewa, alikwenda kwenye mazishi na hatimaye Mawaziri mbalimbali walikuja pale kutufariji na ninyi Bunge Tukufu mkachanga mchango ambao umetusaidia kwa wale wahanga walioathirika. Nawashukuruni sana.
Mheshimiwa Spika, sasa hii ni bajeti, nilitegemea na naomba Mheshimiwa Waziri aone kwamba sisi wahanga wa tetemeko hatujioni katika bajeti hii, watu walioathirika tunaendelea kuwaleaje ili kuwasaidia kuondokana na kadhia iliyowakuta?
Mheshimiwa Spika, nina pendekezo kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba ahimize viwanda na aviwezeshe kufungua factory outlets. Factory outlet nadhani anaelewa maana yake, ni viwanda vya vifaa vya ujenzi hususan Kiwanda cha Twiga, Dangote na hao watu wa Tanga na Mbeya wawe na maduka yao kule Mkoa wa Kagera. Zile zinaitwa factory outlets, ni concept ambayo anaielewa, ni sehemu moja ya kusaidia watu kuweza kujenga makazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipofika kule, yeye anahangaika na shule na miundombinu tunamshukuru, lakini sasa wananchi vifaa vya ujenzi inakuwa ni ngumu kupatikana. Nitoe mfano, mfuko wa cement ‘X’ factory pale Dar es Salaam Twiga ni Sh.9,000/=; unapofika Kagera ni Sh.15,000/=. Kwa hiyo, unaona kwamba mwananchi wa Kagera, huyu mhanga wa tetemeko hawezi kwenda mbele. Hilo naamini kwamba atalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo napenda ku-highlight katika orodha yangu ya vitu kadhaa ambavyo naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, kuna issue ya ukwasi katika uchumi wetu. Mheshimiwa Waziri, yeye ni mchumi mwenzangu na anajua kwamba ukwasi ndiyo damu inayoendesha uchumi. Katika hili wamejitahidi sana, naomba nimupongeze kwamba katika bajeti hii mabenki yatawezeshwa sasa. Wamepunguza vile viwango, yaani minimum reserve wanayoweka kule Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, kuna sekta moja ya fedha ambayo Mheshimiwa Waziri anayoisahau, nami hapa nitangaze mgongano wa maslahi au na-declare interest kwamba mimi ni mdau pia wa Sekta ya Bima kama vile wengi tulivyo wadau katika Sekta ya Benki. Maana yake ukiwa na hisa katika sekta hizi, tayari umeshakuwa mdau, au siyo?
Sasa bima hizi; unajua ukwasi katika bima ni mbaya sana na unaendana sambamba na mabenki. Kwa hiyo, nafikiria hapo angepaangalia namna ya kuwasaidia wasije wakafunga Makampuni ya Bima, badala ya kujenga Makampuni haya tukakuta tunarudi nyuma. Kwa hiyo, hilo nalo ni la kufanyia kazi katika bajeti yetu ambayo ni vizuri.
Mheshimiwa Spika, kitu ambacho naomba nipongeze, tumesikia mengi kuhusu vyeti feki, Mheshimiwa Rais amekamilisha mengi. Watu ambao walikuwa na vyeti feki, nadhani sheria imefuata mkondo wake. Katika bajeti hii kuna kitu ambacho nimekiona kimeni-strike, kumbe kulikuwa na madai feki katika Serikali! Watu walikuwa wanaidai Serikali vitu, kumbe madai yao hayakuwa halali! Naomba jambo hili tulinyooshee bango; watu wanaokwenda kuweka madai feki Serikalini, nao tuwajue, maana Tanzania ni nchi ya uwazi na ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tupo katika awamu ya uwazi na ukweli, kwa hiyo, watu kama hao waliokuwa wanakwenda kudai zaidi ya shilingi bilioni zaidi ya 900 ambazo wamezikomboa, wajulikane ni akina nani, kusudi wawe blacklisted wasiendelee kutusumbua katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia hapo hapo niongezee kwamba katika bajeti hii ambayo ina mambo mengi, kuna suala la wakulima. Ninaposimama hapa, Muleba Kusini sisi ni wakulima wa kahawa, ndizi, mpunga na maharage. Sasa ukiangalia ruzuku zinazokwenda kusaidia
wakulima, Mkoa wa Kagera nasikitika kwamba hazitufikii kabisa. Katika hali hiyo, wakulima unawasaidiaje? Naomba nimpongeze na nishukuru kwamba kodi kwenye kahawa imepunguzwa, lakini bado kuna msururu wa kodi kwenye kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi maboresho ambayo wamefanya, hizi kodi 17 zilizoondoka, zimeondoka kwa wale ambao ni wafanyabiashara wa kahawa na viwanda vya kahawa, lakini mkulima bado amebebeshwa mzigo. Naomba Mheshimiwa Waziri yeye ni mchumi, afanye analysis, aangalie cost breakdown aone kwamba mkulima tunamsaidiaje?
Mheshimiwa Spika, nina pendekezo, hii cess ambayo imesemwa kwamba mazao ya biashara yanabaki kwenye 3%, tumetoka 5% mpaka 3% tunashukuru. Nataka nipendekeze kwamba mazao ya biashara sasa hivi na mazao ya chakula, yaani tofauti ni academic. Kwa mkulima, analima mahindi na kahawa ili auze. Sasa yule wa kahawa ambaye amebeba Taifa hili miaka mingi au yule wa korosho; ninapozungumza kahawa naweza pia kwenda kwenye mazao mengine. Kwa mfano, wakulima wa pamba, wale ambao wamebeba Taifa hili tangu uwepo wake, sasa hivi ni wakati wa Taifa kuwarudishia kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napendekeza hiyo cess na yenyewe iteremshwe ifike kwenye kiwango kinachostahili, wakulima waonekane sawa. Hapo sina budi kushukuru sana ukombozi ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta kwamba mazao tani moja mtu anaruhusiwa, ni ruksa kabisa kuyatembeza. Huu ni ukombozi kwa mkulima, pia kutusaidia sisi Wabunge huko kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa napambana na Halmashauri, wanaweka barrier feki, inabidi niziondoe. Mambo ni mengi, lakini nitayawasilisha kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.