Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nianze na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Mimi naomba niwaambie Mamlaka ya Mapato Tanzania ni lazima wawe marafiki wa wafanyabiashara, wao wanaona ni ufahari kwenda kufilisi wafanyabiashara, badala ya kutoa elimu unaenda kufunga akaunti ya mfanyabiashara, unaenda kufunga biashara yake, sasa ukishafunga biashara yake wale wafanyakazi hawatafanya kazi mnakosa pay as earn na mnakosa mapato. Naomba muwaelimishe, hata kama mnawadai wapeni muda walipe hicho mnachokitaka kwa muda lakini na biashara iendelee, mkizifunga zile biashara na ninyi pia mnakuwa mmekosa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuhakiki TIN sasa hivi unakuta watu wengi hawaendi kuhakiki TIN zao kwa sababu ukienda kuhakiki TIN unakutana na madeni. Haya yamezungumzwa na wengi, magari yamekaa zaidi ya miaka ishirini, wafanyabiashara unakuta unamdai mtu zaidi milioni 40 lakini mfanyabiashara anapeleka returns kila mwaka, hivi ni kwa nini TRA badala ya kukusanya hayo mapato unamwekea mtu deni mpaka linafika milioni 40 halafu ndiyo unakuja kumpa sasa hivi unamwambia alipe milioni 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu hii kodi ya road licence ingizwe kwenye mafuta na tozo itozwe kwenye magari ambayo yanatembea barabarani, badala ya ku- frustrate watu, kuna watu kule Moshi wamekufa. Utakuta mtu analetewa deni la milioni 200, kuna Mzee kweli kabisa amefariki pale Moshi hajui atalipaje hizo fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ndugu zangu mjaribu kuwafanya wafanyabiashara wawe marafiki zetu na Waheshimiwa Wabunge muelewe kwamba hizi pikipiki mlizotoa kwa wapiga kura mna madeni mnadaiwa huko, hakikisheni mnaenda kubadilisha majina na waelimishwe watu wakiuza kifaa chake au ukimkabidhi mtu kifaa cha moto lazima abadilishe jina. Kuna siku 30 za kubadilisha lakini mtu akishauza lile gari hajui kama kuna umuhimu wa kubadilisha jina, badala yake mnakuja kumwaadhibu yule mtu aliyebadilisha jina mnamwambia alipe lile deni nafikiri hii si haki na siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba niulize kuhusu wale waliopanda mbegu DECI, wale walikuwa ni watu waliojikusanya na kesi ilienda Mahakamani na ikaisha. Kuna zaidi ya shilingi bilioni 14 zimelala pale Benki Kuu. Nataka Mheshimiwa Waziri aje atuleze fedha zile zimeenda wapi au ndiyo mtindo wenu wa Serikali mnazitumia bila kuwaeleza, maana yake hapa tulichanga fedha za maafa Arusha tukasikia zinajenga mochuari Mount Meru. Kwa hiyo, hebu tuelezeni zile fedha ziko wako na ni lini mtawapa hawa waliopanda mbegu fedha zao maana yake kuna wengine wameshafariki. Mheshimiwa Waziri akija ku- wind up atuambie ni lini watawalipa hawa waliowekeza fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie EFD machines. Sasa hivi sijui hizi EFD machines zinatumika wapi na wapi. Kwa mfano, Moshi mpaka wamachinga wanatumia EFD machine lakini hapa Dodoma maduka makubwa tu hawatumii EFD machines na mnajua kabisa mlisema wenyewe, Serikali ilisema itazitoa hizi EFD machines bure, hilo zoezi lilianza Dar es Salaam kwenye mikoa mingine ni lini mtatuletea hizo mashine ili wafanyabiashara wadogo wadogo na wao waweze kutumia hizi EFD machine.

Mheshimiwa Menyekiti, EFD machine moja inauzwa shilingi laki nane mfanyabiashara mdogo ni vigumu sana kutumia shilingi laki nane kununua hiyo mashine. Halafu zaidi ya hilo hizi mashine haziko durable zinaharibika haraka sana, ukitengeneza mashine moja si chini ya laki moja mpaka laki moja na nusu. Sasa ni mfanyabiashara gani mdogo ambaye ataenda kununua mashine ambayo inaharibika kila wakati? Ukizingatia umeme wetu ndiyo huo ikiingiza EFD machine kwenye umeme inaweza ikaungua. Unakuta EFD machine zinaharibika kila wakati na inabidi ulipe hela kwa ajili ya kutengeneza hizo mashine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue utaratibu wenu ukoje. Ni watu gani wanaotakiwa kutumia hizi EFD machines na zinatumika sehemu gani Tanzania, maana yake kuwa Watanzania wanaokaguliwa kila siku na kuna Watanzania wengine wanakaa tu bila kuzitumia. Mheshimiwa Waziri wakati anakuja ku-windup naomba na hilo nalo atuelezee. . (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)