Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika bajeti hii ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa bajeti nzuri ambayo ameileta Bungeni, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii bajeti kwa kweli inatekelezeka, ina vipaumbele ambavyo vinakuna maisha ya kawaida ya Watanzania na ina mambo mazuri. Kwa hiyo, nadhani kazi yetu sisi kama Wabunge ni kuendelea kushauri labda marekebisho au nyongeza, mambo gani yaongezewe katika hii bajeti ili iweze kuwa nzuri zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianzie kwenye Sekta ya Kilimo. Kwenye Sekta ya Kilimo inaonekana kwamba kilikua kwa asilimia 1.7 kutoka asilimia 2.1. Sekta ya Kilimo ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi hii. Kuna sekta ambazo tukiweka nguvu ya kutosha tunaweza tukaleta maendeleo ya kweli katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, labda nitaje sekta chache. Tukiweka nguvu kwenye Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, tukafanya vizuri, tunaweza kutoa mchango mkubwa sana katika nchi hii. Sekta hii ndiyo inayotoa ajira ya Watanzania walio wengi. Zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo. Kwa hiyo, lazima tuiangalie. Sekta ya Nishati na Madini, tumeona madini yako mengi. Tukiimarisha hii, tukaweka vipaumbele vizuri, tukaifanyia vizuri, tutakuwa hatuna shida ya fedha za kuendesha nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika Sekta ya Maliasili, ukiangalia mbuga za wanyama tulizonazo, ukiangalia mlima mrefu katika Afrika na wa pili duniani, ukiangalia mambo mbalimbali yanayohusiana na utalii, tukiyawekea mkazo mzuri, tunaweza tukafanya kazi nzuri na maendeleo ya nchi hii yatakimbia haraka sana.

Mheshimiwa Spika, nirudi sasa kwenye Sekta ya Kilimo. Kwenye kilimo Serikali imesema, sasa hivi kwenye upande wa pembejeo wamesema tutafanya bulk procurement. Ni imani yangu kabisa kwamba Serikali itatekeleza mwaka huu vizuri kabisa. Tukifanya hivyo, pembejeo zitashuka bei na kuwawezesha wakulima wetu kuweza kupata pembejeo kwa bei nzuri na hivyo kuongeza tija na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu kwenye Jimbo langu la Vwawa, Wilaya ya Mbozi, sisi ni wakulima sana, lakini tunahitaji pembejeo zije kwa wakati na kwa bei nzuri. Hiyo itatusaidia sana kuchangia mchango mkubwa katika Taifa hili. Pia kuna zao la kahawa ambalo lilikuwa linaongoza Tanzania kwa kutuingizia fedha za kigeni. Zao hili sasa limeshuka, sijui sasa limeshika nafasi ya sita! Lazima Serikali tukae chini tuangalie nini kimetokea kwenye zao la kahawa ili tuweze kulifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona kabisa sasa hivi mazao kama korosho yameanza kuongezeka na yameongeza mchango mkubwa, lakini zao la kahawa, nini kimetokea? Hebu Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anajibu aangalie nini tufanye katika hilo?

Mheshimiwa Spika, kwenye ufugaji tuondokane na uchungaji, twende kwenye ufugaji wa kisasa. Sasa hivi hakuna ufugaji wa kisasa, kuna uchungaji katika nchi yetu. Tukifanya hivyo, tukiwa na mashamba ya ufugaji, naamini kabisa tutaona mchango wetu.

Mheshimiwa Spika, kuna bahari kuu kule, kuna deep sea, hatujaweka jitihada za kutosha kwenda kuvua. Wananchi wetu wanakufa, watoto wetu wanakufa kwa magonjwa mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa chakula. Tungekuwa tumeimarisha uvuvi tukapata samaki, tukawalisha wananchi wetu, mimi naamini hata magonjwa yangepungua. Kwa hiyo, nadhani jitihada lazima zichukuliwe na Serikali katika kuimarisha hii Wizara ili tuhakikishe kwamba inatoa mchango mzuri katika kuimarisha uchumi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili katika upande wa kilimo, nimeangalia sana hii bajeti, inazungumzia subsistance agriculture. Hatuwezi kuendeleza nchi kwa kilimo kidogo kidogo hiki, lazima kama nchi twende kwenye commercial farming. Bila kwenda kwenye commercial farming hatutafika. Lazima jitihada ziwekwe. Nimeangalia mkakati, bado hautoshi, commercial farming bado haipo. Huwezi kuleta maendeleo ya nchi kama hakuna commercial farming, huwezi!

