Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nianze kuzungumzia suala la Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mdhibiti na Mkaguzi huyu amekuwa akifanya kazi ya kukagua fedha za Serikali miaka nenda rudi, nilitaka kujua ukaguzi huu unalenga nini? Kama ukaguzi unafanyika na wanaofanya ubadhirifu wa fedha za umma hakuna hatua inayochukuliwa kuna sababu gani ya CAG kuendelea kukagua fedha. Kila mwaka tunaletewa taarifa kuna Halmashauri zenye hati chafu, sijui ripoti chafu lakini hakuna kinachofanyika. CAG ana kazi gani kama ripoti yake haiwezi kuwa na impact? Tunatenga fedha CAG afanye ukaguzi lakini akimaliza kukagua hatuoni madhara au hatuoni impact ya ukaguzi wake kwenye nchi hii. Lazima ifike hatua baada ya ukaguzi what next, nini kifanyike juu ya ripoti ile kwa ukaguzi mbovu uliopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ukurasa wa 34 ambao Waziri amesema Ofisi ya Mdhibiti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali ndiye yenye jukumu la kufanya ukaguzi wa fedha wa hesabu za Serikali. Sasa nataka kuuliza, nimepata taarifa kwamba CAG anakagua fedha za vyama vya wafanyakazi. CAG ameanza kukagua Chama cha Walimu Tanzania (CWT) chama ambacho kimekuwepo tangu mwaka 1993 hakijawahi kukaguliwa na CAG na kule hakuna ruzuku ya Serikali, hakuna fedha ya Serikali yoyote iliyokwenda kule anakwenda kutafuta nini kule Chama cha Walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi inanipa wakati mgumu sana. Tena vyama viko zaidi ya kumi na mbili, kumi na tatu ameendaje Chama cha Walimu kukagua ambapo vyama vya wafanyakazi vinakaguliwa kwa mujibu wa sheria, vinakaguliwa na Mkaguzi wa Vyama vya Wafanyakazi anayetambulika kwa Msajili ya Vyama vya Wafanyakazi. Huyu CAG amekwenda kufanya nini, kama siyo kuna jambo fulani mtu anafikiri limefanyika anamtuma CAG kwenda kukagua fedha ambazo zimekwisha kaguliwa na ripoti ya vyama vya wafanyakazi na fedha zote zinakaguliwa mwezi wa tatu na taarifa lazima ifike kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi si zaidi ya tarehe 30 mwezi wa tatu. Leo CAG yupo Chama cha Walimu anakagua fedha. Naomba kujua hilo nipate majibu anatafuta nini kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Wazabuni kutolipwa. Serikali lazima ifike mahali ifahamu kwamba uzabuni ni biashara. Wazabuni ni wafanyabiashara! Kama Serikali inawakopa wazabuni, inashindwa kuwafanya waendelee ku-move na biashara zao ni makosa makubwa. Sambamba na hilo wapo watu wali-supply mbolea, pembejeo, waliosambaza pembejeo hapa nchini mpaka leo hajalipwa, wamefilisiwa na mabenki na wengine wamekufa kwa sababu ya kudaiwa fedha za pembejeo na benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakopaje watu binafsi? Nani mwenye capacity kati ya Serikali na mtu binafsi? Ifike hatua Serikali iangalie nani wa kumkopa na nani isimkope. Mnarudisha nyuma uchumi wa wananchi wanaojitolea kuitumikia hii nchi kwa ku-supply kabla ya kulipwa. Kwa hiyo, Serikali ifike mahali ilipe wananchi hawa wanaotoa huduma Serikalini mapema iwezekanavyo wasiwarudishe nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kuchagua tukubaliane, Serikali inataka kodi, inapenda kodi au inapenda machinga. Tumeruhusu machinga wamemwagika Kariakoo wanauza mpaka milangoni mwa watu wanaotakiwa kutumia mashine ya EFD, matokeo yake bidhaa zinatoka kwenye maduka anapewa machinga anauza, mwenye duka hauzi kwa sababu tayari bidhaa zake ziko kwa machinga. Biashara inaendelea wala yule mtu wa dukani halalamiki kwa nini machinga yuko mlangoni kwake, kwa sababu anajua yeye inamlipa. EFD mashine haitumiki kwa sababu yeye hauzi. Bidhaa zake zinauzwa na machinga. Machinga halipi kodi. Ni nchi gani hii tunayokwenda? Halafu watu wamesimama tu wanaona machinga tunapenda machinga tunapoteza kodi za nchi hii, mwenye EFD pale Kariakoo halipi kodi, bidhaa zake dukani zinakwisha, wanapewa wamachinga….(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)