Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii adhimu kuwatakia kheri na baraka Waislamu wenzangu katika Mfungo huu Mtukufu wa Mwezi wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nianze na utangulizi ufuatao. Tarehe 25 Oktoba, 2015, Watanzania walifanya maamuzi ya kumchangua Rais, John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunakubaliana hilo halina hoja wala dawa, ni jambo lilitokea na sisi tunakubali.

Hata hivyo, Watanzania hao hao sambamba na kumchagua Rais waliwachagua Wabunge hawa kuwa ndiyo kioo cha kuisimamia, kuielekeza na kuishauri Serikali yetu. Kwa hivyo, tulichaguliwa pamoja naye Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, ana wajibu mkubwa sana kutusikiliza vizuri sana na kupitia Waziri Mkuu mimi ningependa tu mpelekee salamu moja Mheshimiwa Rais ya upendo, kwamba tulichaguliwa pamoja naye kwa hivyo ayape uzito sana tunayoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uchaguzi ule kuna wenzetu wengine walitukimbia hapa, waliondoka wakati mbaya sana, kuna wengine walikwenda Rwanda kuona dada wenye shingo refu kule, lakini leo wamerudi hapa Mheshimiwa Rais ndiyo anawafanya watu wa karibu sana kuwaalika Ikulu kila linapotokea jambo, hawafai hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ule wa mapambano ilikuwa tukae pamoja kuivusha nchi yetu katika uchaguzi ule wapo tuliokuwa naye na hatutamuacha, aendelee kushirikiana na sisi, aachane na wale wengine wababaishaji, hawatamsaidia. Mheshimiwa mpe hiyo salamu, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie habari ya wafanyabiashara, inaonekana Waziri Mkuu hukunifahamu lakini nitakuja kwenye meza yako nikupe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara si maadui, wafanyabiashara wa Tanzania ni watu tunaowategemea sana katika kuleta pato la nchi hii. Katika nyendo tunazokwenda nazo hivi sasa kauli zetu, kauli za viongozi haziashirii wema kujenga ukaribu na wafanyabiashara badala yake tunajenga uhasama na chuki na wafanyabiashara jambo ambalo halitatuletea tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kuvuna maziwa mengi katika ng’ombe lazima tumlishe vizuri, usitegemee ng’ombe usiyemlisha utapata mavuno mazuri, hutapata maziwa yanayostahiki. Kwa hiyo, tunatakiwa tuangalie, hivi sasa tunakuwa na tabia hasa Mawaziri wetu mnakuwa na ile kitu kuona mseme yale yanayompendeza Mheshimiwa lakini hamtaki kumwambia hali halisi tuliyonayo katika nchi. Sasa hivi Kariakoo mlango wa biashara ulikuwa unatoa kilemba mpaka shilingi milioni 30 kuupata kabla ya kulipa kodi lakini sasa hivi wafanyabiashara wenye majumba wamekosa kabisa wafanyabiashara wa kukodisha fremu za milango. Hiyo ni ashirio moja kwamba biashara inakokwenda sio kuzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna wajibu wa kukaa nao wafanyabiashara tukaona ni kipi kinachowakwaza. Jana alisema mwenzangu mmoja hapa hamtangazi tena mapato ya kila mwezi lakini iko sababu kwa nini hamtangazi. Tuliwaambia mwanzo mnachokusanya ni arrears zinazotokana na malimbikizo ya nyuma zikimalizika hizi makusanyo hayo tunayojidai nayo yatakuwa hayapo tena na ndicho kinachotokea sasa. Likija suala la mapato Taifa linakuangalia wewe Waziri nakushauri hebu tukae na wafanyabiashara tuangalie yanayowakwaza ili tupate njia ya kutokea. Sasa hivi tumekwama na tunapoelekea ni kubaya zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nataka niseme habari ya kodi wanayotozwa watu wenye magari mabovu, jana mwenzangu mmoja alizungumzia na mimi nataka kulirudia. Elimu ni kitu muhimu, Watanzania