Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kusema kwamba, mimi sio mtaalam wa maandiko matakatifu lakini kuna
mahali katika Biblia kunasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa, na nchi yetu inaangamia kwa sababu ya kukosa maarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, asubuhi umesema kwamba haya masuala ya madini yanahitaji semina. Hilo ni jambo muhimu sana, kwa sababu hoja hii inahitaji maarifa sana haiwezi ikajadiliwa sawasawa kwa hizi dakika tano au kumi.
Mheshimiwa Spika, nataka nijikite katika masuala ya madini kwa sababu ambazo ziko wazi kabisa. Kamati ya Rais ya Profesa Osoro ya jana na Kamati ya Profesa Mruma ya mwezi uliopita, siyo ripoti za kwanza kuzungumzia, kuchunguza matatizo ya kwenye sekta ya madini katika nchi hii, siyo za kwanza na Rais Magufuli siyo wa kwanza.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2002, Rais Mkapa aliunda Kamati iliyoongozwa na Jenerali Mboma inaitwa Kamati ya Mboma kuchunguza matatizo ya sekta ya madini, hasa madini ya vito vya thamani 2002. Mwaka 2004 Waziri Mkuu Fredrick Sumaye, Serikali ya Mkapa iliunda Kamati ya Dkt. Jonas Kipokola, kuchunguza matatizo ya sekta ya madini, taarifa yake ni ya Agosti, 2004.
Mheshimiwa Spika, mwaka uliofuata 2005 Rais Mkapa na Serikali yake waliunda Kamati ya Bukuku alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuchunguza matatizo ya sekta ya madini. Mwaka 2006 miezi michache baada ya Rais Kikwete kutawazwa kuwa Rais akaunda Kamati ya Lawrence Masha bahati nzuri nimekuja na taarifa yake hii hapa. Kamati ya Lawrence Masha kuchunguza Sheria za Madini, Sheria za Kodi, Sheria za Fedha, mikataba ya madini, kila kitu cha madini, taarifa hii hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2008 baada ya mgogoro wa Buzwagi hapa Bungeni, Rais Kikwete aliunda Kamati ya Jaji Mark Bomani hii hapa, Kamati ya Jaji Mark Bomani taarifa yake ni ya Aprili, 2008. Kamati ya Osoro na Kamati ya Profesa Mruma ni Kamati ya sita kuundwa kushughulikia masuala ya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimekuja na muhtasari wa Kamati ya Profesa Osoro ya jana hii hapa na kwa sababu nafahamu taarifa zote hizi za Kamati zingine, naweza nikawaambia Waheshimiwa Wabunge, hadidu za rejea za Kamati ya Mruma na Osoro ni zilezile zilizokuwa hadidu za rejea za Kipokola, za Bukuku, za Lawrance Masha na za Kamati ya Bomani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, matokeo yake, findings na recommendations ziko hapa kwa kiasi kikubwa ni findings na recommendations zilezile zilizokuwa kwa Bukuku, zilizokuwa kwa Kipokola, zilizokuwa kwa Masha, zilizokuwa kwa Bomani, hazijawahi kutekelezwa kwa sababu mnayoifahamu.
Mheshimiwa Spika, watu ambao wameuza madini ya nchi hii walipitisha sheria kwenye Bunge hili na ndio maana inashindikana na hii ya Dkt. Magufuli, nazungumza Mungu anasikia na watu wasikie, mtaniambia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika taarifa hii ya jana, wamependekeza watu fulani fulani washughulikiwe, Mawaziri, Makamishna, Mwanasheria Mkuu Bwana Chenge, akina Ngeleja, akina nani, naombeni niwaambieni kitu Waheshimiwa Wabunge ili muwe na maarifa. Mtu wa kwanza kusaini mikataba ya madini na leseni za madini tarehe 5 Agosti, 1994, Meja Jakaya Mrisho Kikwete, leseni ya Bulyanhulu hii inayopigiwa kelele leo, Leseni ya Bulyanghulu ya tarehe 5 Agosti, 1994 ilisainiwa na Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, hakuwa na kinga ya Urais wakati ule, hana kinga ya Urais leo kuhusiana na masuala aliyoyafanya wakati hajawa Rais. Hana! Alisaini leseni siyo ya Bulyanhulu peke yake, pia ya Nzega na ya Geita. Golden Pride - Nzega na Geita Gold Mine zina sahihi ya Kikwete, anaponaje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mapendekezo haya anaponaje? Kama mnataka kweli kushughulikia watu walioshiriki mambo haya, mbona mnachagua chagua? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hizi leseni na hizi sheria tatizo kubwa tangu mwaka 1999 wenye kujua tumesema, tatizo kubwa ni sheria za Tanzania. Sisi ni wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa kulinda uwekezaji (The MIGA Convention). Tumesaini mikataba na nchi moja moja zenye wawekezaji Tanzania, nchi 26, mikataba ya kulinda Wawekezaji hawa. Tumetunga Sheria ya Madini yenyewe, Sheria za Kodi za mwaka 1997, Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997. Hizi za 1997 zilipitishwa siku moja tarehe 26 Machi, under Certificate of Urgency. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama kuna mchango utakaoutoa kama Spika na utakumbukwa, upige marufuku hii habari ya Certificate of Urgency kwenye utungaji sheria, inatuletea mabomu. Sheria za Gesi Asilia na mafuta mlizotufukuza hapa mkazipitisha ni mabomu matupu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma hizo takwimu mlizoambiwa na Profesa Mruma na Profesa Osoro za madini ambayo yameondoka. Mimi sitasema sana, nawaombeni kama mnaweza, mlinganishe takwimu za utajiri wa madini zinavyozungumzwa kwenye Kamati ya Bomani na mlinganishe na utajiri unaozungumzwa kwenye Kamati ya Profesa Osoro, halafu mniambie nani ni mwongo kati ya hizo mbili.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, nashukuru.