Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, nami naomba niungane na wenzangu kuchangia mapendekezo ya bajeti ya 2017/2018 yaliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mpango. Kwanza kabisa nimpongeze sana kaka kwa umahiri mkubwa na utulivu aliotumia siku ya kuwasilisha taarifa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyotangulia kusema Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Shabiby kwamba wengi walikuwa wanasema hasikii, hachukui mapendekezo, amechukua mapendekezo na ametuleta taarifa ya mapendekezo ya bajeti yenye tija, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, nami niseme jamani, niliwahi kusema siku za nyuma, suala la madini linatuhusu watu wote lakini siku Wizara ya Madini inawasilisha hapa chini ya Waziri wa Viwanda na Biashara, aliyesoma taarifa ya Kambi ya Upinzani mdogo wangu Mnyika, alionesha kabisa kwamba Rais ameanza kutatua tatizo dogo badala ya kutatua tatizo kubwa la mikataba.

Mheshimiwa Spika, nami nikasema, anawezaje kuanza na hilo bila kuchunguza na kuona hivi kweli nikivamia mikataba hawa watu ni kweli wanaiba madini? Akaunda Tume ya kwanza, ikatupa taarifa. Tume ya pili, imetupa taarifa na wote tumesikia tangu 1998 mpaka 2017 tumepoteza shilingi trilioni 108. Ukienda kwenye bajeti yetu ya mwaka huu tunayotarajia ianze tarehe Mosi Julai, ni mara tatu ya bajeti tunayokwenda kuipitisha ya trilioni 31.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa, ninachokiona mimi kisiasa kwa sababu wenzetu walikuwa hawaoneshi kuunga mkono kazi anayofanya Rais ya kupambana na wizi wa rasilimali kwenye madini yanayotoroshwa, sasa wanatafuta kick kwa wananchi. Mimi niseme, wananchi ni waelewa, jana kwenye vyombo vya habari nilivyokuwa nasikia wapo wanachama wengi tu wa Vyama vya Upinzani wameamua kuachiaachia nyadhifa mbalimbali ili waweze sasa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niseme hivi ndugu zagu, haya mambo mazuri ambayo Mheshimiwa Rais anayafanya, hata kama msipotaka kuyaunga mkono, hata kama mtayapekuapekua mnavyotaka kupekua ninyi ili wananchi waone kwamba ninyi ndiyo bora na Rais wa Chama cha Mapinduzi siyo bora, nasema hamuwezi kupata tija katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie dhamira njema ya bajeti hii kwenye suala la viwanda. Tunafahamu kabisa kwamba Kigoma tuna kiwanda kimoja tu cha Uvinza Salt Mine. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kuna tatizo la wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya kazi siku za nyuma, tangu 1994 wakaachishwa bila kulipwa mafao yao.

Mheshimiwa Spika, tatizo hili ni la muda mrefu lakini lilifanyiwa kazi na Serikali na ikataka kujiridhisha ni kweli wafanyakazi wale wana haki za kulipwa? Suala hili likapelekwa mpaka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye naye akalifanyia kazi, akalipekua kisheria akaona kwamba wafanyakazi hawa wana haki kabisa za kisheria kulipwa mafao yao.

Mheshimiwa Spika, suala hili lipo mezani Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango, lina muda mrefu, lipo kwenye meza ya Katibu Mkuu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mpango, alifanyie kazi ili wafanyakazi hawa walipwe. Wapo ambao wameshatangulia mbele ya haki, familia zao zipo, wajane na watoto wapo, watapokea ile haki ambayo wazazi wao walikuwa wapokee.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hilo hilo la viwanda niseme pia tunapotaka tuwe na Serikali ya Viwanda na Nchi ya Viwanda, tusiangalie tu baadhi ya Ukanda ndiyo uwe na viwanda na Ukanda mwingine tusiwe na viwanda. Kwa hiyo, ninachoomba, tunatambua kabisa Kibondo pale tuna miwa mingi sana, tunaweza tukaanzisha Kiwanda cha Sukari. Uvinza tunaweza tukaanzisha Kiwanda cha kutengeneza Mafuta ya Mawese na mafuta ya mawese yanalika sana ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, ukienda Marekani kwenye super market zile unakuta palm oil ziko pale na ni very expensive, lakini sasa Serikali kama Serikali bado haijaweka jitihada za makusudi kuongeza tija kuanzisha viwanda katika Mkoa wetu wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la ujenzi wa reli ya kati na ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge. Kwanza niipongeze sana Serikali kwa hatua hii ya ujenzi huu lakini niombe, naona kila mkizungumza ujenzi wa reli mnazungumzia itatoka Tabora itaenda Mwanza. Sasa sisi Kigoma kama alivyosema Kaka yangu Mheshimiwa Nsanzugwako tunapakana na Zambia, DRC – Kongo na Burundi na mizigo mingi sana inatoka huko. Ukienda railway kwenye department ya transportation ukiwauliza watakwambia mabehewa mengi yanayokodishwa yanapeleka mizigo Kongo na Burundi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuombe, katika ujenzi wa reli ya kati, mtakapokuwa mmepata mkandarasi wa kuanzia Tabora kwenda Mwanza basi tupate mkandarasi mwingine wa kuanzia Tabora kwenda Kigoma. Tunafahamu kwamba sisi wananchi wa Kigoma huu ndiyo usafiri ambao tunauamini zaidi kuliko usafiri mwingine. Kwa hiyo, tunaomba mtufikirie katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili, reli inayojengwa kwa kiwango cha standard gauge inapita kwenye Jimbo langu la Uvinza. Niombe, tusiwe na mambo ya kushtukizana, pale ambapo mmeshapanga kabisa ifanyike feasibility study ya kujua reli hiyo itapita kwenye maeneo gani basi mtuambie mapema ili wananchi nao wawe na utayari wa kuipokea hii reli inayojengwa kwa kiwango cha standard gauge.

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.