unapokuja mfumo mpya wa kodi au jambo jipya ni lazima kwanza waelekezwe. Mfano mtu alikuwa na gari amenunua limekufa miaka 10 nyuma lakini leo akinunua kigari chake kingine akienda TRA anaambiwa gari hii uilipie kodi zote za miaka 10, hii kweli ni haki? Haya mambo yapo na sasa hivi imekuwa ni shida kubwa sana kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza Mheshimiwa Waziri, ili gari litembee lazima lipate mafuta, tuhamishie hayo mengine hata kama ni percent ndogo iwekwe kwenye mafuta kwa sababu gari linalotembea litakuwa linatozwa pale gari linapotumika, gari likifa itakuwa hakuna tena kesi baina ya raia na Serikali. Sasa inakuwa tunajenga uadui, wananchi wanaona TRA kama maadui wakubwa na siyo hivyo, nchi za wenzetu wafanyabiashara ni marafiki wakubwa na vyombo vinavyokusanya kodi, kwa nini sisi tunakuwa mahasimu wakubwa? Ni kwa sababu nakuwa na sheria za mwendo kasi, halichachi, ni pale mnapoamka mkaamua kufanya mnafanya, haiwezekani. Lazima tuwaandae watu wetu linapotokea badiliko la kisheria ili watu wajiandae na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie misaada ya nje ya nchi ya wahisani. Hakuna asiyejua kwamba nchi yetu misaada tuliyokuwa tukipata toka Millennium Challenge Account imekatika na haikukatika kwa bahati mbaya wameacha kutusaidia kwa sababu walizoziainisha mapema. Waliainisha mambo mawili wakisema wao hawatakuwa tayari kuendelea na ufadhili kwamba mambo haya ndani ya nchi hayakushughulikiwa nayo ni suala la uchaguzi wa Zanzibar na suala la Sheria ya Mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mawili wahisani walitueleza wazi na bahati nzuri sana Waziri wa Mambo ya Nje nilimsikia kwa masikio yangu akisema kwamba; “haya ni mambo madogo, tutayashughulikia haraka na ufumbuzi utapatikana” yaah, ndiyo alivyozungumza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwa kauli ile murua, mwanana, burudaa wal asilia, jambo hili litapatiwa kweli ufumbuzi. Niwaulize wenzangu mmeshindwa nini? Utawala wa JK tulikuwa na changamoto za kiuchaguzi lakini watu walizungumza wakafikia makubaliano na nchi ikaenda, nchi haikuzuiliwa misaada, tatizo nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu sisi lililokuwa kubwa lipi ambalo halizungumziki. Watanzania ni wamoja, linakuja jambo, msaada ule wa Millennium Challenge ulikuwa ukisaidia sana umeme vijijini, leo sababu ya Wazanzibar milioni moja na nusu na Watanzania milioni 50 wanakosa msaada ule muhimu kwa upande wa Tanzania Bara, kwa jambo ambalo tungeweza kukaa kuzungumza kwani kubwa lipi sisi tunatoa moto kwenye midomo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno asali tunatoa midomoni mwetu, kwa nini nyie msitoe maziwa tukawa karibu, tatizo nini? Msaada ule bado ni muhimu, kweli kuomba ni aibu, lakini ukiwa huna omba kuliko kuiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nasema bado tuna haja na Waheshimiwa Wabunge nawasikia kila siku hapa likija suala la umeme vijijini kila mmoja ananyanyuka REA, REA, hakuna REA ile pesa haiko, mimi nawaambia, tusidanganyane. Ile pesa kubwa iliyokuwa ikitupa kiburi kuendeleza miradi ya REA ya umeme vijijini imekatika kwa sababu ya mambo mawili tu, Sheria ya Mtandao na Uchaguzi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumza uchaguzi wa Zanzibar wengine mnakasirika na huu Mwezi wa Ramadhani sipaswi kumkwaza mtu, nasema kwa lugha nyepesi sana kwa lugha ya maziwa na asali tukaeni tujadili tuone umuhimu wa kuzishawishi nchi za European Union kurudisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)