Mheshimiwa Spika, sekta hii ambayo tunasema inatoa ajira kubwa, watu wengi are not included. So, kwenye ile tunaita financial inclusion wengi hawapo included. Huwezi kuwa- support mmoja mmoja, lakini kukiwa na kilimo cha kisasa, kukiwa na maeneo au mashamba yametengwa, tukazalisha vizuri, tutatoa ajira nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ninalotaka kuchangia, nimeona watu wengi wamechangia kuhusu Property Tax, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amesema Property Tax sasa itakuwa inakusanywa na Wizara ya Fedha kupitia TRA. Naomba niliweke vizuri. Mheshimiwa Waziri alichosema, hajasema Property Tax yote itakusanywa na TRA. Amesema kwa mwaka huu wanaanza na miji, fedha zitakusanywa na Property Tax na TRA na baada ya kukusanywa ndiyo zitapelekwa sasa, zitarudishwa huko.

Mheshimiwa Spika, huko vijijini bado hawawezi kufika, itakuwa bado ni kazi ya Halmashauri. Hebu tuangalie bajeti ya maendeleo. Maendeleo ya nchi hii tunapozungumzia bajeti ya maendeleo ya nchi hii, maendeleo yanayofanywa na Serikali Kuu yanahusu nchi nzima bila kujali ni wapi. Tumeona sasa hivi flyover zinajengwa pale Dar es Salaam, tunasubiri zije hata huku Dodoma zijengwe flyover maana huku ndiyo Makao Makuu ya Mji, tunahitaji maendeleo nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inapokusanya, nami naona kabisa kuna logic. Hebu makusanyo haya tuyakusanye mahali pamoja ili tuweze kutekeleza vipaumbele vile ambavyo vitachochea maendeleo ya nchi. Hii kutawanya mapato mara huku, mara huku, ndiyo kunakuwa na wizi na matumizi mabaya ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Halmashauri yangu kule matumizi ya fedha yalivyo. Makusanyo watu wengi wanaiba. Hata ukiwaambia watumie vifaa vya ki- electronic, wanakuwa navyo lakini hawatumii, wanaiba. Hawa wenye uzoefu wa kukusanya, wakikusanya zikakaa kwenye kapu moja, tutatenga vipaumbele, tutaelekeza kwenye vipaumbele na maendeleo yatakimbia haraka sana, tutaona nchi yetu inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, ni vizuri, maana uzoefu unaonesha kule kwenye Halmashauri zetu zipo Halmashauri sasa hivi hazina uwezo wa kulipa posho za Madiwani. Fedha hizi zikikusanywa zikaanza kupelekwa kule, watatekeleza miradi ya maendeleo, wataweza kufanya mambo mengine, watalipana hata posho za Waheshimiwa Madiwani, kuliko ilivyo sasa hivi makusanyo hayaridhishi katika maeneo mengi kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, naunga mkono hoja, lazima Serikali ikusanye makusanyo pamoja ili yaweze kutoa mchango mzuri na maendeleo ya nchi yaweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kule Jimboni kwangu, ile asilimia 20 inayotakiwa irudi kwenye vijiji, hairudi. Wakikusanya zinatumika hovyo. Hawawarudishii wale wakusanyaji. Usipowa-motivate wakusanyaji, kesho hawawezi kukusanya, nao wanatafuta mbinu nyingine za kuweza kujilipa wenyewe. Kwa hiyo, lazima mikakati iwekwe vizuri ili kuhakikisha kwamba hii fedha inakusanywa na inawekwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, hii Sekta ya Utalii mwaka 2016 tuliweka VAT. Hebu tuangalie, idadi ya watalii waliongia kwenye nchi hii inaonekana wameongezeka, lakini ukiangalia mapato yanayotokana na Sekta ya Utalii, bado siyo mazuri ukilinganisha na nchi jirani kama Kenya.

Mheshimiwa Spika, hii inatupa kwamba kuna mambo lazima tuyafanye kwenye Sekta ya Utalii ili tuweze kuhakikisha kwamba hii sekta inatoa mchango wa kutosha katika kuiendeleza nchi yetu. Naamini tukiweka mikakati mizuri, tukatathmini ile impact ya VAT, maendeleo ya nchi hii yatabadilika kwa haraka sana. Ni muhimu haya mambo yakaangaliwa kwa mapana na marefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba nitamke kwamba naunga mkono hoja na juhudi zote zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwatetea na kuleta maendeleo ya kweli katika nchi hii. Sote lazima tushikamane; na hivi ni vita, lazima wote tupigane katika kuhakikisha tunaleta maendeleo ya kweli. Hizi tofauti za kisiasa hazitusaidii kutupeleka kokote, hebu tushikamane kuleta maendeleo ya kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante sana.