Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niongee au nichangie katika Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuwapongeza sana Wizara hii ya Nishati na Madini na niwakumbushe wananchi na Wabunge wenzangu humu jinsi gani tulikuwa miaka mitatu, mitano, sita iliyopita wakati ambapo tulikuwa na mgawo, siku mbili au siku tatu hakuna umeme na hatukulalamika; leo mgawo umekuwa historia hakuna mtu anayepongeza? Si tuwapongeze hawa wenzetu kwamba, wamefanya kazi kubwa sana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nyuma ya mafanikio yote haya yupo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye amekuwa anatoa miongozo ya kulipa hela chungu nzima kwa mfano Kinyerezi Phase II ilisimama kwa sababu haikuwa na hela. Hela nyingi zimeingizwa pale ili mradi ule uanze, haya ni mafanikio makubwa sana. Vile vile iko miradi ya Rusumo huko, miradi mingine ya gesi inayoleta umeme ambao tunautumia majumbani na viwandani; haya ni mafanikio ambayo Wizara hii inatakiwa ipongezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, niseme ukweli kwamba mwenzangu, rafiki yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo amepata ajali ya kisiasa na amemwacha hapa Mheshimiwa Engineer Merdad. Bado Wizara hii imewasilishwa vizuri na mwenzangu Mheshimiwa Mwijage hapa leo, tumefurahi kwa yote aliyoyasema na kama alivyosema yeye Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Merdad ameziba pengo, amevaa viatu vya Mheshimiwa Profesa Muhongo. Naipongeza Wizara hii kwa mambo hayo makubwa iliyoyafanya, lakini hasa kusimamia miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongea kwangu leo nitaongelea pia, suala la REA ambao ni mradi mkubwa unaoendelea, lakini vile vile ningependa nichukue nafasi hii kuongelea mambo ambayo yametokea hivi karibuni ingawa yameongelewa pia, lakini suala la makinikia haliwezi kupitwa bila kusemewa kwa undani na kwa ukweli wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunapenda ku-quote au kunukuu maneno katika lugha nyingine, mimi ningependa kunukuu leo maneno kutoka lugha yetu ya Kinyamwezi na maneno hayo ni kwamba, “Mradi Kuyile” yaani mradi tunakwenda, “Nabhagemanyile” nilikuwa najua na kudharau yani “Kubyeda”.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo fulani akifanya kiongozi wa nje ya nchi, hasa kutoka kwa wakubwa hawa, kama container hili moja lingekamatwa kule Malaysia au Singapore au Marekani, basi watu hapo wangeandika na kusifia sana. Tumekamata makontena 277 watu wanaona business as usual, mradi kuyile, mradi tunakwenda, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yaliyokuwemo katika mchanga huu wa makinikia umetia hasara sawasawa na bajeti ya nchi hii kwa miaka mitano. Si chini ya miaka mitano, makontena haya kwa miaka 17, tungeweza kupata mali iliyotoka mle ndani tungeweza kuendesha nchi hii kwa miaka mitano, bajeti ya nchi nzima. Sasa Mheshimiwa Rais amefanya juhudi kubwa sana, ametimiza wajibu wake wa kukamata makontena haya, lakini bado naona tayari kunakuwa na watu ambao wameanza kudharau suala hili, jambo hili si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna juhudi kubwa sana ya waliokamatwa sasa kujaribu kufunika jambo hili na kuna watu wanasema tutashitakiwa, mimi nashindwa kuelewa! Umuibie mtu na ushahidi upo halafu ukamshtaki! Sielewi kama kutakuwa na sheria, au sijui watatumia njia gani ya kutushitaki sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napata tabu sana ninapoona wenzetu wanaanza kuongelea, kwamba ni tatizo la mikataba, kwa hiyo mikataba hii ingeanza kwanza kuchanganuliwa kabla ya kushughulikia makontena. Hata hivyo, ijulikane kwamba ili uuchambue upya mkataba lazima mkataba uwe na makosa, sasa makosa yameonekana, kumbe katika mkataba huu watu wanaiba, sasa huu wizi ndio ushahidi wa kuweza kuchambua mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani kwamba, sisi wote humu ndani ya Bunge hili tunao wajibu wa kutetea maslahi ya watu waliotuleta humu ndani, nao ni wananchi, ili wananchi hawa wasiibiwe, lakini vile vile wananchi hawa wasidhulumiwe na wananchi hawa wajione wako salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilinukuu maneno ya Kinyamwezi, lakini sasa ninukuu maneno ya Kiyunani, “Delegatus Non Protest Delegae”; mtu aliyepewa jukumu, wajibu wa dhamana hana haki ya kumkabidhi mtu mwingine tena wajibu huo aliokabidhiwa. Wajibu wetu sote humu ndani ni kuungana kwa pamoja kutetea wananchi waliotuleta humu ndani; leo inakuwaje sisi Wabunge tunaanza kubadilika na kutetea mambo ambayo hayana ukweli ndani yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Wataalam, wamechambua mchanga ule na kutoa majibu; je, hatuaminiani? Wabunge humu ndani wanaanza kuongelea kwamba, inawezekana ule mchanga ni hadithi ambayo wanaicheza ngoma ya walioibiwa. Ukweli ni kwamba kuhusu mchanga ule tufuate maelekezo na taarifa iliyotolewa na wataalam wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye miradi ya REA. Pamoja na mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza na ya pili ya REA kumekuwa na udhaifu mdogo mdogo uliotokana na utendaji, hasa uwajibikaji wa watu fulani katika mradi ule, wameruka vijiji fulani. Kwa mfano jimboni kwangu vijiji vikubwa ambavyo vina shule, vina zahanati, vina vituo vya afya vimerukwa! Bahati nzuri nilimwona Mheshimiwa Muhongo kabla hajaacha kuwa Waziri na tukakutana pia na mkandarasi huyu, nina imani tuliyoongea yatakuwa sahihi kwamba, watafanya variance ya mabadiliko kidogo ya mkataba kwa aslimia 15 ambapo Vijiji vya Majengo, Ikongolo, Kanyenye, Nzubuka na Kituo cha Upuge vitapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa anithibitishie kwamba, waliyoniambia viongozi wa REA kwamba, maeneo haya yatapata umeme, yapate umeme. Maana itakuwa jambo la ajabu bahati nzuri au mbaya katika vijiji hivyo ndiko mimi natoka, sasa watu wamekuwa wanasema ahaa, Mbunge huyu mnaona hafai, hata umeme kwake hakuna! Hayumo kwenye REA Phase Two na Phase Three.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo litaleta matatizo makubwa sana ya kisiasa, nawaombeni sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha awe ameongea na watu wa REA ili waingize Vijiji vya Upuge kwenye kituo kimoja cha afya kiko pekee, Vijiji vya Majengo, Kanyenye, Ikongolo, Nzubuka na Kiwembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengine katika Wizara hii ambayo ni mazuri sana, lakini mambo madogomadogo haya yanaipaka matope Wizara na ionekane kama haifanyi kazi. La sivyo, Wizara hii imefanya kazi kubwa sana kutafuta gesi, kusimamia upatikanaji wa gesi, kusimamia uunganishaji wa bomba kutoka Uganda kuja Tanga, kusimamia mambo mengi, gesi kutoka kule Mtwara kuja Dar-es-Salaam na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema sana, naomba niwaachie na wenzangu. Naunga mkono hoja moja kwa moja.