Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti yetu muhimu sana kwa ajili ya Watanzania. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuumba ametupa uhai na uzima leo tumekuwa hai na tunaendelea na wale wote wanaofunga nawatakia funga njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Rais wa Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Watanzania. Leo Watanzania wameona jitihada za Mheshimiwa Rais za kutetea maslahi ya Watanzania. Naomba Watanzania wote tumuunge mkono Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Vilevile naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kuwa makini sana na kuchukua yale mahitaji yanayotakiwa na Wabunge na mnachukua mawazo, mmechukua mambo mengi kwa Wabunge ambayo mmeyafanyia kazi na mmeweka kwenye bajeti, naomba niwapongeze sana. Wananchi wote wanaunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. Ina maana leo kama kungekuwa kuna uchaguzi CCM ingepata asilimia mia moja. (Vigelegele/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti ya Serikali kwa asilimia mia moja kwa sababu bajeti hii imeeondoa kero za wananchi kwa asilimia mia moja. Leo hii mimi mtu wa Mpanda ukiniambia bajeti haijawasaidia wananchi siwezi kukuelewa kwa sababu nilikuwa najua kero za wanachi wa Mpanda hususani Mkoa wa Katavi. Mkoa wa Katavi ni wa kilimo, leo hii tani moja yule mfanyabiashara mdogo mdogo anasafirisha mazao yake bure ina maana kuwa bajeti hii imemkomboa mfanyabiashara mdogo na mkulima nayetoa mahindi yake Mlele, Mpimwe magunia kumi anayaleta mjini anakuja kuyauza, mmemkomboa kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze sana Serikali kwa hilo ndiyo maana na wenyewe wameiunga mkono asilimia 100 bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niipongeze Serikali kwa kuanza kujenga standard gauge kwa sababu inafika Mkoa wangu wa Katavi. Reli hii itaturahisishia sana sisi wa kanda hii kwa sababu usafiri wetu mkubwa ni reli ya kati. Sasa kwenye reli ya kati mnatupitishia sasa reli ya kisasa ambayo ni standard gauge, naomba niipongeze sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niipongeze Serikali kwa kununua ndege mbili ambazo zipo tayari na vilevile mmenunua tena ndege zingine tatu ambazo zitasaidia na uchumi wa nchi yetu utaongezeka mara mbili, tatu. Naomba sana niipongeze Serikali, leo ni kuipongeza kwa sababu haijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niipongeze Serikali kwa kufuta leseni za magari. Leo wananchi wengi walikuwa wame-park magari yao, walikuwa hawana pesa za kulipia lakini mmewaondolea mzigo magari yote sasa yatatembea barabarani. Naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa mliyoifanya kwa kuwaondolea adha wananchi kwani sasa watatembea na magari yao na watafanya biashara. Wengi walipaki magari, walikosa hela za kulipia lakini leo watatembeza magari, wataenda kufanya shughuli zao mbalimbali ili uchumi wao uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na vilevile naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya kupeleka fedha za tozo ya shilingi 40 kwenye maji itakayotoka kwenye dizeli, petroli na mafuta ya taa. Najua kabisa hii pesa ikienda Hazina siyo lazima ifanye jambo lingine inaweza kupendekeza hizi pesa shilingi 40,000 zikaenda kwenye maji kwa sababu akina mama wengi sana wanateseka na ukosefu wa maji. Naomba hii tozo ya shilingi 40,000…
MWENYEKITI: Mheshimiwa ni shilingi 40.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shilingi 40, si unajua tena, raha imezidi kutokana na bajeti nzuri sana, nzuri mno. Sasa hii shilingi 40 itaenda kwenye maji ili wananchi waweze kutatuliwa matatizo mazito tuliyonayo. Naomba Serikali, najua Waziri upo makini sana tunaomba hii tozo ya shilingi 40 iende kwenye maji ili wananchi sasa waweze kupata unafuu kwa sababu vijijini akina mama wanapata taabu sana kwa ajili ya maji. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mambo mengi yanayofanyika katika Serikali hii ni makubwa na mazuri sana. Naomba tuendelee kuiunga mkono kwa sababu mnaiona jinsi gani inavyofanya kazi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa kilimo. Mkoa wa Katavi sisi ni wakulima, naomba sasa tuweke mikakati mizuri, wale wananchi wa Katavi waweze kupelekewa mbolea kwa ukaribu zaidi na mapema ili kilimo chao kiwe na tija. Naomba Serikali yangu sikivu sasa hivi twende kwenye mbolea tuweke mikakati ya mbolea kwa mikoa yote inayolima ya Katavi, Rukwa, Mbeya na Ruvuma. Naomba Serikali yangu mbolea iwe kipaumbele, wapelekewe mbolea mapema na ukizingatia Mkoa wa Kigoma wenyewe wanalima mapema basi iwekwe mikakati mizuri ya kupelekea mbolea wakulima mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mkoa wangu wa Katavi tuna shida sana ya maji. Tuna Ziwa Tanganyika ambalo lina kina kirefu, tukilitumia ziwa hili nafikiri Mkoa wa Katavi matatizo ya maji yataisha kabisa. Naomba Serikali yangu sikivu tutumie Ziwa Tanganyika. Tumepata mafanikio makubwa sana kwenye Ziwa Victoria, tumeilisha Mwanza, Shinyanga na sasa tunaelekea kuilisha Tabora na bado hapo hapo hata watu wa Mkoa wa Singida wanatamani maji ya Ziwa Victoria yafike. Tukiilisha maji Mkoa wa Katavi kupitia Ziwa Tanganyika tutakuwa tumeondoa kero kubwa sana ya maji kwa sababu yale maji yatapita kwenye maeneo mengi na kwenye vijiji vingi na hatma yake maji yatakuwa mengi katika Mkoa wetu wa Katavi na shida ya maji itakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja asilimia mia moja bajeti hii ya historia ya Chama cha Mapinduzi. Chama cha Mapinduzi tuna raha sana. Unajua ukifanya kitu kizuri lazima ujisifie, naunga mkono hoja asilimia mia moja, ahsante sana.