Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote nami naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kufuatilia vipaumbele vilivyotolewa na Mheshimiwa Waziri, kwa maana ya utekelezaji wa vipaumbele eneo la ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi upande wa barabara, reli, usafiri wa anga, majini na umeme. Ukweli ni kwamba eneo hilo barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini na umeme vikifanyiwa kazi tutafika sehemu, kama hiyo haitoshi eneo lile la pili naambiwa

kwamba kipaumbele kingine ilikuwa ni kuhakikisha madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, mimi nina maslahi katika eneo la uchimbaji wa madini. Naomba nijikite kwenye Taarifa ya Kamati ukurasa wa 32, inaelezea kutoza kodi ya zuio ya asilimia tano ya bei ya kuuzia kwa wachimbaji wadogo ni hatua inayoongeza mapato stahiki ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa ule kwa maana ya Taarifa ya Kamati inasema hivi: “Kutoza kodi ya zuio ya asilimia tano ya bei ya kuuzia kwa wachimbaji wadogo ni hatua inayoongeza mapato stahiki ya Serikali, lakini inatafsiriwa kuwa wachimbaji wadogo watalipa mrabaha kwa asilimia tisa na inaweza kusababisha wachimbaji wadogo kufanya biashara haramu.”

Mheshimiwa Spika, lengo langu ni nini? Ikiwa tumekusudia kuwasaidia wachimbaji wadogo na ambacho nakiona sasa hivi, mkakati mkubwa wa Serikali kutoa ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo, lakini kwa kupitia vyombo vyake kama GST kufanya utafiti ili wachimbaji hawa waende kuchimba katika maeneo yenye tija. Sasa hayo yote ambayo ni nia njema ya Serikali kuyafanya, inapokuja suala la mrabaha kuwa kubwa kwa kiasi hicho, mimi napata tabu.

Mheshimiwa Spika, mchimbaji huyu mdogo na naomba Bunge lako lifahamu ningependa Waziri angeenda hata kwenye tafsiri, tunapozungumzia mchimbaji mdogo ni yupi? Maana mchimbaji mdogo ninayemfahamu mimi hana tofauti na Mmachinga mwingine wa kawaida. Mchimbaji mdogo ambaye anaweza akaenda porini ndani ya miezi mitatu hajapata hata gram moja ya dhahabu, huyo ndiye

mchimbaji mdogo ninayemfahamu. Mchimbaji mdogo anayetumia sururu na nyundo, labda kama tunamzungumzia mnunuaji wa madini, lakini kwa maana ya mchimbaji mdogo na Serikali hii imelenga kumsaidia mchimbaji huyo mdogo.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia habari ya mrabaha kwenda karibu asilimia tisa napata shida na ukizingatia leseni ya hekta moja ni 80,000, kama atakuwa na hekta kumi, maana yake ni laki nane ada ya leseni! Kwa hiyo eneo hilo naomba tuliangalie. Nalisema hilo kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa nafuatilia taarifa ya mtaalam mmoja, ameitaja Botswana na uchimbaji wa diamonds kwa maana ya almasi. Botswana sasa hivi pato la Botswana linatushinda Tanzania lakini wamejikita kwenye uchimbaji wa almasi tu. Nchi yangu nzuri Tanzania, mikakati mikubwa na katika hili nimshukuru Mheshimiwa Rais jitihada anazozifanya katika maeneo yote hayo yanayogusa machimbo, lakini niendelee kusema; ili tukafanane na watu kama Botswana, jitihada hizi za makusudi ziendelee kulenga maeneo mengine yote.

Mheshimiwa Spika, tunapomzungumzia mchimbaji mdogo akiwezeshwa vizuri makandokando mengine yakakaa pembeni mimi ninachofahamu uwekezaji wake haufanyi nje ya nchi, ataufanya Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwangu Katavi, majengo mengi mazuri ni yale yaliyofanywa na wachimbaji wadogo. Biashara nyingi kubwa ni zile zinazofanywa na wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu tuendelee kuliangalia eneo hilo kwa umakini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kufungwa kwa biashara. Kutoka Julai, 2016 hadi Machi, 2017 kuna biashara 7,277 zilifungwa. Nafarijika kwa maana ya taarifa ya Waziri imejikita kwenye kutafuta kujua na jitihada zifanyike ni kwa nini biashara hizo zilifungwa ingawa upande wa pili ametuambia kuna zaidi ya biashara 224,738 ambazo ni mpya. Kubwa ambalo

ningependa kuendelea kushauri, ndugu zetu wa TRA na wafanyabiashara tuendelee kutengeneza mahusiano sio uadui. Katika hili, Mheshimiwa Waziri nashukuru pale aliposema wenzetu wa TRA waendelee kufanya mahusiano shirikishi na wenzetu wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la usambazaji maji vijijini na mijini. Naona Mheshimiwa Waziri ametenga bilioni 188.4. Katika eneo hili niendelee kusema, pamoja na jitihada za Serikali kule kwangu kwa maana ya suala la maji na kila mtu hapa ameongelea suala la maji. Naomba Mheshimiwa Waziri, ufumbuzi wa muda mrefu, tuwekeze fedha kwenye kuyatoa maji ziwa Tanganyika, hiki ni chanzo cha uhakika, watu watapata maji ya kutosha na kelele hizi zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuhusu dawa na vifaa tiba ambapo niliona pale inazungumziwa habari ya bilioni 156.1. Tuseme yote tutakayoweza kusema na nishukuru pamoja na kwamba tunakwenda kusaidia hospitali kwa maana ya Jakaya Kikwete na maeneo mengine hayo, lakini tusipowekeza kwenye hospitali zetu za mikoa kwa maana ya vifaa tiba na madawa kasi ya watu kutoka huku mikoani kwenda kuvamia huko kwenye hospitali hizo nyingine itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Spika, naliona hilo kwa sababu gani? Kwa mfano, kule kwangu Katavi japo hospitali ile ya mkoa haijajengwa, utengaji wa fedha wa bilioni moja kwa kila mwaka kama lengo kweli tunataka tuhakikishe eneo hili la tiba watu wetu wanapata huko huko, maana yake hospitali ya mkoa ikiimarishwa, ikiwa na vifaa vyote, umerahisisha kazi, watu hawatakuja katika hizo hospitali nyingine kama Muhimbili na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, nami niungane mkono na wale wote kuhusu kusamehe kodi eneo la ufugaji pamoja na vyakula vya mifugo. Tutaiona tija katika eneo hilo, eneo la mifugo na kwa kweli tunasema ili mambo mengine yote yakae vizuri, tukiweza kukusanya mapato ya kutosha, maeneo mengine yote hayo yatakaa vizuri. Kwa hiyo, hapa tuliposamehe kodi katika eneo hilo la ufugaji pamoja na vyakula vya mifugo, naliona hilo limekaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ujenzi wa reli ya kati kwa maana ya kiwango cha standard gauge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kama nilivyosema mwanzo, naunga mkono hoja.