Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

HE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia bajeti ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, lakini niwapongeze Menejimenti nzima ya Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti nzuri, bajeti ya kihistoria, bajeti ya Watanzania, bajeti ambayo Wabunge wengi walipigia kelele vitu vyao, leo tumeviona kwenye bajeti hii. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kuhusu Motor Vehicle. Sisi Wabunge kwenye bajeti ya fedha tulisema kwamba tunaomba Motor Vehicle iondolewe, Serikali imetusikia. Napata taabu kuwaona Waheshimiwa Wabunge leo hapa wanalaumu kwa nini Serikali imeondoa Motor Vehicle na imeweka Sh.40/= kwenye lita ya mafuta kama tozo kwa ajili ya Road License. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana dada yangu Mheshimiwa Susan Lyimo aliongea hapa kwamba tunawaonea watu wa vijijini wanaowasha vibatari, kwa nini tunawawekea tozo ya mafuta? Mheshimiwa Msigwa pia aliongea, kaka yangu Mheshimiwa Heche ameongea hapa. Niwaulize tu, tunalipa tozo ya Railway Development Levy, Arusha kuna treni?

Mheshimiwa Spika, mimi nimezaliwa Tabora tena Mjini. Toka nimezaliwa umeme unawaka kwetu, lakini natozwa tozo ya REA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalipa tozo ya maji, mimi kwetu mjini, kuna maji toka nimezaliwa, lakini nalipa tozo ya maji. Waache kutuchonganisha na Watanzania.

TAARIFA .....

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Spika, nimemsikia Mheshimiwa Msigwa.

Mheshimiwa Spika, wamesema kuna mtu ana generator, kuna mtu ana mashine ya unga, kwa nini anatozwa Sh.40/= kwa ajili ya Road License? Wamesahau tunalipia reli, tunalipia maji, tunalipia umeme wa REA na sisi tunakaa mijini. Kwa hiyo, mimi wa mjini ningesema sitaki kutozwa tozo ya REA kwa sababu mimi sikai kijijini. Baba yangu alishakufa, mama yangu alishakufa, bibi yangu alishakufa; sina ndugu kijijini.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mtanzania, tumejengwa kwenye umoja, ndiyo utamaduni wetu, tumejengwa kusaidiana. Leo napata taabu anaposimama hapa Mbunge anatubagua, anasema kwamba hawa watu wa vijijini tunawatoza Sh.40/= wakati hawatumii barabara. Nani asiyetumia barabara? Nani ambaye hatumii barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waache kutuchanganya, waache kutuchonganisha. Sisi ni wamoja na tutaendelea kuwa wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu waache kuichanganya Serikali. Hawa watu wamwache Rais Dkt. Magufuli afanye kazi! Niliwahi kusema humu ndani tumwache Rais afanye kazi na anafanya kazi. Kazi yetu sisi ni kumwombea na kumuunga mkono; lakini wenzetu hawa mimi napata shida kweli, sijui wanamaanisha kitu gani? Wanakuja kuleta sababu ambazo hazina msingi kabisa hapa. Uzalendo wao ni mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais leo anapambana kuhusu rasilimali za Taifa. Mgogoro huu ukikaa mezani, mambo haya yakiwekwa vizuri tutapata zahanati, tutapata maji, tutapara barabara. Mheshimiwa Rais ambaye anafanya kitu ambacho ni cha ukombozi kwa Tanzania, tumeibiwa muda mrefu, tumeonewa muda mrefu, anapambana, badala ya sisi tumuunge mkono, mtu anakuja kulalamika. Halafu mtu huyo huyo anasema sina maji kwenye Jimbo langu, sina zahanati kwenye Jimbo langu, rasilimali zinaibiwa. Mheshimiwa Rais leo amejua, anapambana tuzirudishe, lakini mtu huyu hataki, anasema tunawaonea Wazungu, tunavunja mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza, jana umesema kama nimenukuu vizuri: “Hata kama mikataba imeingia miaka 50 iliyopita, lakini kama ni mikataba ya hovyo tutaikataa.” Amesema kipande chake cha Bunge kitatenda haki ikiwa ni pamoja na kubadilisha sheria hizo haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa uzalendo wako, nasi Wabunge wako tuko nyuma yako tunakuunga mkono, tunazubiri sheria hizo zije tuanze kuzibadilisha haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima Watanzania waelewe kwamba huyu mzee wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya nini? Jana kuna statement aliitoa mpaka nilitamani kutao machozi. Alisema: “Jamani na mimi nina damu, nami ni binadamu, lakini naumia kwa sababu yenu ninyi.”

Hivi Mheshimiwa Dkt. Magufuli angetaka kupokea mabilioni, angetaka kupokea mahati ya nyumba ya Marekani ili akae kimya tu, tungemfanya nini?

Mbona tunaibiwa siku zote hivi vitu? Ameonesha uzalendo wake. Mimi sitaki kuamini kwamba hakufuatwa kupewa hela, lakini amekataa chochote, anataka Watanzania wote wafaidi.

