Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa afya. Pili nawatakia kila la kheri ndugu zetu Waislam ambao wameanza mwezi Mtukufu. Pia nataka kuwapa pole wananchi wa Biharamulo kwa adha inayoendelea huko, sasa hivi ni vurugu tupu baina ya wafugaji na wakulima baada ya hii habari ya mifugo kutolewa hifadhini bila mpango, lakini hiyo tutaisema baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa maana ya hotuba nataka kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima kwa sababu kuna kazi wamefanya ndio maana tupo hapa, vinginevyo tungekuwa hatuwezi hata kujadili, kwa hiyo nawapongeza kwa kazi, lakini tunayo mambo ya kusema kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nitakwenda haraka haraka kwa sababu ya muda nina mambo kadhaa. Ukurasa wa 73 wa hotuba Wizara inazungumzia mafanikio kwa mwaka uliopita na moja ya mafanikio hayo ni kupunguza madeni ya wazabuni na wakandarasi. Wamesema wengi sana waliotangulia, lakini nataka kuweka msisitizo hapa, tunaomba Wizara iwatazame hawa wazabuni na wakandarasi kama sehemu au kama mawakala ambao mbali na kufanya kazi zao ndio wanatusaidia kuwezesha mzunguko wa pesa huko kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, mama mmoja ambaye ndiye analisha shule zetu za sekondari karibu 20 zote pale, huyo ni mfano tu, wako wengi pale wafanyabiashara wa Biharamulo wanaodai pesa na sasa wanaelekea kufilisika. Huyu namchukulia kama mfano, analisha shule lakini hivi tunavyozungumza anaidai Serikali milioni kama 400, imefikia hatua sasa mabenki yanataka kukamata magari yake, lakini watu binafsi wengine ambao wameshamsaidia wao tayari wamekamata magari na rasilimali, amesimama kabisa, yaani ni muda siyo mrefu tunamuingiza kwenye umaskini, tunamaliza mtaji wake wakati ni mtu yeye na wenzake wanashiriki kuwa kama mawakala wa kutusaidia kuzungusha pesa pale, akilisha watu 20 kuna watu anawaajiri pale kwenye kiwanda chake, wanabeba mahindi wanapeleka kwenye mashine, wanapakia kwenye gari, wanasambaza, ni ajira zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa hatumtazami yule mfanyabiashara peke yake, tunatazama mzunguko mzima. Tunaomba mlipe uzito ili haya madeni tuyalipe hata kama hamuwezi kulipa yote angalau sasa naomba Mheshimiwa Waziri tuone namna gani kila mmoja angalau anapunguza ule mzigo ili magari yake yaruhusiwe, mashine zake ziruhusiwe kuendelea, vinginevyo anasimama kabisa na wote waliomzunguka ambao wanapata uchumi kupitia yeye wanasimama kabisa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimeangalia ripoti moja hapa ya Benki Kuu inazungumzia annual growth of banks credit to major economic activities, mengi yamesemwa pale katika chati mojawapo. Interest yangu iko kwenye habari ya kilimo, inaonesha mwezi wa Tatu mwaka huu growth ni minus 9.2 ukilinganisha na 11.2 chanya ya mwaka jana mwezi wa Tatu mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ikanikumbusha nilikwenda siku moja Benki ya Kilimo pale, nimepekela kampuni moja ya binafsi ambayo tunataka itusaidie kushughulika na wakulima wa Biharamulo. Benki ya Kilimo wanatuambia tuna mikoa kadhaa ya kuanzia Kagera haimo, sasa nikawa nashangaa ni namna gani sasa! Hili ndio jambo ambalo linakwenda kushughulika na Watanzania asilimia 80 ambao ndiyo wakulima lakini bado tunalifanya kwa maeneo madogomadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie hapo namna gani wale ambao tuna nia ya kuleta watu watusaidie kwenye uwekezaji wa kilimo tutasaidiwa, kwa sababu benki hii wanatuambia kuna maeneo wanaanza mengine tusubiri. Tusubiri wakati hii ndio ajira ya asilimia 80 ya watu wetu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nataka kugusia kidogo habari ya sekta binafsi, MKURABITA, Hernando De Soto alisema nafikiri ni 2003 kama sikosei mwanzoni mwa 2000 kwamba asilimia 98 ya business transaction kwenye nchi hii zinafanyika nje ya mfumo, kwa hiyo hazilipi kodi na asilimia 90 kama sikosei, figure hizo nitaangalia vizuri, za land property (mali ardhi) iko nje ya mfumo hailipi kodi. Hilo tulishalifanyia uchambuzi kwa kusaidiana na Hernando De Soto ndio ikazaa MKURABITA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, mbona hatuoni mrejesho wa kila tunavyosoma bajeti wa namna gani sasa, MKURABITA imeondoa kwa mwaka mmoja idadi kadhaa ya Watanzania waliokuwa nje ya sekta inayotambulika imewaingiza kwenye sekta, hivyo, hata