Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Waislam wote nchini kwa kuwatakia mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu. Naomba mchango wangu nimtangulize Mwenyezi Mungu. Nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu wote wa Wizara pamoja na Watendaji wa Wizara kwa kutuletea hii bajeti ili tuweze kuijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Benki ya Wanawake. Tanzania ina mabenki mengi lakini Benki ya Wanawake ni benki pekee ambayo ina wateja karibu asilimia 74 ya wateja wote. Sisi wanawake tunao wajibu mkubwa kabisa wa kuipigania benki hii. Mwaka 2010 Serikali ilitoa ahadi ya kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 10 kwa miaka mitano yaani itatoa bilioni mbili kila mwaka katika Benki ya Wanawake lakini toka ahadi hiyo ilipotolewa ni shilingi bilioni 5.75 tu ambayo imetolewa mpaka sasa hivi. Je, hizi bilioni 4.25 Serikali itatoa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu benki hii tumeona inakuwa ikifanya kazi vizuri sana, karibu mikoa sita sasa hivi imefungua madirisha lakini bado ina kazi kubwa kuhakikisha kwamba benki hii inafungua madirisha katika mikoa yote ili wanawake wote waweze kupata haki ya kupata mitaji kama ambavyo Serikali ilitaka, kwamba wanawake waweze kupata mitaji kupitia benki hii ya wanawake. Sasa nitaomba labda wakati Waziri anahitimisha atueleze na asipoeleza vizuri itabidi tushike shilingi ya mshahara wake ili wanawake wote nchini waone kwamba benki hii inatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuzungumzia kuhusu TIB (Tanzania Investment Bank), naungana mkono na wote waliosema kwamba upo umuhimu wa benki hii kupewa mtaji wa kutosha kwa sababu ndio benki pekee inayosaidia kuleta kwa haraka zaidi maendeleo ya nchi hii. Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda lakini bila kuiwezesha benki hii tutapata shida sana, kwa sababu ndio pekee itakayosaidia kuwezesha miundombinu ya viwanda. Serikali iliahidi kuipatia mtaji shilingi bilioni 500 na tena iliahidi kutoa trilioni tatu lakini ilipatiwa shilingi bilioni 150 tu. Sasa niombe Serikali itakapokuwa inajibu itueleze nini mkakati wa kuhakikisha benki hii sasa inawezeshwa ili huu uchumi wa viwanda uweze kwenda kwa kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Naipongeza sana mifuko hii kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya katika jamii yetu kama ujenzi wa daraja la Kigamboni, ujenzi wa majengo ya UDOM na kadhalika. Niiombe Serikali ilipe madeni ya mifuko hii ili iweze kuendelea kuisaidia jamii na Serikali pia. Kipekee naomba nichukue nafasi hii kuishukuru LAPF, NSSF, PPF na Shirika la Bima (NIC) kwa kuniunga mkono katika programu yangu ya ukarabati wa majengo kongwe kwa shule za msingi katika Mkoa wa Iringa. Niombe na mifuko mingine basi iendelee kutusaidia ili kuendelea kusaidia jamii zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alisema mifuko hii sasa hivi ianze kuwekeza katika viwanda ili isaidie pia na kuongeza ajira nchini. Pia nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama alipokuja Iringa kutembelea kinu cha National Milling alisema kwamba NSSF itatoa mtaji. Najua kwamba ikitoa mtaji katika kile kinu itasaidia pamoja pia na kupata soko kwa wakulima wetu wa Iringa vilevile kuongeza ajira katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia kuhusu madeni ya wazabuni. Naipongeza Serikali kwa kuanza kulipa madeni ya wazabuni kiasi cha shilingi bilioni 796 kati ya deni la shilingi trilioni tatu iliyokuwa inadaiwa, lakini bado wazabuni wengi sana wakimemo wa Mkoa wa Iringa wanaidai Serikali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali ingetangaza katika gazeti ili wazabuni waliohakikiwa na wale waliolipwa madeni waweze kujua, kwa sababu kuna wengi walikuwa wanaidai, lakini hawajui hatma ya madeni yao mpaka leo hii, kama yatawekwa wazi angalau hata sisi tunapokwenda kwenye mikutano maswali yanapungua, wanakuwa wanajua kabisa hatma ya madeni yao ni yapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusu Ofisi ya Ukaguzi (CAG), kwanza niipongeze kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiifanya, ofisi hii inafanya kazi nzuri sana lakini changamoto kubwa ni utekelezaji wa ushauri wa mapendekezo yanayotolewa katika ripoti yake. Bado Serikali hawajaweza kuyafanyia kazi yale mapendekezo ambayo yanatolewa. Vilevile wapewe fedha ya kutosha, kwa wakati na waweze kukagua mapema ili kusaidia nchi yetu panapokuwa na matatizo, tuweze kujirekebisha halafu tuendelee mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu TRA; TRA imekuwa ikifanya kazi nzuri sana tu lakini nafikiri sasa hivi wafanyabiashara wale wadogo wadogo wamekuwa wakikadiriwa kodi kubwa sana hata wale wakubwa kiasi kwamba wanashindwa kufanya biashara zao vizuri. Vilevile kuna utaratibu wa kumkadiria kodi mtu anayetaka TIN ya biashara, anatakiwa alipe kadirio hilo kabla hata ya kuanza biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limekuwa ni tatizo sana, watu wengi wanakwepa kuomba TIN kwa sababu wanakuwa wana mitaji midogo, sasa akijua kwamba akienda pale atatakiwa akadiriwe ile kodi yake kabla hata hajaanza biashara halafu baadaye tena ndio alipie anashindwa kujisajili. Sasa ningeomba Serikali iangalie kwa sababu shida yao ni kurasimisha hizi biashara ili kuweza kupata kodi kwa urahisi zaidi, lakini sasa hii itasababisha biashara nyingi kutorasimishwa, watu wanaogopa kwenda kuzirasimisha kwa sababu wanatakiwa walipe kodi hata biashara zao hawajui kwamba watazifanyaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna utaratibu wa kumtaka mfanyabiashara aambatanishe invoice ya madai kwa mtu aliyempatia huduma kabla hata yeye hajalipwa. Ukitolea tu mfano wale wazabuni wanaofanya kazi na Serikali utakuta kwamba wanapeka invoice lakini kuja kulipwa madeni inachukua muda mrefu sana. Sasa TRA wanataka uambatanishe na ile invoice ya risiti wakati hata bado hujalipwa. Hili pia ningeomba Serikali iliangalie na iweke utaratibu mzuri wa kumsaidia huyu mfanyabiashara ili aweze kufanya biashara yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, utaratibu wa kutaka wafanyabiashara kununua hizi EFDs, nafikiri wenzangu wengi sana wamesema. Mfanyabiashara anakuwa na mtaji kidogo sana, sasa anapokwenda kununua hii EFD tayari mtaji wake unakuwa umeathirika. Kwa hiyo, hata hii niungane na wenzangu kwamba Serikali hebu iangalie uwezekano wa EFDs mashine ziweze kutolewa bure. Nakumbuka hata Mheshimiwa Rais alishawahi kutoa ushauri kwamba TRA wawapatie hizi EFDs mashine wafanyabiashara wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie tu mfano kama TANESCO utakuta TANESCO wanakufungia ile mashine yao kwa hiyo inasaidia, inapunguza hata gharama za kufuatilia. Hii ni kwa sababu tayari mtu anakuwa amefunga ile mashine na hata ile kodi inayokadiriwa sasa inasaidia, kwamba unalipa kweli kodi halali, lakini si kama wanavyokadiria kodi kubwa wakati pato unalopata sio. Kwa hiyo, naomba hizi EFDs ziweze kupatiwa bure kwa wafanyabiashara wote, hata Mkoa wa Iringa bado hatujapatiwa hizi mashine za EFDs. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lile la tax clearance kwa mfanyabiashara anayedaiwa kodi. Naona kama sio sahihi kwa sababu utakuta mfanyabiashara huyu, wengi sana wamefunga biashara zao sasa hivi kwa sababu ya hizi tax clearance. Hii ni kwa sababu wamekadiriwa kodi kubwa ambayo kwa kweli hailipiki na hawa wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara bila kupata faida. Utakuta huyu mkadiriaji bado hajaangalia na bado hajamsikiliza huyu mfanyabiashara matatizo makubwa ya kibiashara anayoyapata. Sasa hivi wengi wamekopa benki na utakuta wengi wao bado wanaidai Serikali na wengi wao bado wana matatizo makubwa kwenye biashara zao. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iangalie sana hawa wafanyabiashara kwa sababu ni sawasawa na ng’ombe… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria muda wa mzungumzaji kuisha)