Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Waziri wa Fedha amesoma bajeti vizuri sana na nilikuwa namwangalia kwa makini hata maji alikuwa haombi na sauti yake imekwenda vizuri bila kupungua mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja, kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza, kwanza bajeti hii ni ya kihistoria, mimi nimekaa hapa miaka12 lakini ndio mara kwanza kusikia bajeti inayoeleweka kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kwa hiyo ni bajeti ya kihistoria.

Mheshimiwa Spika, hii ni mara ya kwanza sera za viwanda, uanzishaji wa viwanda na ku-favour viwanda imejikita moja kwa moja kwenye bajeti ya Serikali. Bajeti hii imetoa majibu ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, bajeti hii vilevile inaonesha ni jinsi gani National Development Plan ilivyokuwa incorporated kwenye bajeti hii ya mwaka huu pamoja na dira ya Taifa ya mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti hii pia imepunguzia wakulima na wafugaji ambao tunasema kwamba ni walala hoi wamepunguziwa kodi mbalimbali, hususani kwenye kilimo kwenye chakula kwenye madawa kwenye pembejeo mbalimbali, kwa hiyo ni bajeti ambayo inastahili kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaeleze tu Waheshimiwa Wabunge ambao ni wapya kwa maana ya kwamba wameingia wale asilimia 70 kwamba wasishangae sana kupata kusikia Wapinzani wanaendelea kupinga bajeti hii. Hata siku moja Wapinzani hawajawahi kuunga mkono isipokuwa na kumbuka Mzee John Momose Cheyo na Mzee Augustino Lyatonga Mrema ndio walikuwa Wapinzani wa kweli na ndio waliokuwa wanasema ukweli, kama Mheshimiwa wa Chama cha CUF ambaye ndio amemaliza sasa hivi muda mchache uliopita kuongea. Ameongea vizuri kiungwana, lakini wenzetu pale hawakumpigia hata makofi kwa sababu alikuwa anaongea vitu vya ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kusema kwamba Wapinzani kazi yao ni kupinga na sisi kazi yetu ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano kwa sababu sisi ndio tulioshinda uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wapinzani hawa kwa wale wasiowajua ni watu ambao wanabadilikabadilika, wamekuwa ni kinyonga. Kwa mfano, mwaka 2015 wakati Mheshimiwa Lowassa yuko Chama cha Mapinduzi walikuwa wanasema ni fisadi, alivyohamia kwao wakampa kugombea Urais, sasa si wanabadilikabadilika hao. Sasa hivi tunazungumzia mikataba mbalimbali lakini wasisahau kwamba Mheshimiwa Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kipindi hicho ndio alikuwa msimamizi wa shughuli za Serikali Bungeni alikuwa hapa wakati mikataba hiyo inaingiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii presha ambayo Wapinzani wanaiona ni kwa sababu wanajua kwamba 2020 tunapita bila kupingwa na viti vyao vitapungua.

TAARIFA ....

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa hiyo kwa sababu akiwa kama Waziri Mkuu alitakiwa ahakikishe kwamba inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ajenda ya Wapinzani kwa sasa walikuwa wanasema; maana sasa hivi wanasema kwamba bajeti hii ya Serikali haitekelezeki, lakini ajenda yao ya hapo nyuma, miezi miwili iliyopita walikuwa wanasema demokrasia imebanwa. Sasa hivi wamebadilika wanasema bajeti haitekelezeki, wakitoka hapo wataanza kusema tena demokrasia imebanwa, lakini embu waulize, sisi tangu

mwaka 2000 mpaka leo tumebadilisha Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi watatu, Mheshimiwa Mkapa, Mheshimiwa Kikwete na Mheshimiwa Magufuli, wao bado wako na Mbowe sijui mpaka miaka mingapi ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikimwona Tundu Lissu yeye ndio Mwenyekiti wa CHADEMA nitasema kweli mna demokrasia, lakini kama CHADEMA bado iko Moshi bado. (Makofi)

TAARIFA ....

Mheshimiwa Spika, Wapinzani wanasema kwamba Serikali itapata wapi trilioni 31.7 someni bajeti muone vyanzo vya mapato, kwa nini hamsomi?

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Tundu Lissu akumbuke kwamba tulikuwa chama kimoja cha Chama cha Mapinduzi peke yake. Pili, kujikosoa siyo udhaifu bali ni dalili ya kujiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shazia huwa inashona gunia, lakini shazia ili ishone gunia inatungwa uzi huku nyuma, sasa wasubiri 2020 tunawatunga uzi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kitu cha ajabu sana kuona kwamba Mheshimiwa Rais wetu, kwanza amefanya makubwa yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, nitayarudia tu halafu mtaona hamna hata mmoja atakayepiga makofi kule. Kwanza, ameondoa watumishi hewa zaidi ya 19,700. Pili, ameondoa watumishi wasio na vyeti 9,900; wanafunzi hewa walioondolewa kwenye Bodi ya Mikopo 3000; kugharamia elimu ya msingi hapo nyuma haikuwepo hii, elimu ya msingi sasa hivi inagharamiwa bila malipo, ukusanyaji wa kodi uliongezeka kuanzia bilioni 800 mpaka bilioni 1200 na zote hizo zinakwenda kwenye shughuli ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, pia ameweza kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, maamuzi haya yalifanyika mwaka 1973 lakini yamefanyika leo miezi 18 tayari Mheshimiwa Magufuli ameweza hiyo kazi. Ujenzi wa reli ya standard gauge haijawahi kutokea kwa muda mfupi namna hii. Kununua ndege mbili na zingine zinakuja na akina Mbowe ndio wanazipanda zinakuja, ni makubwa aliyofanya Mheshimiwa Jemedari wetu Dokta John Pombe Magufuli, kwa nini hampigi makofi? Hizi ndege mtapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tumeshinda kwa kukubaliana na Uganda kujenga bomba refu kutoka Hoima mpaka Tanga, Wakenya nao walitaka lakini walishindwa kwa sababu tuko vizuri. Vilevile meli mbili zimenunuliwa kule Nyasa na wanazitumia wananchi na tumefanikiwa kuzuia makinikia kwenda nje na tumeshajua hela tuliyokuwa tunaibiwa. Mambo yote haya aliyoyafanya Mheshimiwa Rais anastahili hongera, anastahili kuombewa na viongozi, anastahili kuombewa na Wakristo na Waislamu ili aweze kuwa na afya na maisha marefu ili aendelee kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, tunaomba kudhibiti kuwe na tracking system inayodhibiti magari yanayosafirisha mizigo, lakini kwenye ada ya registration kwa mara ya kwanza tunaomba angalau iongezeke laki moja kwa kila capacity ya engine kwa sababu hela iliyowekwa ya ongezeko la 50,000 ni hela ndogo sana, kwa sababu wana-register mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, hii ada ya magari iliyofutwa tunaomba ziongezeke Sh.50/= kwa kila lita ili tuweze kupeleka maji vijijini jamani, ndio maamuzi haya yatatusaidia.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.