Waziri wa Fedha atuambie kwa kuingiza hawa sasa tumeingiza nguvu ya kikodi ya kiwango fulani ili mtu akiweza kufuatilia kwa miaka mitano tunaona tunakwenda wapi, naomba maelezo hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne; wenzangu wamegusia, kuna habari ya kukusanya kodi, habari ya kupeleka hela kwenye Halmashauri lakini kuna habari ya kasi ya kuzitumia. Nina mfano mahususi hapa, tuliomba pesa kwa ajili ya maji ya Biharamulo Mjini kutoka Wizara ya Maji, tunashukuru wametupa milioni 200 mwezi wa Kwanza, mpaka leo tunavyoongea mwezi wa Tano huu unakwisha mambo yanakwenda taratibu kama kinyonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza leo na RAS wa Kagera na mtu wa Mamlaka ya Maji Bukoba Mjini, anasema mwanzo kulikuwa na ubishani kati ya Watendaji wetu wa Halmashauri na Mkoani, kwamba Halmashauri wanataka wafanye wao, hawa wanasema haiwezekani hizi hela zitapotea. Hiyo process tu ya kubishana imetumia miezi miwili. Tunaomba Waziri aje na mfumo ambao pamoja na kuzipeleka na kuzisimamia kwa maana zimefanya nini, tuwe na mfumo wa kutazama kasi ya kuzitumia kwa sababu inachangia sana kwenye kukwamisha maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, nimesoma hotuba ukurasa wa 76, tunasema moja ya majukumu ya Wizara; kuweka utaratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini, kufanya tathmini ya miradi ya kuondoa umaskini ngazi ya Vijiji na Wilaya. Hii sasa naleta habari ya ng’ombe na mifugo kule kwenye hifadhi, kwenye muktadha wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kilio cha wafugaji Kanda ya Ziwa na jana nilikuwa Biharamulo ni kwamba tunavyozungumza ng’ombe 11,000 wametaifishwa kwa maana ya kwamba tunawaondoa kwenye hifadhi kwa sababu hawastahili kuwa kule, sina tatizo na hilo. Mimi sio mmoja wa Wabunge wanaotaka ng’ombe wakae hifadhini, lakini swali langu ni kwa nini hatuoni hii kama ni fursa ya kiuchumi? Kwa nini hatujaribu kukaa na wafugaji na wakulima tukawaonesha fursa tulizonazo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nimewahi kusema hapa, nimesaidiwa na UNDP wamefanya tathmini ya uwekezaji kwenye Wilaya ya Biharamulo baada ya kutuambia kwamba sisi ni maskini wa pili. Wakasema mambo mengi lakini nitasema moja tu, asilimia 54 ya eneo letu liko kwenye hifadhi, asilimia 46 ya eneo letu ndio la uzalishaji, lakini hilo asilimia 46 asilimia kubwa ya kutosha ni underutilized, hatujapanga, ardhi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza na Mifuko ya Hifadhi, dada yangu Mheshimiwa Jenista hapa nataka nimshukuru sana, akatukusanyia mpaka Mifuko ya Hifadhi, wakaja viongozi wa Chama cha Wafugaji, wakakaa wafugaji wako tayari, tumefanya tathmini kuna mifugo kama milioni moja kiwango cha chini. Wakasema kila kichwa kichangie elfu 50 tukaona hiyo bilioni 50, tuungane na Mifuko ya Hifadhi tutengeneze viwanda kule, tutengeneze ranchi ndogo ndogo kwa sababu ripoti zinasema tuna underutilized ardhi yetu, tuwaondoe kwa namna ambayo hawatakaa kwenye hifadhi lakini hawataleta vurugu kwa kuwatoa kwenye hifadhi kuleta Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza Biharamulo hatukuwa na migogoro ya wafugaji na wakulima lakini leo badala ya akili ya Mbunge na akili ya watu wengine kuwekeza kwenye kutafuta uwekezaji tunawekeza kwenye kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo haikuwepo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri amesema kwenye ukurasa wa 41 habari ya ubia wa sekta binafsi mpaka wana Tume maalum, watusaidie sasa. Wakati maliasili na kilimo hawajaliona hilo au wanaliona, lakini wanakwenda taratibu waje wao na jicho la uwekezaji ili tukatatue mgogoro wa wafugaji, hifadhi na wakulima kwa jicho la uwekezaji kwa sababu inawezekana, wafugaji na wakulima wapo tayari lakini sisi viongozi ndio tunawagombanisha kwa kutofanya kazi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 75, Mheshimiwa Waziri ameongelea majukumu ya Wizara ya kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera ya uchumi, ndio mambo haya. Uchumi tusiuangalie huku juu tu, twende huko Wilayani watusaidie, tunazungumzia kuondoa umaskini lakini Biharamulo leo tunaongeza umaskini. Mimi pale sasa hivi hotuba pekee ninayopaswa kutoa pale ni kuzungumzia mifugo tu, siwezi kuongelea maji, siwezi kuongelea nini, kuongelea wakulima na wafugaji. Hebu...(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)