Anainuka Mbunge anakutaja kupingana na jambo hili ambalo ni kwa faida yetu sisi zote.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumpongeze Mheshimiwa Rais, tumuunge mkono na tuendelee kumwombea Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya…

TAARIFA......

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, naomba unitunzie muda wangu. Naomba nimwambie dada yangu Mheshimiwa Sophia, mabadiliko hayana wakati. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutuletea Rais jembe, Rais mpambania wanyonge, Rais mpambania maskini, Rais ambaye hana tamaa yake binafsi na familia yake. Leo hii Rais Magufuli angekuwa na tamaa yake na familia yake angekomba mahela yote akaenda kuweka Uswiss huko na yeye na tungeendelea kuibiwa hapa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambie hawa watu ambao hawajui madini; siku ile Mheshimiwa Musukuma aliwaambia, mimi nimetoka Tabora Nzega, ukiona mashimo yaliyopo kule utalia. Kodi iliyolipwa kwa muda wote na Resolute haizidi shilingi bilioni 30. Wametuibia vibaya sana, wameondoka Halmashauri ya Nzega tunawadai Development Levy ambayo walitakiwa walipe shilingi bilioni 10 mpaka leo hawajalipa, Serikali inajua. Toka wameingia mpaka wanaondoka pale wamelipa shilingi bilioni mbili tu ya levy ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mwingine anaongea tu, hajui chochote anachokiongea. Mimi nampongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli na nimefunga na sala zangu zote namwombea kwa Mwenyezi Mungu. Maadui wengine wa Rais Magufuli tunao humu ndani, sijui wanataka nini hawa watu. Mtu anapambana kwa sababu yetu na watoto wetu, hivi vyama kuna vipindi tuweke itikadi pembeni tuangalie Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniongezea dakika kumi. Kwa kweli kuna vitu ambavyo tunashangaza sana kwetu sisi. Nikitoka kuongea mambo ya makinikia ambayo ni mambo yamegusa Tanzania nzima; kule Tabora kuna Mwenyekiti wa UKAWA, jana amenipigia simu ameniambia Mheshimiwa Munde nimeenyoosha mikono kwa Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutaka kuwadhibitishia hilo, nikimaliza Bunge nitafanya mkutano wa hadhara Tabora nitamkabidhi kadi ya CCM ili wajue kwamba Watanzania wamemkubali Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa asilimia 100. Nilisema humu Bungeni kwamba wataelewa tu na wameelewa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba kazi tuliyonayo mbele yetu ni kui-support Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Inafanya kazi vizuri sana. Nimekaa Bungeni, nimepita bajeti saba za Bunge, sijawahi kuona bajeti kama hii.

Mheshimiwa Spika, tusisahau kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli ndiyo bajeti yake ya pili. Ana miaka miwili tu. Hata sisi Majimboni tuna mambo mengi hatujayafanya ya kwetu peke yetu. Leo kuna mtu anafanya kana kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli leo ana mwaka wa kumi. Sijui kwa sababu amefanya mambo mengi, wanajisahau kwamba huyu mtu ameanza juzi tu. Sijui wamechanganyikiwa! Mimi hata sielewi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nawaonea huruma na kuwapa pole na kuwaambia bado nafasi tunazo mpaka 18 Juni tunafunga kupokea watu wa kutoka Upinzani. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, bajeti imekuwa nzuri, nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Mpango, lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba bajeti haiwezi kumaliza matatizo ya nchi nzima, hii bajeti ya pili tu. Tuendelee kuipongeza bajeti hii, watufanyie kazi kama walivyotuahidi kwa kasi yao ya Awamu ya Tano, lakini kila mwaka tutaongea watatukubalia kama walivyotukubalia safari hii.

Mheshimiwa Spika, tumeongea motor vehicle wamekubali, tumeongea sana kuhusu kurasimisha Wamachinga na Mama Lishe. Leo hii wamekuja kutuambia kwamba wanarasimisha sasa. Watajulikana sasa. Wamachinga na Mama Lishe watakuwa wanajulikana na sekta rasmi.

Mheshimiwa Spika, mimi kama Mbunge wa Tabora tuliongea sana kuhusu reli, leo tunaenda kwenye standard gauge. Naomba niongelee sasa kuhusu suala zima la viwanda. Mheshimiwa Dkt. Magufuli wakati anajinadi, akiomba kura alisema anataka Tanzania ya viwanda. Bajeti hii imetuonesha mwelekeo mzuri wa Tanzania ya viwanda. Hivi jamani tunataka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii wamefuta capital goods, wameifuta kabisa imebakia zero, wamefuta VAT kwenye vifaa vya uwekezaji, wamepunguza kodi ya mboga mboga na matunda, wameondoa kodi kwa mtu anatayekwenda kuuza mjini tani moja ya mazao na ndiyo wengi mama zetu hawa, ndiyo wengi baba zetu hawa; anajilimia ekari zake kumi anaenda kuuza mjini kila siku kidogo kidogo. Walikuwa
wanapambana na watu wa kuwadai kodi, sasa hivi hakuna. Jamani Mheshimiwa Rais afanye nini? Serikali ifanye nini? Hii ni bajeti yake ya pili tu, wamejitahidi sana jamani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.