Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja hii ya bajeti ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Wataalam wake kwa kutuletea bajeti hii ambayo ni muhimu sana. Bajeti hii kwa kweli imelenga hasa watu wa chini na wanavijiji. Tofauti na mwaka 2016 ambapo Mheshimiwa Waziri alikuwa anasita kidogo, lakini baada ya kusikia kilio chetu kikubwa, ameweza kuifanyia marekebisho bajeti hii kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuondoa tozo na ushuru mbalimbali, lakini bajeti hii ingekuwa na umuhimu zaidi katika suala la maji ambapo Mheshimiwa Waziri amelisahau kwa kiwango kikubwa sana. Bajeti iliyopita ya mwaka 2016 kwa kweli fedha za maendeleo kwenye Wizara ya Maji zilitolewa kwa kiwango kidogo sana. Kiwango cha asilimia 19 na point something ni kidogo sana. Sasa safari hii tulitegemea kwamba Wizara ya Maji itaongezewa na itapata kwa kiwango kikubwa sana fedha ambazo zingeweza kutosha hasa vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nakubaliana kabisa na mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati ya Bajeti ambayo kwa kweli ilishauri kwamba asilimia 70 ya mapato ambayo yanakwenda kwenye mfuko, yaende kwenye Mfuko wa Maji. Suala hili lingeweza kusaidia sana maji vijijini. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri aangalie suala hilo, ahakikishe kwamba atleast asilimia 70 katika Mfuko wa Maji unaongezewa ili wananchi wa vijijini waweze kuwa na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala la miradi 16 ambayo ilijadiliwa, tulipewa mkopo wa Dola milioni 500 kutoka India.

Naamini kwamba fedha hizi zikiweza kupatikana, zitaweza kuondoa matatizo ya maji kwa kiwango cha hali ya juu. Kwa sababu miradi 16 na miradi ambayo imesambaa nchi nzima, kila siku tunaambiwa kwamba kuna financial agreement ambayo inatakiwa isainiwe, tangu mwaka 2016. Mheshimiwa Waziri tafadhali sana, suala hili lipo kwenye mikono yake na kwenye Wizara yake, ahakikishe hiyo financial agreement inasainiwa ili kazi hii iweze kufanyika kwa bidii.

Mheshimiwa Spika, nilishauri wakati nachangia suala la bajeti ya madini na nishati kwamba sasa hivi ni lazima tuanzishe kiwanda cha kusafishia haya makinikia. Bila kuanzisha kiwanda hiki, Bunge halitaonekana linaunga mkono vizuri juhudi za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, jana kwenye mapendekezo ya Kamati, suala hili limetolewa kwamba atleast lazima tuwe na kiwanda hicho hapa, sasa huo ni mlango wa kutokea. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri aangalie bajeti yake, ajaribu kuifumua kuhakikisha kwamba tunakuwa na hiki kiwanda tuweze kuondoa haya matatizo mengi kwa sababu taarifa ambayo imetolewa jana, kwa kweli inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kampuni inafanya kazi hapa bila kuwa na leseni, kampuni imechukua madini chungu nzima, kuanzia miaka ya nyuma, matrilioni ya hela. Kwa kweli ni very absurd, sikutegemea kwamba kitu kama hicho kingeweza kutoka kwenye ripoti hiyo. Wametuachia mashimo! Wametuachia mahandaki! Kwa kweli sasa hivi never, never, never ever again, hatuwezi kukubali kuendelea kuwa na mahandaki humu ndani wakati tuna uwezo wa kufanya kila kitu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu Mheshimiwa Waziri aangalie suala hilo la uanzishwaji wa kiwanda na ni vizuri hata kama tutabaki na haya mahandaki, tubaki na haya mahandaki na mali zetu ziwe chini, lakini hatutakubali tena sasa hivi kutoa michanga kwenda nje kama alivyosema Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama kuna hizo kesi sasa hivi, sisi ndiyo tuna hoja. Sisi ndio tunatakiwa, kama wakikataa kukaa kwenye makubaliano, sasa hivi tuna hoja ya kuwashtaki sasa kuhusiana na fedha zote ambazo wameiba. Ni lazima tuhakikishe kwamba zinarudi.

Mheshimiwa Spika, suala la utalii utaona kwamba mchango kwenye pato la Taifa umepungua katika mwaka 2015/2016. Tumechangia kwenye asilimia 14 ukilinganisha na asilimia 17.5 ya mwaka uliopita. Hii ni kwa sababu ya VAT. Sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri akaliangalia hilo suala na kuhakikisha hii VAT ambayo inachajiwa. Hili tumelipigia kelele sana kwenye bajeti iliyopita. Kwa hiyo, ni vizuri kuiangalia, pia tuondoe hiki kitu, tupate watalii wengi ili tuweze kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni reli ya Tanga - Arusha na Musoma. Reli hii sasa hivi tunasubiri taarifa ya feasibility study ili iweze kuiuza kwa wafadhili kwa njia ya PPP. Sasa bado haijalipwa hela na Kamati ya Bajeti imeshauri vizuri kwamba fedha za kulipa feasibility study, basi zitoke kwenye Mfuko wa Reli ili tuweze kulipa mara moja. Kwa hiyo, ningeshukuru sana kama suala hilo lingetiliwa maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, suala zima la bajeti, bajeti ni nzuri lakini tunaomba utekelezaji wake, bajeti ikitekelezwa kwa kiwango ambacho tutaipitisha hapa basi itakuwa na maana, lakini kama bajeti tunapisha na haitekelezwi, kwa kweli inasikitisha sana. Sasa ni vizuri kutengeneza bajeti ambayo tunaweza kuipitisha. Tutakapoipitisha, itakuwa ni vizuri sana na papo hapo ni muhimu kuweka maanani kwamba siku hizi nchi nyingi hazi-include suala la wafadhili ambao wana-support kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri ufadhili ambao unatolewa usiingie kwenye bajeti kwa sababu mara nyingi unakuta wanapoahidi kwamba watachangia bajeti, kwenye hatua za mwisho utakuta hawachangii bajeti. Sasa ile inavuruga mipangilio yote. Ni vizuri tuweke bajeti yetu ambayo tunaweza kutekeleza kutokana na hela zetu na hizo fedha za wafadhili zije kama ni kitu cha baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo,naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.