Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nianze kuwapongeza rika langu, ndugu zangu wote, ma-korianga popote walipo nchini kwa kufikia hatua ya muhimu ya maisha yao, tunakwenda kukabidhi madaraka. Hata hivyo, niwatakie heri wenzetu wale wa Kimnyak, Irkimayana kwa namna ambavyo wanapokea madaraka kutoka kwetu kwa mila za kimasaii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimshukuru kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kufika jimboni kwangu na kuniahidi jambo moja, kwamba VAT ya asilimia 18 inayotozwa kwa mnunuzi wa tanzanite kwenye soko huria itaondolewa. Nina imani kwamba Waziri anapokuja kuhitimisha hii VAT ataiongelea. Ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike pia kuhusu ruzuku, hamjatoa kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Mererani hususani akinamama ambao na wenyewe wana wawakilishi wao kila mahali wanajaribu kujipambanua katika suala la kiuchumi lakini wamefanya application na Wizara yenu haijatoa hata ruzuku moja kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niingie kwenye suala la tanzanite. Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo na wewe unaifahamu imeweka bayana kwamba madini ya vito yatachimbwa na wazawa lakini leseni yoyote itakayotoka haitazidi square kilometa moja. Kwenye application iliyofanyika 2013 application ya leseni HQP26116 ya Tanzanite One iliiomba Wizara kutoa leseni ya madini, wao wenyewe wamempa square kilometa 7.6 kinyume na sheria. Kuna majadiliano makubwa ya kisheria kati ya Wizara yako na watumishi, wengine wakikataa lakini kulikuwepo na shinikizo mwaka 2013 na ushahidi huo upo naomba niulete acheni kufisidi nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu mmemwelewa Mheshimiwa Tundu Lissu vibaya. Ninyi mnafahamu kesi ya Dowans tumepoteza kama nchi na kesi ya Richmond tumepoteza kama nchi. Mheshimiwa Rais, Wabunge wa Upinzani hawakatai kwamba kuna madudu nchi hii kuhusu mikataba lakini nendeni kwa style ambayo nchi haitapata hasara kwa baadaye. Eleweni hivyo Wabunge wenzangu wa CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Tanzanite One ilipewa leseni kinyume na masharti ya sheria na aliyehusika katika hilo, aliyesaini leseni hiyo ni ndugu Engineer Ally Samaje na anajulikana yupo, naomba Serikali ifuatilie. Walichokifanya ndugu zangu, kwa sababu sheria ya 2010 inaruhusu yeyote anayechimba mable na graphite aruhusiwe kupewa takribani square kilometa 10; wakasema kwenye leseni yao hiyo wana–apply mable na graphite na si tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ukienda kwenye documentation zote Kampuni ya Tanzanite One haijawahi hata siku moja kusafirisha nje mable na graphite. Ujanja huu ulitumika na ninyi mnatakiwa mwelewe nchi yetu inavyoibiwa. Mtu anaomba leseni ya kitu kingine lakini anachimba kitu kingine, ipo kwenye documentation. Anaomba leseni ya mable na graphite lakini anakwenda kuchimba tanzanite. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nchi yetu inamalizwa; tusiposimama kama wananchi wanaoipenda nchi hii, tutaimaliza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kampuni iliyoingia mkataba na Serikali 2013/2014 inaitwa Sky Associate, sasa huyo Sky Associate ni nani? Ni kampuni iliyosajiliwa mahali panaitwa Virgin Island ambayo inafanya kazi zake Hong Kong. Kampuni hii haipo Tanzania na haijasajiliwa Tanzania. Mheshimiwa Ngonyani anafahamu kwa sababu taarifa aliyotoa kwa umma wakati yupo Wizarani pale; Mheshimiwa Ngonyani aliwaambia watu kwamba ndugu Faisal Juma Shabash ambaye ni Mtanzania anamiliki asilimia 25, alisema Hussein Gonga anamiliki asilimia 35, Ridhiwan Urah, si huyu Ridhiwan anamiliki asilimia 40. Hakuna popote, si TIC, sio kwenye usajili wetu wa makampuni Tanzania, watu hawa wanaonekana. Hii kampuni ni ya kitapeli na Serikali inawalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu lingine, hawa jamaa wanafanya minada. Kampuni hii ya Tanzanite One imeuzwa kwenda Sky Associate kwa dola milioni tano ya kulipana kwa mafungu. Minada miwili waliyofanya Agosti na Februari wameuza takribani dola milioni saba…

T A A R I F A . . . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili, nimwombe Mheshimiwa Rais atumie mamlaka yake leo asimamishe uzalishaji wa kampuni hiyo, lakini na Mheshimiwa Ngonyani pia ashughulikiwe. Pia niombe STAMICO inayohusika kufisadi nchi yetu, wewe tulia…

T A A R I F A. . . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niombe tu kwa heshima kwamba sipokei taarifa hiyo, lakini kwa sababu nimeomba Tume ya Rais iundwe na haya yote anayoyasema yataonekana kwa sababu kwa kawaida na yeye atahojiwa; haya yote atakuja kuyaeleza kwamba, je, kampuni hii ni ya Kitanzania au sio ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea kitu kimoja, akanushe mtu yeyote hisa hizo zimeuzwa kwa dola milioni tano tu, lakini kwa masoko ya Agosti 2016 na Februari watu hawa wameuza madini kwa milioni saba, tayari almost bilioni 16 na capital gain hawalipi, ndugu zangu nchi yetu inaibiwa sana. Hata hivyo, Kampuni ya Tanzanite One Limited imekuwa ikitoa taarifa za uongo kwa mbia mwenza, yaani STAMICO tangu alivyoanza uzalishaji wa tanzanite hapa nchini. Kwa mfano, kuanzia Julai 13 hadi Julai 16, STAMICO ameripoti mauzo ya jumla ya dola za kimarekani milioni 16 wakati kiukweli ni milioni 17, tayari kuna dola almost kati ya milioni moja mpaka laki kadhaa zinaibiwa, ndiyo maana tunasema watu hawa wanaiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hilo halitoshi, minada inayoandaliwa yote, nilimwandikia barua Kamishna Msaidizi wa Madini pale Arusha, ndugu Ali Adam, tarehe 20 mwezi wa pili 2017, kwamba ninaomba uniambie tenda ya kwanza na tenda ya pili waliyouziwa madini yetu kwenye tenda ni akina nani? Alichonijibu officially, tarehe 24 Februari, ipo kwenye documentation na barua imegongwa; wameuziwa Gemoro Company Limited, kampuni ya India, Viber Global Limited Kampuni ya India, Kala Jewels Kampuni ya India, Shree Narayan Gems ya India, hiyo ni tenda ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tenda ya pili ameuziwa Arwi International ya India, Shree Narayan ya India na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge watu hawa wote wana mahusiano ya karibu na kampuni ambayo imesajiliwa Virgin Island inayofanya kazi zake Hong Kong. Waheshimiwa Wabunge nchi yetu inaibiwa, ni muda muafaka madini haya ya tanzanite wengi wenu hamyafahamu, ni madini ambayo yangeweza kubadilisha maisha ya watu wa Simanjiro lakini yangeweza kubadilisha maisha ya watanzania wengi. Ninaomba kwa ukubwa wetu tuingilie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)